Ndugu Rais, siku ya kuoneshana shari imepita! Busara kubwa imetumika kuipisha siku ya kihoro! Lakini tukiendeleza hali hii, siku za aina hiyo zitakuwa nyingi huko tuendako! Hatujui wana busara kubwa kiasi gani, lakini kwa hili walioitikia ushauri wa viongozi wengine wameonesha busara kubwa!

Dunia ina utamaduni wake ambao mmoja kati ya washindani akionesha wingi wa busara na hekima kwa jambo lile lile, sifa mbaya hupewa mshindani wake.

Heri waliozaliwa na busara kwa maana wanatambua kuwa hapa hakuna mshindi wala mshindwa! Hivyo ukimsikia mtu anadai kuwa tumeshinda jua huyo ni mjinga. Atakayesema wameufyata au wameniogopa huyo usigombane naye kwa sababu anatakiwa apimwe akili kwanza.

Ndugu Rais, kipindi kilichopita kilikuwa kigumu sana kwa wananchi!

Mazumbukuku waliwajaza hofu wananchi kiasi cha kuwafanya wapoteze kabisa imani kubwa waliyokuwanayo kwa baadhi ya viongozi wao waliowachagua. Mwanamwema mmoja akaniambia, “Mwalimu Mkuu uchaguzi umepita. Kama ni kweli wanaotufanyia hivi tuliwachagua kwa ridhaa yetu wenyewe, basi Mwenyezi Mungu atusamehe. Hatuna pa kutokea, bali kurejelea yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu ukurasa wa 78 kuwa, “Ama kweli, kilicho sawa sawa (tulichokiona) katika mwanga wa taa si lazima kiwe sawa sawa katika mwanga wa jua. Nimejifunza leo kuwa si busara kumhukumu mtu au kitu kutokana na kinavyoonekana”.

Wagombea wote wote walioshinda waliapa kuilinda Katiba ya nchi. Anayekiuka kiapo chake mwenyewe hastahili kuwa kiongozi wa wengine!

Ndugu Rais, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere siku moja alisema, “Katika kitu nilichokiogopa sana katika uongozi wangu ni kujikuta katika hali itakayonilazimisha kuwageuzia watu wangu mitutu ya bunduki walizonunua kwa kodi zao!”

Mwalimu Nyerere anaona uchungu kuwaelekezea watu wake bunduki inayoua mtu mmoja mmoja. Leo wananchi wasio na hatia yoyote wala silaha yoyote kwa nini waelekezewa mazingira ya kuwatisha na kuwatia hofu.

Kabla ya Septemba mosi yalikuwapo maandalizi kwa vikosi vyote vya ulinzi na usalama. Walijinoa vilivyo kukabiliana na ambao wangeamua kuandamana. Hii ni bahati mbaya sana! Ni bahati mbaya kwa sababu walengwa walikuwa ni waandamanaji! Waliishapita marais wanne na mpaka sasa ni nusu karne tangu nchi yetu ipate Uhuru kutoka kwa wakoloni, wananchi hawajawahi kuoneshwa sheria hata moja inayozuia maandamano kama maandamano. Lakini hata Katiba (msahafu) ya nchi hii inatoa haki ya kuandamana. Kwa yeyote yule, kuzuia raia wasitumie haki yao wanayopewa na Katiba ni kuikanyaga Katiba ya nchi. Hili linaweza kuwa kosa kubwa kuliko makosa yote katika nchi yoyote duniani ambayo viongozi wake wana utu na ustaarabu wa kidemokrasia.

Ndugu Rais, sheria za nchi hazitoki kwenye mdomo wa mtu. Baba wa Taifa alionya akasema hatutaki kiongozi ambaye akishamsikiliza mkewe tu kesho anatuletea sheria mpya. Uvunjifu wa amani unaweza kutokea popote hata katika kituo cha polisi. Maandamano ni mkusanyiko wa watu sawa sawa na mikusanyiko mingine ya watu kama misikitini, makanisani, viwanja vya mpira, kumbi za starehe, harusi na penginepo! Kote huko vurugu huweza kutokea. Lakini busara ni kuwadhibiti wanaofanya vurugu.

Haiwezi kuwa busara hata kidogo kusema ligi kuu mwaka mzima huu hamna eti kuna viashiria vya kuvunjika amani. TFF wakitoa amri kama hiyo halafu wakaitwa ni madikteta ni saizi yao kabisa. Sheria za kiimla haziheshimiwi katika nchi yoyote na hasa katika nyakati hizi tulizonazo! Kiongozi bora ni yule anayeweza kusoma alama za nyakati!

Ndugu Rais, kinachokosekana katika nchi hii ni elimu ya uraia. Wananchi waelimishwe kuwa ni, ‘nchi yangu kwanza’ vyama baadaye! Wajue kuwa hakuna chama cha siasa ambacho kipaumbele chake ni maslahi au ustawi wa wananchi! Lengo kuu la chama cha siasa chochote ni kuongoza wananchi. Hivyo, hakuna Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa au Diwani au

Mbunge au Rais aliyegombea nafasi aliyonayo kwa lengo la kuwasaidia wananchi. Wote waliangalia kwanza nafsi zao, familia zao na wanaowazunguka. Kumshabikia mwanasiasa ni ujinga uleule wa kukishabikia chama cha siasa.

Wananchi lazima waelimishwe kuwa wao katika ujumla wao ndio wenye hakimiliki ya nchi hii. Waliowaomba ridhaa ya kuwatumikia katika nafasi yoyote iwe udiwani, ubunge, urais na sehemu nyingine ni watumishi wao.

Wananchi wanaowaita watumishi wao, ‘waheshimiwa’ wanapaswa kupimwa akili. Na watumishi wa wananchi wanaokubali uheshimiwa kutoka kwa waajiri wao nao wapimwe akili!

Wanapoitwa waheshimiwa wanadhani wana mamlaka ya kufanya chochote katika nchi na juu ya wananchi. Ni busara gani iliyotumika kuonesha silaha nzito nzito kukabiliana na watu ambao hata visu tu vya mfukoni walikuwa hawana?

Ndugu Rais, jamaa wametishia tu kuwa sasa ni Desemba mosi. Bila kujipa muda wa kutafakari wamekurupuka wakukurupuka na kusema watapanda miti!

Hawakuishia hapo. Eti Jeshi la Wananchi litashirikishwa! Anatishia nyau! Utoto maji ya moto! Wasipoachana na utoto huu wajue wenzao ni vichwa na wananchi wameishagundua hilo. Watawaburuza hadi kufikia 2020 watajikuta hawajatimiza lolote! Si kazi yao kujibu tu!

Baba unapofanya vema lazima tukupongeze. Kukataa kuzungumza na wanaojiita viongozi wa dini ubarikiwe sana. Hawa siyo moto siyo baridi! Wangekuwa wanamtumika Mwenyezi Mungu wangekwambia bila kukuficha kuwa kuna mahali umekosea.

Madhali hawajakwambia hivyo sasa wanataka kuja kukuambia nini? Wakate maini! Waambie, hujaribiwi! Kwani ukiachana nao kuna ubaya gani?