Ndugu Rais, Mwenyezi Mungu alipomuumba Julius Kambarage Nyerere katika nchi hii hakumuumba peke yake. Aliwaumba wengi wenye busara kama za Nyerere. Ni kipi baba kinawafanya watu wako wasione kama huwatumii wanawema hawa wengi uliopewa na Muumba wako? Hii ni kasoro ambayo wengine tunaona tuna wajibu wa kukwambia baba yetu kwa uwazi. Baba, kule ulikozaliwa ulizaliwa kama watoto wengine walivyozaliwa. Ulishuhudia baadhi ya mateso waliyokuwa wanafanyiwa baadhi ya watoto na wazazi wao, hasa akina baba. Kuna baadhi ya nyumba hata kama watoto walikuwa wanacheza michezo yao ya kitoto ya usiku kabla ya kwenda kulala, walipohisi baba yao anarudi wote walitimkia vyumbani mwao tayari kwa kulala, wamekula au hawajakula.
Kazi inabaki kwa mama. Kuna wanaume hupiga wake zao hata kukaribia kuua. Baba asiye mwema hujisifia moyoni mwake, ‘Mimi si wa kuchezea!’ Huo ndiyo unyama unaofanywa na baadhi ya wanaume waliozaliwa kwa bahati mbaya! Namshukuru Mungu alinipatia baba wa kunizaa aliyekuwa mwema! Apumzike kwa amani.
Tanzania kama nchi tunao baba wa kikatiba. Baba mzazi habadiliki, lakini hawa hubadilika kulingana na matakwa ya katiba ya nchi.
Tulikuwa na baba Julius Kambarage Nyerere. Alitulisha asali na akatunywesha maziwa. Tukajisahau tukadhani baba wote wako hivyo.
Tukampata baba Ali Hassan Mwinyi. Alikuja akaondoka kama moshi upitavyo baada ya moto kuzimwa. Hakuwa na mateso kwa watu wake. Lakini kilindi alicholitumbukiza Azimio la
Arusha ndiyo moja ya vyanzo vya mateso walionayo wana wa nchi hii. Bila Azimio la Arusha “aliloliua” Mwinyi, huko tuendako tusije tukashangaa kuja kupata mababa wa hatari zaidi. Lakini ni nani wa kuturudishia Azimio la Arusha ili kuitoa nchi katika mzizimo huu?
Alipokuja baba Benjamin William Mkapa watu wakasema ni mkali. Lakini mtu huyu moyoni mwake hakuwa hata na chembe ndogo ya uovu wa kumdhuru mwananchi yeyote -wale waliompenda na hata wale ambao walimpinga.
Aliotuambia ni maprofesa uchwara, wameendelea kuwa maprofesa uchwara hadi leo. Hakimu aliyetumwa na Mungu amekataa kuubeba ushetani wake wa kutaka kujisajili uenyekiti upya alioukataa mwenyewe, Mwenyezi Mungu akiona.
Kwa kuwa Mkapa roho yake ni njema najua halali kila akikumbuka alivyouza viwanda na mashirika ya umma kwa bei ya kutupa. Baba Jakaya Mrisho Kikwete alipotambua kuwa Watanzania wameishatambua kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania ni maneno zaidi akaleta “matokeo makubwa sasa”. Wakamwacha akaenda zake!
Kwa sasa tunae baba yetu John Pombe Magufuli. Wanawema lazima tumpende baba yetu, tusimwogope kama wale baba wa mwanzo. Wenye nia njema na nchi hii lazima wamtii baba yetu. Kwa wale washika dini ni wajibu wao kumshauri baba yetu John Pombe Magufuli. Wampongeze anapofanya vyema wamwelekeze kwa unyenyevu pale ambako hafanyi vizuri sana na kwa pamoja naye wamtukuze Mungu kuiombea amani nchi yetu, ustawi wa watu wa Mungu na afya njema kwake mwenyewe na familia yake!
Ndugu Rais, nimelazimika kuyaandika yote haya baada ya kuisikia kauli ya waziri wetu wa kilimo. Waziri huyu amesema Serikali imefanya tathmini na kubaini kuwa uwezo wa viwanda vya ndani kubangua korosho ni tani 50,000 tu kati ya tani 222,000 zilizonunuliwa kwa wakulima. Ameyasema haya Jumanne, Februari 26, 2019 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Akasema kuwa uwezo wa Serikali na viwanda binafsi ni kubangua korosho tani 42,000 na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) tani 7,000.
Alisema tulitaka tubangue korosho zote nchini ila baada kufanya tathmini na kuangalia uwezo wa viwanda vyetu, tumegundua haviwezi kubangua. Uwezo bado ni mdogo.
Kufanya jambo kubwa kama hili la korosho kunahitaji tathmini kwanza halafu mtu ananunua korosho, au ananunua korosho kwanza halafu anafanya tathmini baadaye? Akaongeza kuwa Serikali haiwezi kujenga viwanda kwa haraka ili kubangua korosho hizo. Akasema zitakazosalia ambazo ni tani 172,000 zitauzwa kwa wafanyabiashara na watu wote wa ndani na nje. Hivi huku si kuwaangukia wale wale walioonekana hawafai?
Anaposema hawaruhusiwi kwenda kununua kwa mkulima, zile walizosema za gredi ya chini hawanunui wamezipeleka wapi kama hawakuwarudishia wakulima wenyewe wazifanyie watakavyo ikiwa ni pamoja na kuziuza? Miaka yote wamekuwa hawana kilio na korosho kwa kiwango hiki, leo kunani? Kama ni kweli wamezinunua zote kupitia kwa taasisi ya serikali iiyonunua maana tumeishanunua zote wasiwasi wake unatoka wapi waziri?
Mama yangu aliwaita watu hawa, ‘’Yamleka zipita nga masala yawazana.’’ Watu wanaopata akili baada ya mambo kuharibika. Hawa hawawezi kumsaidia rais wetu. Mama yangu hakusoma hata darasa moja, lakini huyu ni msomi iweje aseme haya? Au na wewe baba umekuwa mkali mno kwa vijana wako kiasi kwamba wanakuogopa kukwambia kuwa hili kitaaluma au kiuchumi haliwezekani? Wanakuacha ukakwame mwenyewe?
Sasa mnawaita wanunuzi walewale mliowaona hawafai. Wasiowatakia mema wanacheka na kujisemea kimyakimya. Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, ‘Kitabu huleta Elimu, lakini ni maisha yaletayo ujuzi’.
Mama yangu hakusoma shule, lakini amewafundisha wengi. Hata Mwalimu Nyerere alipoleta kisomo cha ngumbaru, mama alishindikana. Mwalimu alipomwambia mama sema ‘A’, mama alijibu, akisema, “mama sema ‘A’”. Mwalimu aliposisitiza nakumwambia, “We mama nimesema sema ‘A’”.
Mama naye alisisitiza akimwambia Mwalimu, “We mama nimesema sema , ‘A’”. Walimu wakajiridhisha kuwa mama amehitimu. Kipi zaidi kati ya elimu na busara?