Ndugu Rais, kusema ni kukiri na kukana kwa wakati mmoja. Walisema unapokiri kuwa hili ni dirisha, labda hata bila wewe mwenyewe kujua unakataa kuwa huo si mlango, wala si kitu kingine bali unakiri kuwa ni dirisha. Hivyo ndivyo ilivyo akili ya mwanadamu.

Baba, kama kuna kitu ulikuja nacho kilichotuvutia wanao wengi ni ujasiri wa kusema ‘ninaweza’ uliouonyesha katika kupambana na ufisadi, hivyo ukawajengea watu wako imani kubwa sana juu yako. Miradi uliyoianzisha ni mikubwa sana. Ikikamilika kikamilifu nchi yetu itang’ara kushinda nchi zote.

Lakini ndiyo tunaianza. Bado iko katika kufikirika. Kusifia miradi iliyoko katika hatua ya kufikirika kunaonyesha uchovu wa fikra za wanaosifia. Watu wa aina hii hawawezi kuwa timamu. Mradi kuanza na kuishia njiani ni jambo la kawaida katika maisha. Tunayo mifano mingi ya miradi iliyoanzishwa na waliotutangulia ambayo imekwama mpaka leo. Miradi mikubwa, hasa hii inayotumia fedha za kuokoteza kukamilika kwake ni majaliwa.

Hivyo ujasiri ulioanza nao pale juu ya Daraja la Mwalimu Nyerere, Kigamboni kwa kumtumbua marehemu Wilson Kabwe japo ulikosewa sana na kusikitisha na kuwaliza wengi hadi leo, lakini ulitoa alama kuwa huko tuendako kwa ufisadi hakuna mzaha tena. Lakini leo wananchi wanashuhudia kitu tofauti kabisa!

Tuliukuta mradi wa gesi uliokuwa unaendelea vizuri. Wengi walidhani mradi wa gesi ungegawiwa fedha kidogo tu kati ya hayo mengi yanayomwagwa leo baada ya miaka minne Tanzania ingekuwa nchi nyingine kabisa katika Afrika. Miradi mingine yote tungeitimiza bila kumfukuza jogoo wala kuwachubua ngozi watu wetu. Wala tusingekuwa na shida ya kufukuzana na vijitu vidogovidogo vinavyosema vyuma vimekaza.  

Mlezi mwema hawakatazi wanaye kusema wana njaa. Kuwakataza watoto kusema wana njaa wakati ukweli wana njaa ni ukatili mkubwa wa mzazi asiyetosha. Lakini kwa muda wote wa miaka yetu minne wananchi wamenyimwa fursa iliyojitokeza ya kujifungua kutoka katika minyororo ya umaskini kwa kubaniwa mradi wa gesi.

Wakati huu tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu tutumie muda mwingi kutafakari. Labda kwa sababu tumelitaja mno jina la Mungu mpaka wengine wametuona tumelifanya kichaka, basi tutumie utu tu wa kawaida kujiridhisha kwanza sisi wenyewe kama miradi yote hii mikubwa na miujiza yote hii tuliyoianzisha kuna hata mmoja unaoyagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, hivyo kuwapunguzia uzito wa mizigo yao mitatu walioambiwa na Baba yao wa Taifa; yaani ujinga, maradhi na umaskini?

Shule zimefunguliwa, michango imezidi ile ada iliyokuwa inatolewa kabla ya kufutwa, huku madarasa na madawati yakiwa yamepungua kwa kiasi kikubwa. Serikali ilipokuwa inalitangazia taifa kuwa hakuna michango tena, ilikuwa inamdanganya nani? Tujipange vema kwa sababu wakati wa kutakiwa kujibu haya maswali ni sasa.

Bajeti ya Wizara ya Elimu kwa kipindi chote cha miaka yetu minne fedha zote iliyoomba na kuidhinishwa na Bunge haikuwahi kupunguzwa hata shilingi moja. Iweje kuwe na upungufu mkubwa wa madarasa na madawati nchi nzima kama vile wanafunzi wameshuka kama mvua kubwa iliyoshuka ghafla?

Mzee wangu kaniuliza, hawa waliofanikiwa kuzuia misaada kutoka nje kuja kuwasaidia wananchi, je, hawajui kuwa wanaoumia ni wananchi? Wanawapenda kweli Watanzania? Nikakumbuka Nyerere alipokuwa anaizunguka dunia kuitaka izuie misaada kwa Afrika Kusini wakati wa ubaguzi wa rangi, jibu la Makaburu lilikuwa moja, ‘watakaoumia ni wananchi weusi’. Kwa kuwapuuza hao, Nyerere alionyesha uzalendo wa kweli kwa nchi za Afrika.

Wizara ya Afya nayo bajeti yake haijawahi kupunguzwa hata kidogo katika miaka yote hii yetu minne. Iweje wananchi waendelee kuziacha maiti za wapendwa wao zizikwe na City kwa kukosa fedha za kuzikomboa kutoka katika hospitali zetu? Ni upi katika miradi yetu yote hii unaowaondolea wananchi machungu haya hivi sasa? 

Kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliposema: “Maendeleo ni lazima yawaguse watu” alikuwa anasema kweli, na kama ni kweli kuwa katika miradi yetu hii hakuna inayogusa watu, sisi sasa tuseme nini? Je, tukiri kuwa kwa fikra za Baba wa Taifa hakuna maendeleo tuliyoifanyia nchi yetu? Tusikae chini kuanza kulia kwa kuipoteza hii miaka minne, tukae chini tuwatafutie wananchi majibu!

Wastaafu wa TTCL tunaodai nyongeza ya Sh 50,000 walioidhinishiwa na Bunge baba ukiwa waziri, sasa tumebaki wachache sana, ni vema ukatulipa sasa kabla hatujamalizika wote ili tukuombee nawe utakapopita upite kwa amani. Wasije kutokea wa kujisikia afueni kwa kupita kwako!

Bunge liliamuru kima cha chini cha pensheni kipande kutoka Sh 50,000 hadi Sh 100,000 kwa wastaafu wote. Wengine walipandishiwa lakini tuliokuwa tunatokea TTCL, kama vile hatukuifanyia nchi yetu lolote la maana, hatujapandishiwa hiyo Sh 50,000 mpaka leo. Baba mimi siwezi kukuchukia kwa hili hata kama ninaona jinsi fedha zinavyomwagwa katika barabara tunazopita. Najua wewe ni mtu mwema.

Lakini watumishi walioko chini yako wamefaulu kukutengenezea chuki kubwa dhidi ya vikongwe hawa ambao wote au ni baba au mama au ni babu na bibi zetu. Wanajua wakati wa kampeni vikongwe ambao watakuwa bado na nguvu za kusimama, watakuja kwenye mikutano yako kuwaonyesha wananchi wapiga kura na dunia kwa ujumla jinsi ambavyo baadhi ya viongozi wao walivyo na roho ngumu! Hakika watahurumiwa kwa gharama ya kuwanyima kura wote walioshiriki katika ukatili huu.

Bashiru Ally mkumbushe baba kuwa hawa wazee kwa uadilifu wao waliitumikia nchi hii kwa makumi ya miaka na kuifanya nchi ya kuvutia hata tulipoingia juzi tu sasa tunajitanua. Kuwatunza wazee ni wajibu wa viongozi wote waliopata uongozi kihalali. Matarajio ya wengi yalikuwa kwa Phillip Mangula, ambaye sasa wanaona si ridhiki. Hatujui Komredi Abdulrahman Kinana yuko wapi na anafanya nini huko, lakini alijiuzulu kwa heshima zote. Mungu ampe wepesi wa kutambua kuwa wote tunapita.

Huyu anapodhani anayaanika madudu ya Lugola anasahau kuwa Lugola aliletwa na Baba. Kila alilolifaya Lugola ilifanya serikali. Waliosema samaki huanzia kuoza kichwani hawajakosolewa popote!