Ndugu Rais, kama ilivyo kwa viongozi wetu wa dini wanapofanya ibada
hurudia maneno yale yale na kwa msisitizo ule ule, kuwa tuache dhambi na tumrejee Muumba wetu.
Maneno haya yamekwishatamkwa mara nyingi mno, lakini kwa umuhimu wake hayajawahi kuchosha wala kukifu. Basi na iwe hivyo kwa wosia aliotuachia Baba Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Mhashamu Evarist Marc Chengula. Na sisi tutaendelea kukaririsha na kukaririsha mpaka hapo tutakapobadilika kama yalivyokuwa mapenzi yake. Ikitokea kuwa wosia huu ukashindwa kutubadilisha, basi hakuna neno lingine tunalostahili, bali ole wetu! Na ole wetu sisi kwa maana ingelikuwa bora kwetu kama tusingelizaliwa!
Tunapomlilia Baba Askofu Mhashamu Evarist Marc Chengula tujiulize kwa dhati kabisa kabisa katika vifua vyetu, tutakapoitwa na sisi, tutaliliwa na nani? Tutaliliwa kwa lipi? Hakuna watakaotuona kuwa tulichelewa kuitwa? Katika kutenda kazi zetu hakuna ambao yawezekana tuliwaumiza? Hakuna watakaotamani kufukua makaburi yetu ili wakayapime mafuvu yetu? Ikiwa watatokea wenye visasi tutawasaidiaje watoto wetu na ndugu wengine wakati huo sisi tutakuwa tumegandamizwa na uzito wa mchanga katika makaburi yetu? Kwanini tumelewa na leo kama vile ndiyo siku pekee kuliko jana na kuliko kesho? Tusipungukiwe maarifa na wala mioyo yetu isijae kiburi.
Mwenyezi Mungu alituumba kwa upendo. Akatuacha tuishi katika kupendana huku tukimtukuza Yeye. Ukatili na ujivuni ni kiburi tu cha kishetani. Kuyaendekeza haya ni kutokujua kwetu tu kuwa ni kwa hasara yetu wenyewe. Tumwombe Mwenyezi Mungu atuepushe na haya yasiyompendeza.
Tubadilike na tuwe wanyenyekevu kwa Mungu Muumba wetu na kwa waja wake.
Baba, tulipoongea pale Chuo Kikuu tuliongea kwa kirefu sana, lakini hotuba yetu ilikuwa njema sana. Marehemu Remry Ongara aliwahi kuimba kuwa barabara ‘mrefu’ haikosi kona. Kutamani kufanya kazi na Profesa Lipumba pia lilikuwa ni jambo jema. Hili lingeonekana kuwa ni kona katika barabara yetu ndefu kama lingewapelekea wengine kumkumbuka Rais mstaafu mzee wetu Benjamin William Mkapa. Akiwa rais aliwaambia Watanzania kuhusu maprofesa uchwara. Watanzania hawajasahau. Inakuwa ngumu zaidi kusahau kwa kuwa fujo zinaendelea kuletwa katika nchi na hivyo kuyafanya maneno ya Mzee Mkapa yazidi kuaminika. Inakereketa katika masikio ya wapenda haki kutamani kufanana nao.
Tuliokuwa tunawahutubia ki-inchi rais ndiye baba yao. Lakini watoto wenyewe, wakubwa. Wasisukumwe kuyaamini maneno ya Profesa Mukandala kuwa baba anaweza kuwa analeta chakula nyumbani kila siku, lakini kama mama na watoto hawana furaha huyu hana haki ya kusema amefanikiwa.
Tusikubali watoto wetu watuhesabu pamoja na hao.
Baba na tulipoongea na watumishi wa Mungu kule Bagamoyo pia tulisikika, lakini ni nani atawajibia Maaskofu wale ombi lao?
Kuwanyamazia ni kwa hasara yetu wenyewe. Wakilia walisema, “Tunajua tunakabiliwa na changamoto nyingi. Yesu alisema kama mti mbichi uko hivi, je, mti mkavu. Hakuna masika yasiyokuwa na mbu, ila ikikupendeza Mheshimiwa Rais utupe nafasi ya kukuona kwa baadhi ya viongozi wenzetu wachache ambao watawawakilisha wengine na kukushirikisha changamoto zetu na ijulikane namna ya kuzitatua.’’ Wangeonesha unyenyekevu gani zaidi ya huu?
Mhashamu Baba Askofu Evarist Marc Chengula alisema, “Ujumbe uliokuwa umetolewa na maaskofu ulikuwa haumlengi mtu fulani, bali wanafiki wanaodai ni Wakristo, lakini hawana imani ya dini hiyo ili waweze kubadilika na kuwa watu wema. Narudia, uliwalenga wanafiki wanaodai kuwa ni Wakristo, lakini hawana imani ya Kristu.’’
Aliwataka Wakristo kwa kutumia jumuiya zao ndogondogo kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa mwakani kwa kuchagua watu ambao hawatawafanya waishi kwa kuogopaogopa.
Baba Askofu Evarist Marc Chengula alisema, “Tuangalie, kulialia tu hakuna maana. Tuangalie kabla ya utendaji kitu, sisi maaskofu tumeona udhaifu wetu ni huu, kila mara baada ya uchaguzi ndiyo tunaanza kumchambua mtu na kumtathimini mtu kuwa ataweza au hawezi. Hakuna maana tufurahie watu fulani tumewachagua, lakini tunaishi katika hali ya woga woga, sasa wote tunaanza uchaguzi wa mwaka kesho.’’
Haya maneno yalikuwa ni yake binafsi? Sasa wote tunaanza uchaguzi wa mwaka kesho, ulikuwa ni uamuzi wake binafsi? Maaskofu wakinyamaziwa na hivyo kuhisi kama wamepuuzwa hawatayakumbatia maneno haya na kuyafanyia kazi kuhakikisha katika uchaguzi ujao wanamchagua mtu atakayekuwa tayari kuwasikiliza? Mhashamu Askofu Evarist Marc Chengula kwa kuwapenda Watanzania wote aliwaosia, “Mtakapokwenda kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka kesho na katika uchaguzi mkuu ujao, msichague vyama vya siasa. Chagueni mtu atayekuwa tayari kuwasikiliza. Mchagueni mtu atakayewafanya muishi kwa amani, upendo tena kwa furaha na siyo kwa kuogopaogopa.’’ Hakika makali yao Maaskofu wale yatashinda makali ya upanga.
Wosia wa Baba Mhashamu Chengula utubadilishe ili tuwe watu wema. Tukaeni chini wana wa taifa hili la Mungu, tuangalie anayetuletea shida hii ni nani? Je, tumepungukiwa maarifa au tumejaa kiburi?
Tunashindwa nini kuongea lugha moja wakati wote tunaijua? Mama yetu ni mmoja – nchi yetu Tanzania. Baba ni mmoja tuunganishe wanao. Hakuna atakayeishi milele. Hizi silaha tulizonazo hakuna atakayezikwa nazo!
Na wala tutakapoondoka hatutaondoka na funguo za magereza yote. Tutaziacha na wengine nao watazitumia iwe ni kwa kutufunga au kwa kutufungua. Kwa maana wako wafungwa waliotoka gerezani nao wakawa wakuu wa nchi zao. Na wako wakuu wa nchi waliofia katika magereza ya nchi zao.
Imamu Msaidizi wa Msikiti Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Katanga alisema, “Askofu Chengula alikuwa mshauri mkubwa na alikuwa kiongozi wa kiroho aliyesimama katika ukweli siku zote. Alituunganisha wananchi wa Mbeya bila kujali tofauti zetu za kidini.’’
Baba Askofu Mhashamu Evarist Marc Chengula hatakufa, bali ataendelea kuishi katika mioyo ya Watanzania wote wenye mapenzi mema kwa nchi hii kwa muda mrefu ujao. Amewaachia Watanzania wosia muhimu.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe! Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi na mwanga wa milele umwangazie Ee, Bwana!