image001Ndugu Rais, wako wapi wale viongozi wenye fikra nzito? Fikra zilizo juu ya vyama vyao vya siasa? Fikra sahihi kama za Baba wa Taifa aliyewafanya Watanzania kusema ‘nchi yangu kwanza?’. 

Fikra zilizowafanya wanawema wa nchi  hii kuiona nchi hii ni moja na ni yao wote katika umoja wao? Liko wapi lile Bunge la chama kimoja? Bunge la sasa halimtamanishi mtu yeyote timamu. 

Wako wapi wagombea urais, wagombea ubunge na udiwani waliopanda gari moja na kuhutubia katika jukwaa moja? Ah! Fahamu umewatoka uanadamu umeenda kwa wanyama. Wakuja wamekuja na sasa wanawaita waliowapokea eti ndiyo wakuja. 

Wameifilisi nchi, na kupandikiza chuki kati ya watu wa Mungu na sasa wamejaa hofu. Tumwache Rais wetu afanye kazi yake.

Wametoka wapi hawa waliopoteza hofu ya Mungu? Wametoka wapi hawa wasioogopa hata mauti? Tunaelekea shimoni, waliopaswa kutuongoza wanaongea upuuzi wa vyama vyao vya siasa. 

Mbele yetu imejaa giza totoro. Harufu inayosikika imejaa damu, ndugu Rais ni nani kama si wewe wa kusimama hili Taifa lipone?

Mwana wa kipanga ni kipanga. Wananchi wa Mleni, Kibatini Kata ya Mzizima mkoani Tanga, wanaishi kwa hofu kama vifaranga vya kuku vilivyokimbiwa na mama yao mbele ya mwewe baada ya Polisi waliokuwa wakiwalinda kuondolewa. 

Hatari imekwisha vipi bila wahalifu kukamatwa? Mapango hayaingiliki badala yake wanarudi kwenye nyumba zao ishirini-ishirini walizojijengea. 

Na humo ndimo wanamotangazia kupiga marufuku kwao kutembea wala kukutana kwa wanaotaka kutimiza kilicho haki yao. Mapangoni watu hawazidi kumi na watano lakini mapambano yao, zaidi ya saa kumi na tano. Sasa kudhani kuwa unaweza kuzuia mafuriko kwa mikono nia yake inatofautiana vipi na nia ya kutaka kuchinja?

Tumwombee Rais wetu atumie busara katika hili ili amani katika nchi yetu ipate kudumu. Kwa nini kila mtu anatoa amri zake katika nchi hii?

Hawa ndiyo viongozi wetu waliouza sehemu ya nchi yetu, kiwanja ambacho wengine walikiita Oysterbay Police, kwa wageni. Hawa ndiyo wanaotuletea habari za mkataba nyongefu wa Lugumi.

Polisi wetu na wahalifu wetu waliokuwa wanapambana kwenye pango la Mwanza walikuwa hawafukuzani. Hawa walikuwa nje ya pango na wale ndani ya pango. Baada ya mapambano yaliyochukua zaidi ya saa 14 eti majambazi wote walifanikiwa kutoroka isipokuwa watatu waliotolewa mhanga. 

Watakosa kutoroka vipi wakati wewe unatumia silaha za kudungulia ndege angani kwa watu walio nyuma ya mawe? Ndugu Adadi amesema huu ni ugaidi kwa kuwa ni zaidi ya ujambazi. 

Wanaodhani kulikuwa na mazungumzo ya kukubaliana namna ya kuyamaliza tuwakatalie vipi?

Ndugu Rais, kuna kila dalili za kufanana kwa matukio ya Mwanza na Amboni, Tanga. Sehemu zote mbili wahanga walichinjwa, watoto wakakamatwa na makazi yao ni mapangoni. Polisi wamejipanga vipi katika kujua nini kiko nyuma ya haya yote? 

Lakini Polisi wamejipanga vipi kuwaaminisha wananchi kuwa wao siyo washirika wa hao wauaji? Mke wa marehemu Mkola aitwae Asha Said wa kule Kibatini Tanga, anasema alisikia mtu anapiga hodi mara mbili na kusema ‘toka nje mpumbavu wewe’.

Mume wake alipofungua mlango walimpiga na kumtaka atoe fedha. Akasikia wakimwambia kuwa yeye ndiye aliyepeleka taarifa Polisi akishirikiana na kaka yake. Kwa hili polisi wanatakiwa walifafanue vizuri kwa wananchi kwa sababu kama itathibitika kuwa wauaji walipata majina ya wananchi waliotoa taarifa Polisi kuhusu uwepo wa wauaji hao kutoka miongoni mwa Polisi, watavunja nguvu za raia wema wanaotoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Polisi.

Mjane mwingine wa marehemu Issa Hussein, Mwanaisha Amir, anasema “Sisi tumehama Kibatini kwa sababu Jeshi la Polisi limewaondoa Polisi wake, na tambua kuwa tulikuwa na wanaume sasa tupo wenyewe, hivyo ni rahisi kudhuriwa au kuuawa na sisi”. 

Anasema tangu kutokea kwa tukio hilo, wamekuwa wakiishi kwa hofu kwani bado wanaamini kuwa upo uwezekano wa tukio hilo kurudia ikizingatiwa kuwa vijana wa wavamizi hao bado wanashikiliwa na Polisi.

Polisi lazima waje na maelezo ya kina. Kufichaficha mambo mazito kama haya kwa sababu za kipuuzi huu si wakati wake. Wako wanaojiuliza Polisi wanangoja mpaka achinjwe nani?

Ndugu Rais, kumbuka busara za Baba wa Taifa ulipotokea wakati wa majaribu kama huu. Wakati Polisi wa Mwinyi wakihaha kumdhibiti Augustino Lyatonga Mrema na wafuasi wake, alisema kidogo tu kuwa kama kuna mtu anapenda kubebwa, na wanaombeba wapo, waacheni wambebe hata kama watakuwa wanapokezana kama jeneza (mwacheni abebwe kama maiti). 

Tangu siku hiyo biashara ya Mrema ikaanza kuporomoka. Leo, Baba wa Taifa hayupo. Tumebaki sisi mawe tunapiga kelele. Baba aliyepo ni wewe ndugu Rais; kama kuna watu wanapenda mikutano, na kama wa kuwasikiliza wapo, waacheni wafanye mikutano. Sheria za nchi si zipo? Wananchi watawapima. Hao wanaosema mikutano marufuku ndiyo hao hao wenye nyumba arobaini arobaini.

Ndiyo hao hao waliouza viwanja vya Polisi kwa wageni. Ndiyo hao hao wanaohangaishwa na bilioni 37 za mkataba wa Lugumi. Watapata wapi muda wa kulinda msikiti kule Mwanza waumini wasichinjwe, mapango ya Amboni halafu na waandamanaji? Baba, wewe huna cha kuficha? 

Kazi unayoifanya wananchi wanaiona. Waache wananchi wakapime. Na ninyi mlioamua kufanya mikutano nchi nzima mnapotangaza kwa mabaragumu mnamtisha nani? Wenzenu wanaweweseka.

Ndugu Rais. Mrema wakati wake alihofiwa sana na wenye mamlaka. Mativii yalipoanza kuonesha watu wa Burundi wakichinjana, alionya akasema, “Hawa hawakuzaliwa wanachinjana.” Amri za hovyo hovyo zikitolewa na watu wa hovyo hovyo ndizo zinazofanya watu kuchinjana. Zinawaondolea wananchi imani wakati kazi ya imani ni kuwezesha pale elimu iliposhindwa.