Ndugu Rais, kwa unyenyekevu mkubwa nakusihi ulitegee sikio lako huku kunena kwangu mimi mtumishi wako nisiyestahili. Kusema polisi wanatumika vibaya umegusa, ‘penyewe’! Taifa limekusikia na wananchi wamekusikia pia!

Ubarikiwe sana kwa kuwarudisha masikini wa Nyalingoko katika mashimo yao wanakohangaika kutafuta utajiri wao wa dhahabu ambao waliwekewa ardhini na Muumba wao!

Ndugu Rais, ni kilio cha nchi nzima tena cha muda mrefu kuwa wananchi katika kuhangaika kwao wamekuwa wakichimba kule, huku, hapa au pale kwa jasho jingi, lakini kila wagunduapo madini hasa dhahabu, basi serikali kwa maana ya mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa wakitumia polisi hujisokomeza katika eneo hilo wakidai kuwa ardhi ni mali ya serikali.

Baba, sawa ardhi ni mali ya serikali, lakini na huu ugunduzi uliofanywa na hawa wananchi masikini nao ni mali ya serikali?  Nguvu zao, muda wao na kuhangaika kwao ni mali ya serikali kweli? Hawa vijana wako wanawatumia polisi vibaya. Na kwa matumizi hayo mabaya wamewafanya wanyonge wa nchi hii wasiipende serikali yao. Serikali ni Rais! Baba ni kipi utakifanya masikini wako wakufurahie kwa matumizi haya mabaya ya polisi?

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita amewataka wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Mwasabuka uliopo katika Kata ya Mwigiro warudi kuendelea na shughuli zao za uchimbaji dhahabu. Awali, Mkuu wa Wilaya alikuwa amewaondoa na kufukia mashimo yao. Cha ajabu ni kwamba hata baada ya agizo la Rais, polisi 50 wa mkuu huyo wa wilaya waliendelea kuilinda sehemu hiyo huku wakiwa na silaha za moto walizokuwa wanazitumia kuwafukuzia wananchi ambao wewe baba uliagiza wasibugudhiwe! Fahamu hawa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa hawana cha kupoteza pale mtakapowarudia masikini hawa kuomba kura!

Tena uliagiza vema sana kuwa haiwezekani wahamishwe wananchi zaidi ya elfu saba kumpisha mwekezaji ambaye ni mtu mmoja. Ukauliza kwanini mtu huyo asitafutiwe sehemu nyingine? Lakini hawa wawekezaji katika madini na hasa dhahabu, kwanini wawekezaji wengi kila mwaka wanapata hasara, lakini wanaendelea na biashara? Kulikoni? Hasara ya kila mwaka mbona hawafilisiki? 

Kama Mungu amekuongoza kuliona hili, basi kwa agizo lako watu wa Mungu wanaweza kutoka katika dimbwi la umasikini juu ya ardhi yao tajiri. Kwa kuwapenda watu wake Mungu aliwawekea Watanzania rasilimali lukuki na za kila aina, lakini kila wanapovigusa vile vilivyowekwa kwa ajili yao wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa wanawatimua kwa madai kuwa wamepata mwekezaji. Kwanini wawekezaji hawa wanapenda kuwekeza pale wananchi walipopatafuta kwa jasho lao? 

Je, hawa wananchi hapo hawajawekeza nguvu zao na jasho lao? Wawekezaji wa nchi hii ni tofauti kabisa na wawekezaji halisi kwa maana ya mtu mwenye mali sasa anataka kuwekeza. Wawekezaji wetu wengi wamekuja nchini wakiwa hawana fedha wala chochote! Akisha pata hiyo ardhi ya wananchi ndiyo anaenda kukopea benki. Natamani iwe kweli kuwa kwa kuwa umeliona hili, basi unapoinyosha nchi utalinyosha na hili.

Ndugu Rais, haya yote yaliandikwa tangu zamani katika kitabu cha

Mwalimu Mkuu wa Watu. Ukurasa wa 90 tunasoma; “Msauzi alipoambiwa aseme, alihekemua kidogo kisha akasema, kwanza hawakuwa wanaijua nchi hii, bali walifuatwa na ndugu zao waliokuwa wanafanyakazi katika mashirika ya fedha ya dunia kuwa wanaweza kutajirika kwa raslimali nyingi za nchi hii mradi tu wajiite wawekezaji…walijipanga katika vikosi mbalimbali. Wengine walikwenda katika machimbo ya dhahabu na madini mengine. Wengine katika hifadhi na mbuga za wanyama na wengine katika uvuvi na sehemu zote zilizoonekana kuwa na mali nyingi.  Wengine walichukua viwanda na mashirika ya umma huku wakiwa hawana fedha.

Mashirika hayo yalijinunua kwa fedha zake yenyewe. walichofanya wawekezezaji ni kuja na hongo kidogo ambayo viongozi wetu waliita takrima!”

Ndugu Rais, kilio kikubwa cha watu wako tunasoma katika ukurasa wa 103,

Imeandikwa; “Tunataka Rais atambue kuwa utajiri mkubwa wa nchi hii, dhahabu na madini mengine walimilikishwa wageni! Wameachiwa wachimbe, wapeleke kwao kiasi chochote watakacho, sisi watupatie mrabaha wa asilimia duni tu wa kile wanachotaka kutuambia wamechukua, kisha wakimaliza watuachie mashimo na mapango ya kutisha pamoja na milima ya michanga (mawe) iliyotoka ardhini. Huo ndiyo uwe urithi kwa vizazi vyetu!” 

Baba, wananchi wa kawaida wanapoiona hali hii na viongozi wao wapo na wanaiona, lakini si tu hawafanyi chochote kuizuia, bali wameridhia, unadhani wanasemaje? Lazima wanasema viongozi wetu ni sehemu ya uporaji huo. Ndiyo kumbe wasemeje? Siku ya kucharuka watacharukiwa wote!”

Wakuu wa mikoa kama walivyo wakuu wa wilaya ni watu wakuja katika sehemu zao za kazi! Walikotokea wananchi hawakujui. Na wao hawawajui wananchi wanaowakuta. Wametumwa kwenda kuwatawala wananchi bila ridhaa yao! Hawa ni wanyampara tu! Wakati wa Yesu hawa waliitwa Liwali.

Hawakuchaguliwa na mwananchi yeyote. Uchungu wao kwa wananchi utatoka wapi kama si unafiki wa kuiga? Hawa ni watu wa mshahara tu! Ndiyo maana hata baada ya agizo la Rais la kutowabugudhi wachimbaji wadogo wadogo bado polisi wa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita waliendelea kuwatimua wachimbaji wadogo wadogo huku wakiwa na silaha za moto.

Ndugu Rais, gharama ya matumizi haya mabaya ya polisi yatakuja kuonekana katika uchaguzi unaokuja. Umejengwa uhasama mkubwa kati ya wananchi na polisi kiasi cha wananchi kushangilia wanaposikia raia kaua polisi! Baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kwa kuwatumia polisi vibaya wamewatengenezea wapinzani mtaji mkubwa! Kumbuka hawa hawaendi kwa wananchi kuomba kura. Wala hawa hawakula yamini kuwa watakutumikia wewe binafsi. Wanamtumikia rais. Hivyo yoyote atakayetokea kwao ni poa tu! Hapa hapendwi mtu!

Baba, watu wako wanangoja kuona hatua utakazochukua. Ukiishia hapo, watasema; “Ah! Hata rais wetu anaishia kulalamika! Twafwa!”