Ndugu Rais wananchi wa nyakati hizi wamechoshwa na makelele ya wanasiasa. Wanasiasa kwao wamekuwa ni laghai. Kinachofanyika katika nchi hivi sasa siyo siasa, ni chuki, ufitina na kukomoana! Walio na madaraka na wanaotafuta madaraka wamepumbazwa na uroho wa madaraka.
Mwananchi sasa hana nafasi katika siasa hizi.
Ndugu Rais, nimekuwa nikiwalilia Watanzania wenzangu kuwataka watambue kuwa katika nchi hii hakuna chama cha ukombozi na wala hakuna mtu wa kuwakomboa, bali wanatakiwa wajikomboe wao wenyewe. Hakuna mwanasiasa hata mmoja ambaye anashindwa kupata usingizi nyumbani kwake eti kwa kuyaona mateso ya masikini wa nchi hii. Anayedai kuwateteawanyonge na masikini mpuuzeni, awe na mamlaka au awe hana mamlaka.
Wanaendesha maisha ya ufahari katikati ya ziwa la wanyonge. Ukitaka kuwatetemesha watamkie neno ‘Azimio la Arusha’. Wote wanagwaya!
Watawala hawataki kulisikia na wapinzani nao hawataki kulisikia kwa sababu hili, na ni hili pekee ndiyo ukombozi wa kweli wa masikini na wanyonge wa nchi hii!
Wameanza kunielewa na sasa wanataka mahali patakapowaunganisha tena.
Mahali ambako hawataendekeza tofauti zao ziwe za kiitikadi, kidini, kikabila au kikanda. Mahali watakapojiona kuwa kumbe nchi hii ni yao wote na wao ni watoto wa mama mmoja- Tanzania! Mahali watakapoacha vyote na kwa pamoja waseme nchi yangu kwanza. Mahali hapo ni Jukwaa la Mwalimu Forum kwa kifupi MWAFO. Baba kwa kuwajengea watu wako MWAFO utakuwa unawajengea umoja na kuwatoa kwenye utengano.
Ndugu Rais miaka kadhaa iliyopita lilizuka neno ‘ufisadi’. Nasema lilizuka ingawa lilikuwapo kwa sababu walitokea manabii wa uongo kumi na mmoja, ambao walibadilisha maana ya hilo neno na wakalitumia kupandikiza chuki katika nchi yote. Walifanikiwa kuuondoa upendo uliokuwa umetamalaki kati yetu na kuuparaganyisha umoja wetu na mshikamano tuliokuwa nao! Kwa unyama wao waliigawanya nchi yetu nayo ikawa katika vipande vipande! Siasa za Awamu ya Nne zilijaa chuki na fitina. Walipopewa vyeo walivyoahidiwa wakanyamaza na kuwaacha wajinga waliowatengeneza wakibaki na fikra potofu kuwa fisadi ni mwizi!
Ndugu Rais, kuna wezi walioukomba utajiri wa nchi yetu bila huruma.
Hawajaguswa. Uliposema hutaki kufukua makaburi uliwafariji sana. Lakini baba kunyosha si kukunjua? Hii mikunjo ya ESCROW, LUGUMI, EPA na sasa RUZUKU YA CUF kama hainyosheki nchi itanyokaje? Ruzuku ya CUF watu wanajipigia hela za wajinga (wananchi) watakavyo!
Baba leo tuna neno uchochezi. Nalo kama ilivyokuwa kwa neno ufisadi limeongezewa maana. Nalo limewagawa Watanzania kwa kueneza chuki kati yao, lakini mbaya zaidi, visasi vingi vinatengenezwa!
Kwa kukosa dira watumishi na watendaji wengi wa serikali hawajui wafanye nini bosi wao ujue kama wanafanya kazi. Wanachofanya badala yake ni kupuyanga tu. Ziko shule nyingi katika nchi hii, si Mtwara tu, ambazo zina upungufu mkubwa wa walimu. Ni kawaida kukuta shule ina wanafunzi kwa mamia, lakini ina mwalimu mmoja au wawili. Nyingine ni za nyasi na nyingine miundombinu yake inasikitisha. Tutajifanya wajinga kutegemea ufaulu kutoka kwa wanafunzi wa shule hizi. Na tutajifanya wajinga zaidi wanafunzi kutoka katika shule hizi wanapofeli, tukawatwisha walimu lawama. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu ameamuru walimu wakuu wa shule 63 wavuliwe nyadhifa zao.
Ndugu Rais, wakati Mama Halima anajifariji kuwa angalau ametumbua hivyo utamwona, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania, Gratian Mkoba, amesema mkuu huyo wa mkoa hana mamlaka kwa mujibu wa sheria za nchi kumshusha cheo mwalimu. Alichofanya ni kuvunja sheria. Anasema kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2005 na Sheria ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2005 na kanuni zake za mwaka 2016 mkuu wa mkoa si mamlaka ya nidhamu. Akaongeza kuwa hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu, Waziri, Mkuu wa Mkoa au Wilaya au yeyote hana mamlaka ya nidhamu juu ya mwalimu. Kwa mujibu wa sheria, Tume ya Maadili ya Walimu ndiyo yenye wajibu wa kufanya hivyo. Mama yetu hili katika akili yake halimo! Hawa ndiyo viongozi wetu!
Wakati Halima Dendegu akipuyanga; Geita nako wanapuyanga. Uchaguzi mkuu uliopita Baba ulitangazwa mshindi ukifuatiwa na Edward Ngoyayi Lowassa aliyechaguliwa na mamilioni ya watu kutoka katika kila pembe ya nchi hii! Ndiyo kusema baada ya wewe baba, Edward ndiye Mtanzania anayependwa na Watanzania wengi zaidi. Ana Watanzania wengi sana nyuma yake. Ni mtu muhimu sana kwa amani ya nchi yetu. Inapotokea amekwenda sehemu nyingine ya nchi wapenzi wake wa huko hutumia fursa hiyo kusalimiana na kipenzi chao. Katika nchi inayoheshimu uhuru wa raia kuna ubaya gani? Idadi kubwa ya wanaokusanyika ndiyo kipimo cha umaarufu na heshima kubwa aliyonayo mtu huyo katika jamii yetu! Waacheni Watanzania wambebe mtu wao kama hawavunji sheria!
Baba, vijana wako waandishi wa habari ambao wao walikuwa hawamsalimii mtu yeyote, polisi waliwapiga na baadhi yao wakavunjiwa vitendea kazi vyao na vingine wakanyang’anywa. Wananchi nao walipigwa. Baba, wananchi walikosa nini mpaka wapigwe? Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mponjilo, alisema walimkamata Lowassa kwa sababu ya usalama wake; kwani wananchi waliopigwa na polisi na waandishi wa habari walikuwa wanamshambulia Lowassa?
Ndugu Rais, polisi aina ya Latson Mponji wanapomkamata Lowassa katikati ya umati wa watu bila kosa lolote eti kwa usalama wake, haiwezi kuwa ni njama za kumjengea umaarufu ili apate huruma ya wananchi? Haiwezi kuwa ni njama ya kuidhalilisha serikali ili ionekane inamwogopa Lowassa sana kiasi kwamba akikohoa tu serikali yote inatetemeka?
Haiwezi kuwa ni njama za kutaka kuiaminisha jamii yetu na ya kimataifa ionekane kuwa nchi inaendeshwa kiimla? Wananchi waliopigwa kule Geita bila kuwa na makosa watakupendaje wewe na serikali yako?
Baba mimi na wewe tuulizane. Ni kweli hakuna polisi wafuasi wa Lowassa katika Jeshi la Polisi? Je, hivi siyo vigezo vya kuwatambua? Latson Mponji na polisi wengine wana kila dalili za kuwa wafuasi wa Edward Ngoyayi Lowassa!