url-4Ndugu Rais dhamira yako njema kwa nchi yetu na watu wake wanawema wote wanaiona. Ugumu uliopo mbele yako katika kutekeleza dhamira hiyo njema pia wanawema wanauona. Umesongwa na kuzingirwa kila upande.

Umefanana na waridi lilisongwa na michongoma yenye miiba mikali au ndama aliyezaliwa katikati ya wanyama wakali baada ya mama yake kukimbia. Pamoja na yote hayo nakwambia usiogope! Msujudie Muumba wako kwa maana kwake hakuna lisilowezekana!

Ndugu Rais, wakati Watanzania bado wanamshangaa Naibu Spika Tulia Ackson kwa hitimisho lake tata la kuipa Serikali miezi mitatu kwenda kusimamia utekelezaji wa mkataba tata kati ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises, umekuja na kashfa nyingine ya kufanana na hiyo ndani ya Jeshi hilo hilo la Polisi. Umeliambia Taifa kupitia kuapishwa maafisa wa polisi kuwa: “Kuna minong’ono kwamba mwishoni mwa mwaka jana kuna mtu amelipwa fedha, wengine wanasema bilioni 20, wengine bilioni 40 na wengine wanasema bilioni 60 kwa ajili ya sare za polisi, lakini hakuna hata ‘unifomu’ moja iliyokabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.”

Ukahitimisha kuwa: “Nina uhakika Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba), IGP (IGP ni Ernest Mangu) na Katibu Mkuu, (Jaji, Meja Jenerali Projest Rwegasira), mmenisikia na nategemea siku moja hao wahusika wakuu watapelekwa mbele ya haki”.

Uliyatamka maneno hayo kwa upole na unyenyekevu mkubwa na hivyo ukavuta hisia nyingi za huruma! Hukuamuru kama tulivyokuzoea, badala yake ulisema: “Nategemea siku moja hao wahusika wakuu watapelekwa mbele ya haki”. Ulijipa imani kuwa; kwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, IGP na Katibu Mkuu wamesikia ulivyosema, basi labda watachukua hatua! Wananchi wanajiuliza, ina maana hao viongozi wakuu watatu walikuwa hawalijui hilo? Au walikuwa wanasubiri hadi Rais aseme? Kwanini baba hukuagiza wahusika wapelekwe

mbele ya haki? Kilikosekana kipi mtu asitumbuliwe?

Ndugu Rais, ulikuwa mnyenyekevu mno kiasi kwamba ulionekana kama mchovu

mithili ya mtu anayepandisha mlima kwa baiskeli. Laiti ingekuwa ni enzi za hayati Edward Moringe Sokoine, pangechimbika! Nakuapia baba, pale zisingezidi siku saba wahusika wangekuwa mbele ya haki! Hivi majuzi umemrudisha Augustine Mrema Wizara ya Mambo ya Ndani. Wengine

wanasema kwanini usingembadilisha na mmoja kati ya hao watatu uliowataja? Na yeye aliitwa bwana siku saba.

Ndugu Rais siku saba siyo ukali! Siku saba ndiyo nidhamu ya kazi katika polisi! Polisi aliyetimia anafanyakazi kwa kutii amri. Staili uliyokuja nayo ya kutumbua majipu ndiyo inayowafanya wengine

wajiulize, pale uliona uzito gani? Kama na wale wakubwa waliona kuwa uliona ni pazito unatarajia nani afikishwe mbele ya haki? Waziri wetu pale atasema ni mpya, simlaumu. Lakini angekuwa ni mtu wa mchakuro kwa siku alizokaa pale angekuwa na mkanda mzima. Asingekubali useme

‘nategemea’. Angekufanya useme: “Nafurahi wahusika wakuu wamepelekwa mbele ya haki”. Ndugu Rais, yawezekana vipi mtu akalipwa mabilioni fedha za Serikali bila viongozi wakuu hawa kujua? Halafu asishone hata shati moja, pia wasijue? ‘Dili’ hii ingefanikiwa vipi bila watu

kushirikiana? Na siku polisi watakapokuwa ndiyo wezi wetu, watakamatwa na nani?

Ndugu Rais, IGP lazima akujibu swali ulilouliza, “Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, Ofisi ya IGP iko palepale, Ofisi ya DCI iko palepale, makamishna wote mnazunguka mnakwenda pale pale, mwizi naye mnaye palepale, mnashindwaje kumshika?”

Ni jukumu sasa la Jeshi la Polisi kuwaaminisha wananchi kuwa wao polisi si sehemu ya hao wezi na majambazi na wala si washirika wao. Utamshikaje mwizi uliyeshirikiana naye kuiba? Huko si kujishika mwenyewe!

Anayesema IGP alikuwa haujui wizi huu atakuwa anautilia shaka uwezo wa kipolisi wa IGP. Anayesema alikuwa anaujua atakuwa anautilia shaka uadilifu wa IGP. Moja kati ya hilo lazima liwe na ukweli.

Ndugu Rais, Lugumi Enterprises anatuhumiwa kulipwa Sh bilioni 34 ili afunge mashine 108 za kuhifadhia alama za vidole kwenye vituo vya Polisi, lakini mashini zilizofungwa zilikuwa ni 14 tu.

Naibu Spika Tulia Ackson ameipa Serikali miezi mitatu iende ikatekeleze mkataba huo kati ya Lugumi na Jeshi la Polisi. Kilichofanyika hapa ni wizi. Ilitakiwa ijadiliwe ili wahusika wachukuliwe hatua. Watuhumiwa hapa ni polisi ambayo ni Serikali kwa upande mmoja na kampuni ya Lugumi kwa upande mwingine. Tulia angetulia kwanza ili, awaambie wananchi alipotoa miezi mitatu kwa mmoja wa watuhumiwa, yaani Serikali kwenda kusimamia utekelezaji wa mkataba huo, katika kichwa chake alikuwa anamlenga nani ambaye kwake mtu huyo ndiye anaitwa Serikali? Tulia aelewe kuwa hata kama watakubaliana wakazifunga zote bado hawatakuwa wameondoa kosa walilotenda.

Uamuzi kama huu hauonyeshi busara kwa sababu unatoa picha kuwa kuna baadhi ya watu hata wangefanya ufisadi mkubwa na wa kutisha tena wazi wazi kama huu, hawawezi kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kutokana na mazingira waliojitengenezea wenyewe. Hii ni hatari kwa

amani ya nchi kwa sababu hawa wanaoibiwa na wanaoonewa sasa hawatakubali kuonewa na kuibiwa milele.

Ndugu Rais, hali ya Jeshi la Polisi kama ndiyo hii, usije ukashangaa utakapotokea msululu wa ‘Lugumi’ nyingi! Kwa maneno yako umesema: “Kuna wachache ambao inawezekana ni asilimia 0.0001 ya watendaji ndani ya Polisi ambao kwa makusudi au kwa nia yao mbaya wanalichafua Jeshi la Polisi, nawaomba mkawashauri, mkawaelekeze na ikishindikana mkawaondoe katika Jeshi la Polisi, nayasema haya kutoka moyoni na msema kweli ni mpenzi wa Mungu.”

Hapa ndugu Rais tusaidie; watakapotwambia kuwa, hiyo asilimia ndogo uliyoisema wewe, kuwa ndiyo inayolichafua Jeshi la Polisi, ni ofisi ya

IGP; tukitaka kuwapinga tuwape sababu gani? Baba nilikuomba utengeneze Polisi yako! Elewa kuwa katika hili, umesimama peke yako! Hata hivyo, Mungu atakupigania kwa sababu unawapigania waja wake!