Ndugu Rais, Mei ‘Dei’ ya Mbeya imepita. Wanaotaka kujifunza wataisoma.

Lo! Maandamano yalikuwa marefu! Lo, mabango yalikuwa mengi yale, lakini yote yalibeba ujumbe mmoja unaofanana. Ulisomeka: “Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana. Wakati wa mishahara na masilahi bora kwa wafanyakazi ni sasa.”

Wafanyakazi walisisitiza nyongeza ya mishahara kwa nguvu zao zote kistaarabu. Tunasema kistaarabu kwa sababu katika nchi nyingine hali ikifikia kama hapa ilipofikia wafanyakazi huchukua hatua mbadala.

Hawa wetu wanasema sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Hivyo kama atatokea wa kukataa kuongeza mishahara, ambalo ni jambo muhimu la wanyonge hawa, itakuwa vigumu mno kwao.

Kwa yaliyotokea mwingine anaweza akasimama na kusema mtetezi wa kweli wa wanyonge Tanzania bado anayo safari ndefu ambayo labda inaweza kukamilishwa na kizazi kinginge. Wameibuka wanaotafuta fursa, hivyo kujifanya ni watetezi wa wanyonge kumbe wanawafanya mtaji wa kisiasa na kuwafanya maskini zaidi kuliko walivyowakuta.

Ah! Kambarage! Maskini wako watakulilia mpaka lini? Machozi yao yamegeuka kuwa chakula chao! Maskini wafanyakazi waliyanywa machungu ya ‘Mei Dei’ kama mtu anywavyo dawa chungu isiyotibu. Baada ya tamko la kutokuwa na ongezeko la mishahara ghafla watu wote waligeuka wanyonge. Sauti zilizokuwa zimejaa bashasha zikijibu: “Mbeya oyee,” zilififia. Zikabaki zile za kinyonge zilizosema: “Mbeya oyiiii!” Hata ilipotangazwa kuwa sasa tupunge mikono yetu juu kumuaga rais wetu, ah! Ilisikitisha! Ule msitu wa mikono tuliokuwa tunauona wakati wote ukishangilia ulitoweka ghafla! Unyonge ulitamalaki katika kiwanja chote na watu wakaondoka kama wanaotoka msibani.

Baba wewe unampenda anayekuambia ukweli. Ni mwaka kesho tu tunakwenda katika Uchaguzi Mkuu. Nina mtazamo binafsi kwamba kura zetu nyingi tumezipoteza Mbeya na katika nchi nzima kwa hili. Sasa yanasikika maneno kila mahali ya “Ah!

Wasitufanye namna hiyo.”

Baba ni wewe ulisema kuwa Watanzania si wajinga. Wana uwezo wa ‘kuanalaizi’ na kuchambua mambo. Tukidhani tukiongeza mishahara mwaka kesho karibu na uchaguzi ndiyo tutapata kura nyingi tutakuwa tunafanya kosa la kiufundi.

Mei Dei ya Mbeya imeacha fundisho. Mabango yalikuwa mengi lakini yote yalibeba ujumbe mmoja. Bango moja lilifikirisha zaidi. Liliandikwa: “Tupandishe madaraja na sisi tupande Bombadier.” Kwa nini halikuandikwa: “…na sisi tupande ndege”, badala ya kusema “tupande Bombadier?”

Bango hili yaonekana liliugusa hata moyo wako. Bombadier inayosemwa katika bango hili ni moja kati ya ndege zilizonunuliwa kwa

mpigo bila taarifa. Baba hao wote wanaodai wanataka kupanda Bombadier hakuna hata mmoja anayehitaji kupanda ndege. Kwa nini walisema wapande Bombadier wasiseme na wao wanataka wapande ndege?

Wakiwezeshwa ndege zingine ambazo si Bombadier hawawezi kupanda? Hapa jina la Bombadier limetumika tu kupeleka ujumbe uliofichwa. Shida yao kubwa haiwezi kuwa kupanda ndege. Mahitaji yao ya msingi yametekelezwa?

Tuwaache waendelee kusema elimu bure wakati hakuna elimu ya bure, lakini inawasaidia nini watoto karibu mia mbili wanaokaa katika darasa moja na mwalimu mmoja ambaye hawezi hata kupitia nusu ya madaftari yao? Maendeleo katika sekta ya afya ni tarakimu zaidi zinazotamkwa na baadhi ya viongozi wetu lakini hakuna dawa wala vifaa tiba katika hospitali zetu. Ni mambo gani makubwa ambayo mtu anaweza akajigamba nayo ambayo hayawasaidii wananchi kwa lolote?

Baba, tukubali ukweli ili twende sawa na watu wetu. Wananchi wanawachagua viongozi ili wawaongoze vile wanavyotaka wao na si wanavyotaka viongozi. Katika hili la Bombadier imekuwa dhahiri sasa wananchi hawana furaha nalo. Wanaona ni moja kati ya uamuzi ulioleta zahama kwao.

Hivi baba tungeamua kuongeza ndege moja moja hata kila mwaka kungekuwa na ubaya gani? Wananchi hawakushauriwa lakini ndege ndiyo ilikuwa shida yao kubwa? Huko tuendako na mradi huu wa ndege tutafikia mahali kutaja tu hizi ndege itakuwa vigumu.

Uliwaambia vema kuwa ahadi yako ya kuongeza mishahara kabla haujaondoka madarakani iko pale pale. Lakini haukuwaambia katika kifua chako umepanga kuondoka madarakani lini ili kuwawezesha kuhesabu siku zilizobaki mpaka nyongeza ya mshahara. Je, ni hii 2020 au ni tarehe nyingine? Majuzi baba katika ziara zako ukiwa Uyole, mkoani Mbeya uliwakumbusha watu wako kuwa ahadi ni deni. Baba hukusema walikuahidi nini na wengine wajue.

Ahadi hii isipotimizwa mwaka 2020 watu kiasi gani watatuamini? Baba uongozi wetu umekuwa kama uongozi wa mtu mmoja. Amekosekana mtu ambaye angekuwa anafuatilia matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wetu kwa lengo la kuyafuta au kuweka sawa baadhi ya matamko yanapoonekana kukera jamii.

Tishio la kufutwa kwa baadhi ya madhehebu ya Kikristu lililotolewa baada ya zile nyaraka zao, Watanzania bado wanalo vichwani. Ilitamkwa kwamba kuna baadhi ya makanisa yalikuwa yanaishi kwa kutegemea sadaka zilizokuwa zinatolewa na mafisadi. Baada ya mafisadi kubanwa yasemekana baadhi ya makanisa yamekuwa hoi kiuchumi.

Tukumbuke Mbeya ndiko alikokuwa akihudumu marehemu Baba Askofu Mhashamu Evarist Marc Chengula. Akihubiri katika ibada ya Ijumaa Kuu Machi 30, 2018 aliwataka Wakristu kwa kutumia jumuiya ndogondogo kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kwa kuchagua watu ambao hawatawafanya waishi kwa kuogopa.

Akasema ujumbe uliokuwa umetolewa na maaskofu ulikuwa haumlengi mtu fulani, bali wanafiki wanaodai ni Wakristu, lakini hawana imani ya dini hiyo ya Kristu ili waweze kubadilika na kuwa watu wema. Angekuwa bado hai Mbeya ingekuwaje?

Alitakiwa mtu atangulie kuyanyoosha haya kabla baba hajachukua beseni na kuanza kukusanya sadaka. Marais waliotangulia wote Wakristu kwa Waislamu walipoalikwa katika hafla za kidini walipofika kanisani, walisali kama waumini wengine. Mbele ya Mungu wote ni sawa.

Umekuwa na ziara ndefu mikoani ukifanya kazi njema kabisa. Hata ule utaratibu wa kutembea na fedha na kugawa kwa baadhi ya wananchi katika mazingira ya sasa unakwaza, bila shaka wananchi hawajazoea.

Baba hii nchi ni ya Waswahili. Watasema matukio ya kugawa fedha yalipangwa au watasema watu wameanza kampeni mapema.