Ndugu Rais, nilipoandika kuwa, ziko sikukuu nyingi ambazo unaweza ukaamuru zifanyike sehemu mbalimbali za nchi kama kutia hamasa, lakini si siku ya uhuru wa nchi, Watanzania wengi, hasa wazee kutoka kila kona ya nchi yetu walionyesha kuguswa sana.
Wazee walioshuhudia tukio la Tanganyika kupata Uhuru katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) wamekiri kuwa haikuwa sahihi kufanya kumbukumbu ya siku ya Uhuru wa nchi yetu Mwanza au mahali pengine popote ambapo si Dar es Salaam.
Kwa umri wao, baadhi ya viongozi wetu siku ya Uhuru walikuwa bado wadogo sana. Hata hawakujua kilichokuwa kikifanyika katika Uwanja wa Taifa siku hiyo. Busara, wasiwe wababe, wakubali kujifunza.
Tungewauliza wazee, mbona wengine wengi tu bado wapo? Mkubwa haambiwi ulikosea ila unaweza kusema tulipotoka. Baba wa Taifa alisisitiza umuhimu wa viongozi kukubali kujisahihisha.
Kama hakuna nia yoyote ovu katika uamuzi ule ni matarajio ya wengi upotoshaji huu utarekebishwa na hautajirudia. Kwa mamlaka tuliyopewa yatulazimu tusome kwa makini historia ya nchi yetu tusije tukajikuta tunaikanyagakanyaga halafu historia hiyohiyo ikaja kutuhukumu.
Hapa baba ninakuwekea baadhi ya meseji za baadhi ya wazee wetu wenye busara. Simu ni nyingi za kunitia shime! Mzee wangu Ernest Mashuda kutoka Nzega, Tabora akaniandikia: “Mwalimu Mkuu! Naomba niseme tu kuwa, wewe ni mdomo wa Mungu wetu! Tazama unavyoililia nchi yetu, ninakufuatilia sana kwenye fikra za Mwalimu Mkuu ila cha ajabu sioni kama baba yetu na kardinali pamoja na viongozi wetu wa kiroho wanaongozwa na roho wa Mungu kweli, kwani yaonyesha ni kama wanatumiwa… Kenya ni majirani zetu, yaliyowatokea yanawafanya waanzishe BBI. Sisi ndiyo kwanza tunatumia ubabe kusababisha mifarakano! Mzee P. Mayega ninakuombea kwa Mungu uendelee na uzalendo huu kwa nchi hii. Nimeguswa mno na makala yako, ndani ya Gazeti la JAMHURI, toleo 429, Jumanne Desemba 17-23, 2019. Ubarikiwe sana mtumishi wa Mungu. Ndimi mzee Ernest Mashuda, Nzega.”
Wanawema kutoka Iringa kuna wazee wengi. Katika hili mzee wangu mstaafu aliandika: “Naam! Hivyo ndivyo tunavyovipotosha vizazi vipya. Kwamba Union Jack iliteremshwa Mwanza na Bendera ya Tanganyika labda ilipandishwa Songea. Na pengine labda Capt. Alexander Nyirenda aliwasha Mwenge wa Uhuru Mlima Meru, kwa vile nao ni mrefu wa haja!
Mwalimu Mkuu Paskally, kweli historia inajirudia. William Shakespeare katika igizo la King Henry V, anaandika hayohayo unayoyaandika leo. Kwani igizo hilo mfalme anajifanyia tathmini na kugundua kuwa ijapokuwa raia wanatetema mbele ya mfalme na kumwona kama Mungu, kumbe kwa upande wake mfalme ana hofu kubwa kuliko raia wanaomwabudu yeye mfalme!”
Mzee wangu mstaafu Ndunguru kutoka Iringa akaandika: “Ndugu yangu Pasco, mwenzangu una karama kubwa mno ya kukemea uovu, bila kutafsiriwa kuwa mchochezi. Kwa makala ya leo ni kama umevua gamba kwamba litakalotokea na litokee. Hii ndiyo hofu yangu kwako. Lakini ndiyo ukweli. Watawala hawa wa zama hizi hawatuunganishi bali wanatutenganisha Watanzania. Vita ya Kagera ingetokea leo, ni wazazi wachache sana wangekubali kupeleka watoto wao mstari wa mbele!”
Anasema: “Jamani Katiba mpya si hisani wala utashi wa mtu binafsi. Ambacho hawataki kusema ni hofu ya kupunguziwa madaraka ya kuteua, kutumbua na kuidhinisha malipo badala ya kuviachia vyombo husika. Leo hii pamoja na Katiba ya sasa kuwa mbovu, kila mtu anajipendekeza apate uteuzi; si profesa, si daktari, si jaji, si spika, si mkuu wa majeshi, si mhariri, wote wanaimba wimbo wa utukufu wa mtu. Tuna heri sisi tulio nje ya mfumo.” Ni mzee Ndunguru wa Iringa.
Mzee wangu mwingine aliandika: “Naitwa Eliazar, ndugu yako katika Kristo. Ninapenda sana makala zako unazoandika katika magazeti. Hakika ninafarijika sana! Ninaamini Mungu ana sababu na kusudi nawe kukuweka hapo na kukupa maneno unayoyaandika. Ubarikiwe sana! Endelea, usiogope, usiache!
Hakika kuna maneno ya hekima sana. Tayari nimepiga photocopy kurasa kuwagawia bure wale wote waliotamani kununua na kusoma gazeti lakini hawana uwezo. Naamini Mungu ana sababu na kusudi la kukuweka hapo na kukuwezesha kufanya kazi hiyo. Ninamshukuru Mungu kutupatia maneno hayo kupitia kwako. Mara nyingi Mungu hutoa maarifa, elimu, vitu na mambo mbalimbali kupitia watu awapendao na aliowachagua. Alileta mwanae kutukomboa kupitia kwa mtu (Bikira Maria). Usiache, usiogope. Endelea kutupatia kila Mungu anachokupa ili utupatie. Bwana yuko pamoja nawe. Ni Bwana wa majeshi yote mbinguni na duniani, atakulinda. Ubarikiwe sana!”
Haya ni baadhi ya maneno mengi kutoka kwa wazee.
Imesemwa kutoka zamani kuwa baraka ya nchi imo katika maneno ya wazee wa nchi hiyo! Kudhani nchi yoyote inaweza kuendeshwa kwa mawazo ya mtu mmoja ni kujilisha upepo. Tunamfukuza jogoo. Jogoo anatoka damu na sisi tunatoka damu! Tuingie ndani tuchukue mtama tuitie kuku, yote haya tutayapata bila kuwachuna ngozi Watanzania.
Waliyonayo Watanzania katika vifua vyao ni mengi sana! Tutahubiri mengi na kuamuru mengi pia, lakini neno ni moja tu kubwa kuliko yote, upendo. Upendo miongoni mwetu. Taifa limesawajika lakini limesawajishwa na baadhi ya viongozi wetu ambao kwa upofu wao wanajiona wao ni wao na wale ni wale. Hawana uelewa wala fahamu kuwa wote tuliomo katika nchi hii ni sisi.
Nchi ni yetu wote tuliyopewa na Muumba wetu katika umoja wetu. Hakuna mwenye haki zaidi kuliko mwingine. Wanaohubiri mifarakano wanaifanya kazi ya shetani. Wajue kuwa hawatafaulu lakini watawaingiza watu wa Mungu katika ghasia kubwa.
Tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, baba wapange watu wa Mungu wakamchague mcha Mungu atakayewaunganisha Watanzania pamoja. Watanzania eleweni kuwa nyinyi ni wamoja tangu enzi za Julius Kambarage Nyerere, hata kabla yake. Hakuna aliye mkubwa kuliko nchi. Asiyetaka maridhiano huyo si mwenzenu, hawafai!
Wenzetu wa Kenya wanaifaidi amani ya kweli inayojengwa na BBI, mawazo halisi yaliyoasisiwa katika nchi yetu, juu ya ardhi yetu na wana waliotokana na udongo wa nchi hii. Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Yakobo awaepushe na ushetani wa shetani aliyeupitia uchaguzi uliopita.
Mwisho