Ndugu Rais, mwanadamu mambo yake yanapomwendea kwa ufanisi mkubwa
haombi ushauri. Anaomba ushauri yule ambaye kuendelea kwake kunampatia
wasiwasi. Ndiyo kusema kama tumekubali kuwa tunahitaji ushauri kutoka
kwa viongozi wetu wakuu wastaafu sasa, tunakiri kuwa kuna tatizo
katika kuongoza au kutawala kwetu. Tukishakiri hivyo, tuwe tayari
kutubu.
Baadhi ya viongozi wakuu wastaafu walionekana dhahiri kuwa hawakujua
walichoitiwa. Waliposema waliishia kumsifia na kumpongeza rais.
Anapongezwa mshindi. Amepigana akashinda. Huyu ndiye kwanza anaanza
mapambano haijulikani atayamaliza vipi. Busara ingekuwa ni kumtia
shime. Waliompongeza rais kwa dhati kabisa kabisa walikuwa hawajui
watendalo. Ila kwa baadhi ilikuwa ni unafiki wao tu.
Ndugu Rais, ushauri uliotolewa ulikuwa mzito ambao kama utazingatiwa
tunaweza kurudi katika hali ya utangamano na Watanzania
wakaifurahia tena nchi yao kama zamani. Na ni hapo tu maendeleo katika
nchi hii yanaweza kupatikana.
Mama Anne Makinda na Mzee Bejamin Mkapa walisema kitu kimoja, lakini kila huyo
kwa namna tofauti. Wakati Mama Anne anasema anasikia karaha kusikia
kila kitu, rais kasema hivi, rais kaagiza hili, rais, rais….Mzee Mkapa
anasema rais ni wa CCM. Awamu ya Tano ni ya CCM. Serikali ni ya CCM.
Ina maana naye anasikia karaha kusikia kila kitu changu,
changu….serikali yangu, utawala wangu, na yangu nyingine nyingi.
Tumetanguliza mno u-mimi.
Ununuzi wa ndege ni jambo jema sana, lakini wakosoaji wanapata heshima mbele ya wananchi kwa sababu fedha zilizotumika inadaiwa hazikuidhinishwa na Bunge. Ni fedha za walipa kodi. Kutumika nje ya utaratibu wa Bunge ilikuwa ni makosa
makubwa. Waliotii maagizo nje ya utaratibu wanapaswa kuadhibiwa hata
kama siyo leo. Viongozi wakuu wastaafu wameonyesha kutoridhishwa
kuiona nchi ikiongozwa kwa kutotumia akili za watu wengi.
Ndugu Rais, ushauri wa Mzee John Malecela una umuhimu mkubwa. Amesema
busara ni viwanda vilivyojengwa na serikali zilizopita, vifufuliwe.
Akatolea mfano kuwa kiwanda kikubwa duniani cha kusokota kamba za
mkonge kiko Tanga. Na kwamba Tanzania ndiyo nchi iliyokuwa inaongoza
katika Afrika Mashariki kuwa na viwanda bora na vingi vya nguo.
Wajenzi wa viwanda hivi vipya hili hawakuliona.
Muulizeni Mzee Joseph Mfugale wa Peacock Hotel mchango wa vitenge vya
MWATEX katika miaka ya 1970. Shati langu la MWATEX ninalo mpaka leo
na uzuri na ubora wake haujachuja. Nililinunua nilipopita Mwanza kwa
mara ya mwisho mwaka 1975. Kwa uzuri wake lilinivutia watazamaji wengi
kila nilipolivaa; si Dar es Salaam tu, bali hata Nairobi nchini
Kenya.
Miaka ya sabini nikiwa naishi Mtoni kwa Aziz Ali mara nyingi
mboga yetu ilikuwa ni nyama iliyosindikwa vizuri na kiwanda cha
Tanganyika Packers. Sasa vyote hivi vimekwisha kwenda. Imebaki ni
historia. Mzee Malecela anashauri viwanda hivi vifufuliwe. Ni busara
tukauzingatia ushauri wa kuvifufua viwanda hivi. Tusipoanza sasa
kuvifufua viwanda hivi, mkutano wote ule utaonekana ulikuwa ni ubatili
mtupu.
Labda Mzee Mwinyi alimwita Mstaafu Nyerere kwa siri, lakini Nyerere akiwa
kijana tu wa miaka 38 alikuwa anamwita mstaafu yupi kwa ushauri?
Nchi gani hii iliyojaa kelele za kulazimisha vyerahani vinne
kuwa ni kiwanda? Baba, vijana wako kwa kuganga njaa kwao wameifanya
kaulimbiu yako njema sana ya Tanzania ya Magufuli itakuwa ni ya
viwanda kuonekana ni mzaha unaoigharimu nchi fedha nyingi. Hapana,
hapana Baba.
Ndugu Rais, unapendeza sana unaposema ukweli. Umewasifu viongozi wakuu
wastaafu huku taifa likikusikia kuwa walimpika vizuri sana Edward
Ngoyayi Lowassa. Ukasisitiza kuwa Edward Lowassa ni mwanasiasa
mstaarabu sana. Tunapowasifia wengine kwa ustaarabu tukumbuke
kujifunza ustaarabu huo kutoka kwao. Kuna kijana sikumbuki vizuri jina
lake, au anaitwa Mtinga, au Mkinga, au Mjinga, ukimtaja Edward Lowassa
tu anasema amekununua. Edward ana mfuko mpana kiasi gani? Ni bahati
nzuri hawa waliojitia uewendawazimu huu katika nchi hii ni wachache.
Busara kubwa na hekima yake Edward aliyoitumia baada ya matokeo ya
uchaguzi mkuu kutangazwa ndiyo iliyoifanya nchi hii ibakiwe na angalau
na haka ‘kaamani’ kadogo ambako nako tunakachezea. Kistaarabu kabisa
Edward ameonya kuwa hata hii amani ndogo iliyopo nayo itapotea ikiwa
baadhi ya viongozi wataendelea kusema maneno ya hovyo bila kuyapima.
Mwingine angesema baadhi ya viongozi ni waropokaji tu. Kwa kuwa ni wewe
baba uliyetuonyesha kuwa Edward Lowassa ni hazina muhimu kwa nchi hii,
basi anayeona tofauti na baba, hana adabu. Kama hatuna ugomvi na
shangazi wa wenzetu, tuwaheshimu. Nikisema amueni nami nitawaunga
mkono nimeyapima, sikuyapima? Kwanini tujihisi kutukanwa kila mara na
kila mtu? Katika marais wote waliotangulia ni sisi tunaongoza kulia
kuwa tunatukanwa na wananchi wetu. Tuwaache wananchi waseme. Kama mtu
anazuia midomo ya watu kuzungumza kuhusu mambo mema anayowatendea, kwa
namna yoyote anajua kwamba hana jema analowafanyia watu wake.
Nimewasikia baadhi ya wapinzani wakisema, “Serikali imetumia mabilioni
ya fedha kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Uwezo
wa bomba tunaoutumia ni asilimia 6 tu. Tukiweza kulitumia kwa
asilimia 25 tu, tutatengeneza umeme mwingi kuliko wa Stiegler’s Gorge
tunaotaka kuutafuta kwa matrilioni ya mapesa. Baba kuna tusi gani hapa!
Baba wa Taifa katika kitabu cha nukuu za Kiswahili za Mwalimu Nyerere
anasema, “Wananchi wanapoonyesha uamuzi wa kipumbavu, wanatumia haki
yao ya kiraia. Wanaponung’unika kwa uamuzi ambao si wa kipumbavu
wanaweza wakaelekezwa mpaka wakaelewa kwanini uamuzi ule ulifanyika,
na faida zake ni nini”. Kwanini hawa hawaelekezwi ili wajue kuwa uamuzi
huu si mbaya? Badala yake anatokea kiongozi mwenye mawazo ya
Tumbusi na kusema, “Piga, ua, galagaza na watakaobishia tutawafunga