Ndugu Rais, tunasoma kuwa wanafunzi wa Bwana Yesu walimwomba Yesu, awafundishe kusali kama Yohana Mbatizaji alivyowafundisha wafuasi wake. Yesu akawajibu akisema, mnaposali semeni hivi, “Baba yetu uliye Mbinguni jina lako litukuzwe; ufalme wako uje, utakalolifanyike duniani kama mbinguni, utupatie leo chakula chetu cha kila siku, utusamehe makosa yetu kama vile sisi tunavyowasamehe wale waliotukosea!’

Ndugu Rais, watu wako nao wanakuomba uwafundishe kusali. Waambie wanaposali waseme hivi, “Tumetishwa kiasi cha kutosha; tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndiyo unaotufanya tutishwe, tunyonywe, tunyanyaswe na tupuuzwe! Sasa tunataka mabadiliko. Mabadiliko ya kuuondoa unyonge wetu ili tusitishwe tena, tusinyonywe tena, tusinyanyaswe tena na tusipuuzwe tena!”

Ndugu Rais, wako wananchi wengi hivi sasa ambao wakiukumbuka uongozi wa Awamu ya Kwanza machozi huwalengalenga wasijue lakufanya! Awamu ile iliwajaza matumaini ya amani na ustawi yaliyoifanya mioyo yao ifurike kwa furaha! Nao wakaishi katika upendo, umoja na mshikamano bila kugundua kuwa walikuwa na tofauti zao!

Awamu ya Pili ilipoingia, ilitenda dhambi moja kubwa! Kuyazima matumaini hayo, kwa kulifuta Azimio takatifu; Azimio la Arusha! Labda ni kwa sababu ya uwepo wa Baba wa Taifa wakati ule wananchi hawakugundua mara moja ukubwa wa dhambi iliyotendwa! Lakini dhambi hii ilimtoa machozi Baba wa Taifa! Machozi yale ya Baba wa Taifa kwa hakika hayatakauka mpaka wote waliohusika watakapokuwa wamekwisha hukumiwa! Wamekwenda wengi na wengi wamepanga mstari wanafuata!

Ndugu Rais, Azimio la Arusha lilikuwa ni Azimio takatifu kwa sababu lilikuwa na miiko na maadili ya uongozi! Haya mawili ndiyo vitendeakazi yaani rula, pimamaji na pasi vilivyotumika kuinyosha nchi. Nchi ilikuwa imenyooka! Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwaongoza viongozi wenzake katika kikao kilichofanyika katika mji (sasa jiji) wa Arusha kuanzia tarehe 26 hadi 29 Januari, 1967. Kikao hicho ndicho kilichotoka na uamuzi wa kuasisiwa kwa Azimio la Arusha. Uamuzi ambao ulikuja kutangazwa rasmi na Baba wa Taifa, tarehe 5 Februari, 1967 jijini Dar es Salaam. Jumapili ya tarehe 5, Februari mwaka huu tamko la Azimio la Arusha litakuwa linatimiza miaka 50.

Akitangaza Azimio, la Azimio la Arusha, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “Tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha.

Unyonge wetu ndiyo uliotufanya tunyonywe, tunyanyaswe na kupuuzwa!

Sasa tunataka mapinduzi. Mapinduzi ya kuuondoa unyonge wetu ili tusinyonywe tena, tusinyanyaswe tena na tusipuuzwe tena!”

Ujamaa ni imani. Azimio la Arusha linamtaka kiongozi asiwanyonye wale anaowaongoza na wala asitake kuabudiwa! Kiongozi wa nchi zetu hizi za Kiafrika ambaye bado anadhani ni mtawala au anadhani ana utawala wake, hasomi alama za nyakati! Yuko nyuma kwa zaidi ya miaka 50.

Awamu ya Tatu ndiyo iliyokuja kuonesha madhara ya kifo cha Azimio la Arusha baada ya uamuzi wake wa kuuza kila mali ya umma vikiwamo viwanda, mashirika ya umma na wenyewe ukajiuzia nyumba za wananchi (Serikali) kwa bei ya kutupa! Kabla hajaitwa mbele ya haki Baba wa Taifa alilaani uamuzi huo, lakini alipuuzwa na uuzaji uliendelea!

Tunaoamini katika kitubio, tunaamini hakuna atakayesamehewa bila kufanya kitubio!

Awamu ya Nne wanaosema waliiacha nchi ikiwa majipu matupu, wanawaoneaaibu! Wangesema ukweli tu kwamba kilichofanyika kwa wakati wao wote ulikuwa ni wizi mtupu! Akina baba waliiba wao na wake zao na watoto wao hata na nyumba zao zilizokuwa ndogo mwanzoni nazo ziliiba mpaka zikawa kubwa! Wananchi wakaachwa kama manyani jangwani! Hapa jangwani Baba, ndipo ulipowakuta watu wako! Mioyo yao imepondekapondeka sasa na wewe usiwajaze vitisho watu wako kwa kuwa wamekata tamaa! Isome tena sala yao huruma juu yao, ikurudie!

Baba, warudishie watu wa Mungu Azimio lao la Arusha na nchi itanyooka yenyewe! Tukidhani kuwa tunaweza kuinyoosha nchi tukiwa na viongozi waliokwisha tupa miiko na maadili ni sawa na kuinyoosha nchi bila kuwa na chakunyoshea, iwe rula, pimamaji au pasi. Huku ni kujilisha upepo.

Tusiwape nafasi wasiotutakia mema ya kutuona tunapuyanga!

Ndugu Rais, walichoonesha wananchi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 ni kiu yao ya mabadiliko bila kujali nani angewaletea! Wanayaona mabadiliko wayatakayo? Kama hawayaoni kiu yao ya kutaka mabadiliko itaendea kusumbua. Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu imeandikwa, “Mabadiliko yakiamua kuja huja. Hayana mjadala wa mbadala. Ni kiongozi mwenye busara tu ndiye huyakubali mabadiliko kwa amani!” Imeandikwa nguvu ya wananchi waliokata tamaa na kuamua liwalo na liwe, hushinda nguvu za majeshi yote! Kuibuka viongozi kama Yahya Jameeh wa Gambia ni ushahidi kuonesha jinsi mamlaka makubwa yanavyowalevya baadhi ya viongozi wa Afrika waliokosa busara.

Ndugu Rais, mwanadamu timamu anamtaka mtu wa kumwongoza, na si mtu wa kumtawala. Kiongozi huwaongoza watu wa Mungu kuelekea kule anakokuona kuna malisho mema kwa ajili ya ustawi wao na wa nchi yao.

Silaha yake kubwa ni kufundisha, kushauri na kushawishi. Wakati wa Azimio la Arusha kiongozi kujiita mtawala au mheshimiwa ilikuwa ni kukufuru.

Mtawala ni mheshimiwa kama walivyokuwa wakoloni. Ni mnyampala ambaye silaha yake kubwa ni makali ya upanga. Atatumia makali ya upanga kuwanyamazisha wale anaowatawala wasifurukute. Katika baadhi ya nchi za Kiafrika wakoloni wanarudi kupitia madirishani.

Baba, Iweje hadi leo magari ya nchi hii bado yanatumia mafuta yanayoagizwa kwa fedha nyingi za kigeni wakati gesi ipo mpaka Dar es Salaam? Fedha ambazo zingeokolewa si ndiyo zingetumika kuboresha miundombinu hata kununua meli na ndege bila ya kuwafanya wananchi watuchukie kwa kuyafanya maisha yao kuwa magumu? Badala yake nchi imejaa mikataba ya siri. Wanaosema gesi yenyewe imeuzwa yote wajibiwe vipi? Baba siku zinakuja zitakazoyafanya yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu yaonekane ni utabiri! Imeandikwa, “Kila kaya ikiache kibatari chake kikiwaka kwa maana tumelishauri jua lisitokee mpaka nchi itakaporejeshwa kwa wananchi! Nenda katangaze neno hili!

Usinitaje, kwaheri!”