1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliNdugu Rais, tunaandika hapa kukusaidia wewe ili uwahudumie wananchi wako kwa namna ipasayo. Unaweza ukawa unafanya mambo mengi makubwa, lakini wananchi wakawa hawana furaha na wewe kwa sababu ya jambo moja tu au mawili unayowakera sana.

Hivyo utakuwa umefanya vyema kama utatutegea sikio lako kwa maana tuandikayo ndiyo maoni ya wananchi.

Kadri siku zinavyokwenda ndivyo baadhi ya kauli na maagizo yako yanavyoonekana kutoeleweka vema kwa wananchi. Kama ufafanuzi hautolewi na wahusika kwa muda mwafaka utajikuta umewekwa kando na wananchi ambao mwanzo walikuona kama u mwenye dhamira ya kutaka kuwasaidia.

Tukifikia hapo nchi itakuwa imeshindwa. Tutaanza kutafutana na kumwona kila asiye wetu kuwa ni adui. Machafuko na ghasia za kumwaga damu katika nchi nyingi, hasa za Kiafrika huanza kwa kauli za kipuuzi.

Agizo la mkuu wa nchi ni amri. Na ni amri zaidi kwa watekelezaji ambao, ama kwa ushabiki wao wa kinafiki, au kwa ujinga wao, huamua kutekeleza agizo la mkuu wa nchi bila kufikiri sawa sawa na hivyo kuibua hofu, wasiwasi na sintofahamu katika jamii. 

Amri zikizidi hudumaza jamii na kushawishi usugu. Zikitolewa kwa jazba na ukali mwingi husisimua mishipa ya ufahamu ya kutaka kuthubutu. Jamii iliyojaa hofu na wasiwasi haiwezi kufanya mambo ya maendeleo. Muda mrefu hutumika kwa malumbano na mikwaruzano isiyokwisha. Hayo yanapotokea kero za wananchi husahauliwa hivyo hazitatuliwi.

Viongozi wanajishughulisha na kazi moja tu, kujibizana na washindani wao. Mwisho wa hadithi Serikali inajikuta katika kipindi chake chote haijafanya kitu kinachoeleweka. Ubovu, unyang’au na wizi wa baadhi ya viongozi ndivyo vinavyoustawisha upinzani na kuupa nafasi ya kukubalika kwa wananchi.

Hivyo, jambo lolote linalofanywa kwa lengo la kuudhoofisha upinzani, hufanywa na viongozi wasiokuwa na busara. Wasio na uelewa wa kujua kuwa kufanya hivyo ni kuufanya upinzani ujulikane zaidi. Kiongozi aliyejaliwa busara na hekima atakazana kuwaondoa viongozi wabovu, manyang’au na wezi katika utawala wake kwa kuwa akifanikisha hilo, upinzani utajiteremsha wenyewe. Utakosa cha kuwaambia wananchi. Lakini ni viongozi waliofilisika kisiasa tu ndio wanaodhani wakitumia mabavu wanaweza kuufifisha upinzani. 

Awamu ya tano ilipoanza kwa kutumbua majipu, kuziba mianya ya wizi katika makusanyo ya fedha za Serikali na kubana matumizi upinzani ulitulia tuli! Ilipotolewa amri ya kuzuia mikutano hadi mwaka 2020 imeibua nguvu kubwa walionayo wapinzani. Leo kila mwananchi anahofia Septemba Mosi. Wananchi wamejawa hofu kubwa! Ulimi hauna mfupa, lakini ukitumika vibaya unakata kuliko upanga!  Kwanini baadhi ya viongozi wetu hawajifunzi busara na hekima za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere? Alisema: “Kama wapo wanaotaka kumbeba (Mrema), waacheni wambebe hata kama watakuwa wanapokezana kama machela!”

Lakini baba kabla ya kutoa agizo hilo tulisoma Katiba ya nchi tulioapa kuilinda inasemaje? Kwa agizo hilo hatuoni kuwa tumewafanya wanaosema umevunja Katiba waonekane wanasema kweli? Kuvunja Katiba ya nchi ni uhaini! Kinachotutisha wakikutana, mpaka tunatetemeka hivi ni nini?

Ni kweli, wakienda kwa wananchi watawaambia yaliyomo katika mkataba tata wa Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi. Ulisema mwenyewe kuwa kule polisi kuna jamaa kalipwa mabilioni ashone sare, lakini hajashona hata shati moja, watawaambia wananchi. Wanaweza hata watawatajia wezi wa ‘esikroo’.

Kama unaona haya yanaweza kuamsha hasira za wananchi, si uyatumbue kabla hawajaenda? Unadhani yatabaki siri hadi lini? Hakuna mwenye busara anayeweza kusema waacheni wakutane? Nchi inaongozwa kwa mujibu wa Katiba na sheria. Hii mamlaka inatokana na Katiba ipi au sheria ipi? Yatubidi tujitafakari, tusije tukajikuta tumeiingiza nchi katika vurugu na ghasia kubwa kwa kudhani tu kuwa sisi ni wababe!

Ndugu Rais, upinzani katika nchi hii haukuanza leo. Uko kila mwaka na kila awamu. Uko kihalali na kisheria pia. Ni kweli unazidi kuimarika na kukomaa kadri siku zinavyozidi kusonga. Siasa za ushindani katika nchi zilizostaarabika ndiyo msingi wa kuwa na utawala ulio bora. Walioko madarakani hulazimika kufanya mambo ya maendeleo kwa nchi na wananchi kwa kuhofia upinzani. 

Wapinzani nao hulazimika kuikosoa serikali iliyoko madarakani kila inapojisahau au kukosea. Ushindani huu unapoendeshwa kidemokrasia maendeleo ya kweli ya nchi na wananchi hupatikana kwa kasi. Lakini ushindani huu unapogeuzwa kuwa ugomvi, machafuko katika nchi huwa hayaepukiki. Na mara nyingi walioko madarakani ndiyo husababisha machafuko hayo! 

Tumeyaona katika nchi nyingi! Na hapa kwetu wasiwasi na hofu ya ghasia kubwa ndiyo maongezi kwa kila unakokwenda!

Hatuoni watu makini wakijitokeza kusawazisha hali hii yakusikitisha! Tulitarajia viongozi wa dini wangeiona hofu iliyowajaa watu wa Mungu wakamsujudu Muumba ili awaondolee hofu hiyo kwa kuwalazimisha viongozi wa pande zote mbili kutumia busara na hekima badala ya ubabe, nguvu na vitisho.

Chakushangaza, wameonekana baadhi ya viongozi wa dini wakiwa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere eti wanauombea uwanja wa ndege unaojengwa! Unaweza ukacheka. Ni nani hawa hata wakague miradi ya Serikali?

Tamaa ya fedha na ukubwa vikimtawala mwanadamu vinaweza kumfanya afanye mambo kama mwendawazimu wakati si mwendawazimu. Daraja la Kigamboni (Daraja la Nyerere) halikuombewa, watuambie lina kasoro gani? Kiwanja kimekamilika, si wangeenda wakaombee ujenzi wa reli mpya ambao haujaanza kujengwa? Tulisema huko nyuma kuwa kama elimu maana yake ni kujua, basi kuamini usipojua ni kinyume chake!

Ni kwa fedha tu Bwana Yesu alisalitiwa! Ni kwa fedha tu wameacha misikiti na makanisa yao. Wamepumbazwa na anasa za kidunia! Mambo ya Mungu wamemwachia Mungu afanye mwenyewe! Hatujui kule misikitini kwao na kwenye makanisa yao waliwaachia nani wakaimu! Lakini, vikundi vyote ambavyo vipo nchini ambavyo havitambuliwi na Katiba wala sheria za nchi ni vikundi vya wahuni!

Ndugu Rais, tulikoanza tulianza vizuri sana, lakini huko tunakokwenda siko kabisa! Kunatisha kama nini! Baba tusikilize tunayokwambia! Amri yako ya kukataza maandamano na mikutano hadi mwaka 2020 ifafanue kabla haijaingiza nchi katika ghasia kubwa!