Ndugu Rais ulipoongea na wahariri wa vyombo vya habari ulisema mengi na mengi mengine uliyafafanua vizuri. Nia yako njema kwa nchi hii ilionekana dhahiri. Ukasema tukuamini! Tumekusikia, tumekuamini!
Umefanya vema kuwajibu watu wako wema wanaouliza kila siku kutaka kujua kama Rais wao anasoma haya tunayoandika. Umesema unasoma nao wamekusikia! Sasa wanawema msiniulize je, akishayasoma anayafanyia kazi? Kumbukeni huyu ni Rais wa nchi.
Baba, ulijibu maswali mengi sana na mengine kwa ufasaha sana, lakini swali moja lililoulizwa na watu wawili tofauti hukulitendea haki.
Maswali mengine ulisema ni magumu, lakini uliyajibu. Iweje hili lisipate jibu mpaka leo? Wa pili aliuliza kwa ufasaha zaidi akasema, “Uliapa kuilinda Katiba ya nchi hii. Katiba ya nchi hii inatambua haki za raia ikiwa ni pamoja na haki yao ya kufanya mikutano yao ya kisiasa na maandamano ya amani. Ulipoamua kuzuia haki hiyo inayotambuliwa na Katiba uliyoapa kuilinda, hayo mamlaka uliyapata wapi?” Baba hukuwajibu wale wanawema wawili!
Sitaki kuwa mnafiki kwako. Tuliandika tangu zamani kuwa Chama Cha Mapinduzi kilikuwa na wagombea wawili waliokuwa na nguvu kuliko wengine. Edward Lowassa aliondoka akajiunga Chadema. Chama kilipolazimika kumtema chaguo lake kilikuwa tayari kimetumia nguvu nyingi na fedha nyingi kwa mtu wao. Ulisema uli-beep, lakini hakukuwa na jinsi wakalazimika uwe wewe. Ndiyo maana tulisema katika hili wewe unakidai chama, chama hakikudai kitu! Kosa kubwa tunalolifanya ni kuwaona wapinzani wa nje ya chama chako kuwa maadui wakubwa katika urais wetu. Tumesahau maneno ya wahenga, “Kikulacho ki nguoni mwako!” Hatua ya kuzima televisheni bungeni, kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na maandamano ya amani ya vyama vya upinzani tunaonesha udhaifu wetu kwa kuogopa nyoka wa plastiki. Nyoka wa kweli au hatumwoni, au hatumjui!
Hukueleza ni kwanini hutaki kuyafukua makaburi uliyoyakuta Ikulu, lakini elewa kuwa katika imani za makabila karibu yote, mtu hajengi nyumba juu ya makaburi! Tuna uhakika gani kama wenye makaburi yao hawajakuingizia watu unaofanya nao kazi ili wawalindie makaburi yao?
Umekuwa kila mara ukiomba tukuombee, lakini kuna baadhi ya mawaziri wako hata siku moja hawajawahi kusikika wakiwataka wananchi wakuombee!
Wanangoja nini kama siyo kungoja umalize hii ngwe, uende? Makaburi kama ESCROW, EPA, LUGUMI na hayo mamilioni ya dola uliyosema yalikuwa yakajenge kiwanda Lindi, lakini hayakujenga, usipoyafukua yatakufufukia! Sasa wanakwambia unabomoa mema uliyoyakuta.
Ulisema vema kuwa Ikulu siyo pako, Ikulu ni mahali pa Watanzania.
Viongozi watakuja, watakwenda nao watafanya mengi na kuhangaika sana nao watapita, lakini Ikulu na nchi vitabaki. Ili kuilinda nia njema uliyoionesha na kuyafanya unayotaka kufanya yawe na maana zaidi lazima utambue kuwa bila kuirejesha miiko na maadili vilivyomo ndani ya Azimio la Arusha, itakuwa sawa sawa na kusaga unga katika upepo mkali! Ukipita kama wengine walivyopita hakitabaki kitu cha kukumbuka!
Baba ungependa uje ukumbukwe kwa lipi?
Wako viongozi wamepita, wengine utadhani hakuwako, lakini heshima ya mwasisi wa Azimio la Arusha, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, haitapita! Kukumbukwa ni kukumbukwa hata kwa mabaya ayatendayo mwanadamu, lakini baba ungependa uje ukumbukwe kwa jema lipi? Unafanya mema yanaonekana, lakini kwa hili fanya kama ulivyofanya la kuhamia Dodoma. Lirejeshe Azimio la Arusha nawe utabarikiwa kwa kuwa utakuwa umewang’atua waja wa Mwenyezi Mungu kutoka katika makucha ya manyanga’au wachache ambao leo ukilitaja Azimio la Arusha nguo zao za ndani zinawabana!
Baba, Taifa limegawanyika na sasa linatawanyika. Katiba mpya ingekuwa ndio suluhu iliyo njema kama wenye roho mbaya wasingeshika kwenye mpini! Ulipoulizwa kuhusu mchakato wa Katiba mpya jibu lako lilikuwa kama mfano wa swali. Ukasema katika siku zako zote ulizofanya kampeni hakuna popote ulipotamka, ‘Katiba mpya’. Kwa hakika ulikuwa na maana yako, lakini wenye kuelewa wakawa wameelewa. Ingawa mwishoni ulisema mchakato ulikuwa katika hatua nzuri, lakini sentensi ya kwanza ilikuwa imejibu yote kuwa kuendelea na Katiba mpya kutalipasua zaidi Taifa letu. Lakini kwa kuwa Katiba mpya ni muhimu na ni lazima basi busara ya kutambua kuwa bila Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi kupatikana amani ya kweli haiwezi kupatikana katika nchi.
Waliozihujumu jitihada za kupatikana Katiba mpya, ile yenye matakwa ya watu wa Mungu, Mungu wa Yakobo, Mungu wa Eliya ameanza kuwaadhibu wakiwa bado wako hai, hapa hapa duniani. Kwa unyang’au wao waliyavuruga mawazo mema ya wananchi na kuyaingiza ya kwao ya kinyang’au! Mwisho wao sasa ni mchungu kama shubiri!
Ndugu Rais, ilikuwa ni faraja kubwa kukusikia ukisema mwenyewe kuwa unayasoma haya tunayoyaandika. Kama watu wako wema wanayasoma na kuyakubali halafu wewe huyasomi, hiyo ingekuwa ni hasara yako mwenyewe. Na kwa sababu hiyo baba nataka ujue kuwa, kama kuna jambo nitalililia mpaka pumzi yangu ya mwisho, basi ni Azimio la Arusha!
Laiti Azimio la Arusha lingalikuwako hadi leo, nina hakika hayo makaburi uliyoyakuta Ikulu ambayo umesema hutaki kuyafukua, usingeyakuta!
Ndugu Rais, nitaendelea kuililia nchi yangu, na kuwalilia masikini na wanyonge wa nchi hii tajiri, huku nikijililia na mimi mwenyewe!
Namshukuru Muumba wangu kwa sababu kadri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo idadi ya wanaoungana nami katika kilio hiki inavyozidi kuongezeka.
Hii ni sauti ya kilio cha mtu aliaye jangwani, iko siku Mwenyezi atakisikia! Najua ugumu uliopo, lakini imani yangu iko kwa maneno ya wahenga, waliosema, “Papo kwa papo, kamba hukata jiwe!”.