Ndugu Rais maandiko yanasema katika nchi yoyote hapa duniani, wenye hekima na busara wakinyamaza, wapumbavu na wajinga huongezeka na nchi ikaangamia!
Kwa udhaifu wake mwanadamu anajiuliza, kwanini basi katika kuumba ulimwengu Mungu aliumba na wajinga na wapumbavu na akawaweka katika nchi zote alizoziumba hapa duniani?
Hayo ni makusudi ya Mwenyezi Mungu mwanadamu anaweza asiyajue. Kwakuwa tunakatazwa kuweka alama ya kuuliza pale Mungu mwenyewe alipoweka alama ya kituo, basi jina lake lihimidiwe!
Lakini Mwenyezi Mungu huyohuyo alijiumbia wanadamu aliowajaza hekima na busara ambao nao aliwaweka katika kila nchi aliyoiumba hapa duniani. Kazi yao ni kuwadhibiti wajinga na wapumbavu wasiongezeke katika nchi.
Hivyo wenye hekima na busara katika nchi yoyote wakinyamaza wajinga na wapumbavu huongezeka na kuifanya amani ya nchi hiyo kupotea!
Ndugu Rais kama zilivyo jamii zingine Watanzania nao pia wana viongozi. Wako viongozi waliochaguliwa na wananchi wenyewe kwa kura zao. Kati yao hao wote hakuna hata kiongozi mmoja ambaye mtu timamu anaweza kumweka katika kundi la wendawazimu.
Wako na viongozi wa kimila. Kwakuwa hayo ni makubaliano ya jamii husika kwa hiari yao wenyewe basi hiyo ndiyo maana ya neno demokrasia. Kuna wanaoitwa viongozi wa dini. Sijui ni kwa nini hawa jamaa wanakubali kuitwa viongozi. Kiimani hawa ni wachungaji wa waja wa Mwenyezi Mungu.
Wakati kiongozi hutangulia mbele, Mchungaji mwema hukaa nyuma ya mifugo yake akihakikisha ulinzi na usalama na kwamba hakuna anayepotea! Ndiyo maana tunasoma kuwa Bwana Yesu hakusema kiongozi mwema bali alisema Mchungaji mwema ni yule aliyetayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake!
Wako na viongozi ambao si viongozi. Jana tu walikuwa wanawaambia wananchi kuwa nchi yao inaongozwa kama gari lililokatika usukani. Leo kuitwa Ikulu kidogo tu wanasema uongozi huu ni imara kama sunami.
Lakini wako na watu walioteuliwa halafu wakapelekwa wakawatawale wananchi wapende wasipende! Wanapelekwa kuangalia maslahi ya yule aliyewapeleka si ya nchi wala si ya wananchi.
Hawa, pia hawana mapenzi ya kweli kwa yule aliyewateua kwasababu ikitokea yeyote akakalia kiti kile, watamwitikia, ‘Ewala Maulana!’ Hawa ni watu wa mshahara tu! Hapendwi mtu hapa.
Hawa kuitwa viongozi wa watu ni kuitukana demokrasia. Mteule kujifanya anawapenda watu asiowajua ambao nao kwakuwa hawamjui au wanadhani alipitia njia za panya kufikia hapo alipofikia hivyo hawawezi kumtaka, ni unafiki mkubwa!
Kuwafanyia ziara ya kusikiliza kero zao ni kichekesho cha mwaka! Uchungu kwa kero za wananchi wanaupataje, wasiupate kwa yule aliyewateua? Bwana Yesu aliwalaani sana wanafiki! Ni kweli baba anasikia uchungu kumwona mke wake akiugulia kwa uchungu wa kujifungua, lakini je, na huo uchungu wa baba nao huwa ni sawa na uchungu wa kujifungua?
Ndugu Rais katika Mapendekezo ya Mabadiliko ya Katiba Mpya katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu ukurasa wa 110 imeandikwa, “Hakutakuwa na Liwali mkoani (mkuu wa mkoa) wala wilayani (mkuu wa wilaya). Viongozi watachaguliwa na wananchi wenyewe katika uchaguzi mkuu. Wataunda serikali zao ambazo zitakuwa chini ya Serikali Kuu.”
Tupende tusipende uko umuhimu mkubwa wa nchi kuwa na katiba mpya tena mapema. Waliouchafua mchakato wa kupatikana katiba mpya wengine sasa hatunao.
Wako mbele ya Muumba wetu! Ndugu yetu Samweli Sitta alipata fursa ya kukumbukwa kama Spika aliyeipatia nchi hii katiba mpya, lakini aliiachia hiyo fursa, nayo ikaanguka. Kwakuwa ametangulia mbele ya haki, sisi si wenye kuhukumu!
Tumwachie Mwenyezi Mungu ampatie haki yake! Amani ya nchi hii iliwekewa misingi imara na madhubuti na viongozi wenye hekima na busara kubwa ambao nao wametangulia mbele ya haki.
Walitujengea upendo, umoja na mshikamano kuwa ndiyo nguzo kuu ya umoja na amani yetu ambayo leo wajinga wachache wanaitikisa kwasababu wenye hekima walioko juu yao wamenyamaza.
Ni kweli hakuna mwenye uthubutu wa kuwakemea hawa? Waziri Mkuu wetu Kassim Majaliwa Mwenyezi Mungu amtie shime aendelee kuwakemea wote wanaoendekeza utoto na upuuzi!
Mwenyezi Mungu alitujalia amani bila sisi wenyewe kumwomba. Lakini yanayoendelea nchini mwetu hivi sasa na hasa mikoa ya Dar es Salaam na Arusha vinaashiria kuwa wenye hekima na busara wamenyamaza.
Imeandikwa kuwa wakiachwa hawa waongezeke, Watanzania wanaweza wakajikuta wanashuhudia ghasia ambazo jicho halijapata kuyaona, wala sikio halijapata kuyasikia!
Ndugu Rais Mwenyezi Mungu ambariki Waziri mkuu wetu Kassim Majaliwa kwa kuliona hili kwa wakati na kukemea utoto huu palepale. Baba Majaliwa kwa ujasiri wako wa kukemea utendaji wa kipuuzi na utendaji wa kitoto, matumaini ya Watanzania yamebaki kwako!
Mwenyezi Mungu akufanyie wepesi uanze nao mapema ili uwarudishie Waja wa Mwenyezi Mungu wa nchi hii urithi wao walioachiwa wa upendo, umoja na mshikamano! Ni katika hali ya amani na utulivu tu ndiyo nchi inaweza kupata maendeleo ya kweli ya watu; siyo maendeleo ya vitu!