Ndugu Rais waasisi wa nchi zetu hizi tatu, Tanganyika, Kenya na Uganda
waliwajengea fikra ya umoja wananchi wake. Tuliopata nafasi
ya kufanyakazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ile iliyovunjika
tunaweza kuthibitisha kuwa wananchi sisi na hasa tuliokuwa kwenye
mashirika yake tulikuwa wana ndugu pasipo shaka.
Watanzania wanaofanyakazi leo katika Jumuiya Afrika Mashariki wana Utanzania
zaidi kuliko Uafrika Mashariki. Na Wakenya na Waganda ni hivyo hivyo.
Hao wengine walioingia sasa wapowapo tu.
Tulifanya mengi kwa kufanana. Ubora wa elimu katika nchi zote tatu
ulikuwa ni ule ule. Hata mitihani tulifanya ile ile. Leo kielimu ni aibu
kujilinganisha na Kenya na Uganda. Ni nini kilitusibu? Awamu ya pili
ilipoanzisha mpango wa kuchangia katika elimu ndiyo ulikuwa mwanzo wa
kifo cha elimu. Upuuzi wakupanua milingoti ya magoli ili tupate
matokeo makubwa sasa ndiyo ulikuja kuiua elimu. Awamu ya Tano kwa
lugha ya kwetu wangeiita ‘mkoma chifwile’ yaani inaua elimu ambayo
tayari ilikwisha kufa!
La mgambo limelia kuwa ukifuja au kufisadi fedha za Serikali ya Awamu
ya Tano, umekunywa sumu. Tena sumu yenyewe ni ile kali sana! Katika
hali ya kawaida, ukinywa sumu na hasa ile kali sana, hakuna njia
nyingine lazima ufe. Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi wamekunywa sumu ya Awamu ya Tano, lakini hadi sasa hata homa tu hawaisikii! Kwa
kauli hii tulikuwa tunamdanganya nani? Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi ikitumia mabilioni ya fedha, kupitia Taasisi yake ya Elimu (TIE) ilichapisha vitabu vingi kutosha nchi nzima, vitabu ambavyo
Serikali kupitia Waziri wa Elimu ilikiri bungeni kuwa vitabu vile
vilikuwa havifai hata kidogo! Matarajio ya wananchi ni kwamba vitabu
vile ambavyo sasa ni vitabu-sumu vingeharibiwa na Serikali na
ingewaambia wananchi hatua ilizochukua dhidi ya waliofanya ufisadi
huo. Hiyo haijawa mpaka leo. Ni sumu gani hii waliokunywa hawa jamaa
ambayo mpaka sasa hajafa mtu?
Ndugu Rais, Waziri anasema bungeni kuwa vitabu-sumu vile vimesahihishwa!
Vilipotazamwa vitabu vipya baadhi vina makosa zaidi ya vitabu-sumu!
Huyu kasema uongo bungeni. Haelewi kitabu kikishachapishwa hakiwezi
kusahihishwa kikiwa hapa duniani! Ilichokokifanya Wizara ya Elimu ni
kuchota mabilioni mengine ya fedha na kuchapisha vitabu vipya. Mungu
alivyowapiga kofi, baadhi ya vitabu vipya vikawa na makosa zaidi ya
vile vitabu-sumu. Makosa mengine mengi wakayarudia yale yale. Baba, bado
huku siyo kunywa sumu? Hii ni sumu gani baba uliyonayo mpaka sasa
hajafa mtu? Watu kunywa wanakunywa, lakini mbona hawaonyeshi hata
dalili za homa tu! Au sumu inachagua? Sumu inayochagua wa kuua haiwezi
kuwa sumu ya kujivunia hadharani.
Ndugu Rais, kwa elimu ileile tulioianza pamoja na Wakenya, wakati sisi
tunashindwa hata kutengeneza vitabu bora wenzetu Kenya, Ijumaa
iliyopita waliweka historia kwa kuwa na setelaiti ya kwanza kuwahi
kutengenezwa nchini humo iliyotumwa katika sayari. Chombo hicho cha
kuzunguka sayari kilitengenezwa na wanafunzi na watafiti wa Chuo Kikuu
cha Nairobi kwa ushirikiano na shirika la teknolojia za sayari la
Japan Space Agency (JAXA).
Naibu Makamu wa chuo hicho, Profesa Peter Mbithi amesema mafanikio hayo ni dhihirisho la hatua zilizopigwa nchini kuhusu utafiti wa kiteknolojia ambao unaweza kuchangia katika maendeleo yatakayokuza uchumi wa kitaifa. Wakati wanafunzi wa Kenya wanatengeneza setelaiti wanafunzi zaidi ya 900 wa shule yetu iliyoko
Geita wanatumia matundu mawili ya vyoo na darasa moja wanasomea zaidi
ya wanafunzi 240. Jirani unajengwa uwanja mkubwa wa ndege! Lini hawa watawaza
kutengeneza setelaiti?
Tuna nchi kubwa kuliko Kenya. Tuna watu wengi kuliko Kenya. Tuna
vivutio na raslimali nyingi kuliko Kenya. Wanachotushinda Wakenya ni
nini? Baba wa Taifa angesema, ujinga! Pamoja na ujinga baadhi ya
viongozi wetu wamekosa aibu. Mtu anasimama hadharani
na kusema Tanzania ya Awamu ya Tano itakuwa ni ya viwanda na baada ya
miaka miwili tu anasema wamejenga viwanda zaidi ya 3,000. ‘Twende basi
ukatuonyeshe viwanda vyenyewe vilipo, anakupeleka chini ya mwembe kwa
mbangaizaji wa vyerehani nne! Kwa wale vimbelembele hapa simchochei
yeyote. Nasema kama wanadhani wananchi watadumu katika ujinga milele,
wakayarudie maneno hayo katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Watakapopopolewa kwa mawe kutoka kwa wananchi wenye hasira, ndipo
wataelewa kuwa wananchi sasa ni waelewa!
Hapa anadanganywa nani? Anadanganywa baba, Rais wetu mpendwa? Kwa hili
hata mwananchi mjinga kabisa kabisa hadanganyiki. Atakuona wewe ni
mpuuzi mmojawapo kati ya wapuuzi wengi waliopo katika nchi hii. Rais
Julius Kambarage Nyerere katika urais wake wa miaka 24 alijitahidi
sana kujenga viwanda vingi, lakini mia nne havikufika. Iweje katika
miaka miwili tu tuwaambie wananchi kuwa tumejenga viwanda zaidi ya 3,000? Yawezekana wanawaona wananchi wetu kuwa ni wajinga, na
inawezekana baadhi ya wananchi kweli ni wajinga, lakini siyo kwa
kiwango wanachowadhania! Kama wananchi hao hao leo wanawaita waliopanua
milingoti ya magoli ili wafunge magoli mengi kuwa ni wajinga kwa
matokeo makubwa sasa, watashindwa nini kwa hawa wa vyerehani vinne
vinavyohamishika? Wanawadhalilisha wanaowafuga na wanaowafuga
wasipowatupa sasa wananchi watawaingiza katika kundi moja la wapuuzi.
Mwanamwema Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amesema pamoja na
kuhimiza ujenzi wa viwanda, lakini ‘ujanja’ wa vyerehani vinne chini ya
mwembe hautaitwa kiwanda katika mkoa wake. Kauli hii inaonyesha kuwa
hata katika Serikali ya Awamu ya Tano, viongozi timamu wamo. Bila
tahadhali baadhi ya viongozi wenye dhamana ya viwanda watawasukuma
wananchi waione dhama nzima ya Tanzania ya viwanda ifanane na yale
mambo ambayo Baba wa Taifa alikuwa akiyaita ya kijingajinga! Wananchi
hawamdharau kiongozi wao, lakini kauli ya vyerehani vinne au koroboi
tano upenuni mwa nyumba ya mtu kuita kiwanda kiongozi amejitoa fahamu
mwenyewe! 2020 watawazomea na kuwapopoa mawe kama waliovaa nusu
uchi! Waliokunywa sumu ya Serikali ya Awamu ya Tano, lakini
hawakudhurika watanyweshwa sumu ya wananchi inayoitwa, ‘kill me
quick!’ (Niue mara moja).