Ndugu Rais, tuutafute kwanza ufalme wa mbingu na haya mengine yote tutayapata kwa ziada! Ufalme wa Mbingu hautafutwi kwa kubadilisha nyumba za ibada au madhehebu, leo kanisa hili na kesho kanisa lile kama majumba ya sinema kuona lipi leo linaonesha mkanda mzuri!
Natena ufalme wa Mbingu haupatikani kanisani wala msikitini. Tuliza imani yako! Kama mtu amekuwa muumini wa kanisa la Mtakatifu Petero na huko hajamwona Kristu, basi atamaliza madhehebu na makanisa, huko nako Yesu Kristu hatamwona!
Zamani tuliambiwa kila mamlaka ilitoka kwa Mungu. Andiko hili linaonekana kutenguliwa na baadhi ya viongozi wa Awamu ya Tano. Huku akitumia televisheni na vyombo vingine vya habari, kiongozi wa Awamu ya Tano amenukuliwa akisema, “Ukiniona mimi nimesimama hapa ujue kuwa ni Mungu mwenyewe amesimama hapa!” Mamlaka imegeuka na kuwa ndiyo Mungu mwenyewe! Kwa kuwa kauli hii haijakemewa, basi watasikilizwa wale wanaosema tangu kuasisiwa kwa Taifa hili hakuna awamu iliyomdhalilisha Mwenyezi Mungu kama awamu hii! Karibu kila kitu kingeitwa uchochezi hata sala!
Ndugu Rais, wanawema hawawezi kumkataa kiongozi kwa sababu ya uzee wake au ujana wake; la hasha! Bali watamkataa kiongozi kwa sababu ya upumbavu wake! Kwa umri wetu Waziri Mkuu wetu Kassim Majaliwa ni kijana. Lakini ni mtu ambaye ameonesha umakini mkubwa katika utendaji kazi wake akitumia zaidi busara badala ya misuli.
Dada zetu na mama zetu kote ulimwenguni hawafurahii kuitwa wazee, lakini Makamu wa Rais mama yetu Samia amekuwa tofauti sana na wanaume waliomtangulia. Ni kiongozi wa juu ambaye amethibitika kuongozwa na ukweli. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni kijana. Sifahamiani naye, lakini tulipomsikia akizungumza na Waziri Mkuu unaweza kuiona hazina kubwa ya busara iliyoko kifuani mwake. Anatia matumaini ya Taifa kuwa na viongozi makini huko tuendako.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye wengi wanaamini kuwa ndiyo nguzo kuu peke yake iliyobaki imekishikilia chama ameonesha uongozi wa busara kubwa. Alipoingia, alikuta manabii 11 wa uongo wakiizunguka nchi huku wakipandikiza chuki katika jamii kila walipopita! Kinana aliwaadabisha!
Baba, kwa mila na utamaduni wetu na wewe ni kijana kwetu, lakini Mwenyezi Mungu amekubariki akakusogezea vichwa vyote hivi ili uchote busara kutoka kwao ili ukichanganya na yako waja wake wastawi kwa nchi kupata mabadiliko ya kweli. Kwa utajiri huu wa busara, kuna sababu gani baba, ya kuendelea kupuyanga?
Ndugu Rais, ndani ya chama chako watu waadilifu wanaomcha Mungu bila unafiki, wapo. Hali ya hewa chafu iliyoifunika Arusha inaashiria uwepo wa nguvu za shetani. Unganisha busara ulizojaliwa ulitafakari hili kwa kuwa hali hii imeinajisi nchi yetu. Nchi alimozaliwa Mwenyeheri, Mtakatifu mtarajiwa Julius Kambarage Nyerere! Kama ilivyo pepo, vivyo hivyo mwanadamu hujitengenezea jahanamu yake kwa mikono yake mwenyewe akingali hapa hapa duniani! Wasiyeona ukali wa ncha ya mkuki wanaojichongea leo, wataiona kesho itakapoelekezwa katika vifua vyao!
Ilikuwa kama kujibu hotuba yako vile; mara baada ya kumaliza kuhutubia kule Shinyanga, kituo kimoja cha televisheni kikaweka hotuba ya ‘wasia wa baba’ ambako Mwalimu Nyerere alisema, kiongozi hata ungefanya nini ni bure; kiongozi makini lazima aelewe kuwa watu wanachotaka kwanza kabisa, ni kuishi kwa furaha katika nchi yao! Baba, Nyerere anasema kama hayawapatii furaha yale tunayoyafanya, basi tujue tunapuyanga!
Kesho yake alfajiri mzee mmoja aliyekuwapo katika mkutano akaniambia, Rais aliposema huu ni wakati wa wakulima kupiga hela, hivyo wauzemahindi kwa bei waitakayo hata kwa ng’ombe watatu kwa debe, hakujua kuwa hakuna mkulima mwenye mahindi kwa sasa. Wafanyabiashara waliyanunua yote kutoka kwa wakulima. Alichofanya Rais ni kuwaruhusu wafanyabiashara kuwalangua wananchi kwa bei waitakayo. Wafugaji watanunua, lakini ni mkulima gani ataiweza bei hiyo?”
Kama wananchi walisombwa kutoka vijijini kuwaleta kwenye ule mkutano, basi neno ndege halikutakiwa kutamkwa pale hata mara moja. Karibu wotewale hawajawahi kuiona ndege ikiwa imesimama karibu yao, juu ya ardhi. Lakini shida ya maji imevivimbisha vifua vyao karibu ya kupasuka.
Ndugu Rais, andiko lililopita niliandika juu ya Mwalimu Forum-(MWAFO).
Mwitikio wake umekuwa na kishindo kikubwa. Baba niliandika hivi; Baada ya kuona vyama vya kisiasa vimeuparaganyisha umoja, upendo na mshikamano katika nchi yetu, wanawema walikaa pamoja wakaunda jukwaa la kitaifa kwa jina la Mwalimu Forum kwa kifupi MWAFO. Lilisajiliwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kama asasi isiyo ya kiserikali kwa namba SA 15891 mnamo Julai 24,.2008.
Madhumuni ya jukwaa hili ni kutoa elimu ya uraia kwa wanachama na jamii yote kwa lengo la kuamsha ari ya UZALENDO na mapenzi ya mtu kwa mtu na mtu kwa nchi yake. MWAFO inalenga kuwapa Watanzania jukwaa la kuzungumza na kujadili mambo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii bila kuingiza itikadi zao za kisiasa, kidini, kikabila au ubaguzi wa aina nyingine yoyote kwa kutumia kaulimbiu ya NCHI YANGU KWANZA! MWAFO inaeneza elimu ya uraia kwa kutumia njia mbalimbali kama;
• Kuandika makala mbalimbali katika magazeti.
•Kuandaa vipindi maalum vya kutoa elimu ya uraia kwa kutumia redio na luninga.
• Kuchapisha vipeperushi vitakayoelezea haki na wajibu wa raia kwa nchi yake.
• Kufundisha elimu ya uraia kwa kutumia sinema na michezo ya kuigiza.
• Kufanya mijadala ya wazi katika sehemu ambazo viongozi wa MWAFO wataona zinafaa.
• Kusambaza elimu ya uraia kwa njia yoyote ile ya mawasiliano.
Matarajio ni kwamba baada ya elimu ya uraia kutolewa kwa wengi nchi ingerudi katika misingi yake iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya upendo, umoja na mshikamano!
Baba makabrasha ya MWAFO nilikuletea ofisini kwako kule Vetenari ukiwa Waziri wa Uvuvi na Mifugo. Leo ungekuwa Rais wa Watanzania wamoja kama alivyokuwa Rais Nyerere! Ukiwaacha wazee wa Dar es Salaam zimekuja salamu kutoka sehemu zote za nchi yetu. “Komaa mwanamwema mpaka kitaeleweka. Mungu yuko nawe kwa kuwa unayoshauri na kukosoa ni mema kwa Taifa letu na kwa wana wa Mungu pia!”