Ndugu Rais, Mungu ni mwema. Ni mwema siku zote. Alikuwapo mwanamwema mmoja akiitwa Beni Kiko. Huyu alikuwa mtangazaji ambaye aliwavutia wasikilizaji wengi kwa namna alivyokuwa akiziwasilisha ripoti zake.
Siku ya kwanza akiwa Dodoma mnyama mkali alimshambulia mtu hadi kumuua.
Beni Kiko akaripoti. Haukupita muda tembo alimuua mtu kwa kumkanyagakanyaga huko huko Dodoma. Beni Kiko akaripoti. Wakati watu wanatafakari namna ya kuikabili changamoto hiyo iliyojitokeza ya wanyama wakali kushambulia watu, fisi akamjeruhi mtu vibaya kwa
kumuuma mkono. Safari hii Beni Kiko alionekana kuchoka. Akionyesha sononeko kubwa Katika kuripoti, Beni Kiko alisema, “Sijui vipi mkoa huu…”
Baba, tunayo treni ijulikanayo kama Reli ya Kati. Inaanzia Dar es Salaam hadi Mwanza, Kigoma na Mpanda. Imejengwa miaka mingi iliyopita.
Nakumbuka vizuri tukiwa mafrateli wa chuo cha filosofia kule Ntungamo, Bukoba tulivyokuwa ‘tunatesa’ (kufaidi) katika mabehewa yake mazuri ya daraja la pili tukitokea Itigi hadi Mwanza na wakati wa kurudi. Leo tunatembea kifua mbele tukiwaambia Watanzania huku na wenyewe wakishuhudia kuwa tunajenga treni nyingine ya kisasa zaidi na ya gharama zaidi. Hii itaendeshwa kwa umeme. Kasi yake karibu sawa na kasi ya duma; mnyama anayesadikiwa kuwa ndiye mwenye kasi zaidi duniani. Hili ni jambo jema sana. Jambo la kusifia. Hata kama haikuwa lazima leo, lakini tunaihitaji hii treni kwa maendeleo yetu ya baadaye.
Linapofanyika jambo kubwa kama hili halafu wananchi wanakutana na
habari kuwa TAZARA imeuzwa lazima watalikumbuka sononeko la Beni Kiko, “Sijui vipi mkoa huu…’’ Lakini hawa watasema, “Sijui vipi awamu hii…!”
Baba TAZARA ndiyo reli peke yake katika nchi hii inayojulikana
kama Reli ya Uhuru. Hii ni reli alama ya ukombozi hasa ukombozi wa kiuchumi. Rais wa Zambia, Kenneth Kaunda na Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walishuhudia uzinduzi wake. Lengo kwa upande wa Tanzania lilikuwa ni kusukuma maendeleo katika maeneo ilimopita reli hiyo.
Tangu ianze kazi kumekuwapo maendeleo ya viwanda katika maeneo ilimopitia, pamoja na mtambo wa uzalishaji umeme wa Kidatu na Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi (SPM Mgololo). Leo baada ya miaka 44 kupita Watanzania wanaambiwa TAZARA imeuzwa. Kama ni kweli, TAZARA imeuzwa, inauma sana!
Imebainika kuwa njia ya reli ya TAZARA imekodishwa kwa kampuni ya Calabash kutoka Afrika Kusini. Kampuni hiyo ndiyo sasa inasafirisha shehena kwa kutumia mabehewa na vichwa vyake. Sasa treni za Calabash ndizo zinazofanya kazi ambazo kimsingi zinatakiwa zifanywe na TAZARA.
Kitendo cha kukodisha njia ya reli kwa kampuni binafsi kinalenga kuidhoofisha TAZARA. Treni ni njia zake. Ukishauza njia umeuza treni.
Baba, hii haikubaliki. Huku tunajenga reli mpya wakati huku tunauza reli iliyokwisha jengwa. Maendeleo yatafikiwaje?
Ndugu Rais, watu hawa hawaiuzi TAZARA peke yake, bali na kiwanda chake cha kuchakata kokoto cha Kongolo kilichopo Mbeya. Lakini kuhusu kiwanda hicho wenyewe wanasema, “Hatujampatia mwekezaji yeyote mgodi wa kokoto wa Kongolo, isipokuwa tumesaini hati ya makubaliano na mdau mwingine ambaye tutashirikiana naye kuhakikisha tunauendesha mgodi huo vizuri na kwa ufanisi zaidi.’’
Ah! Wacha wauze. Lakini wanunuzi ni nani? Baba wanunuzi wa TAZARA si ndiyo walewale watoto wa baba mmoja na wale waliotumalizia ndege zetu zilizokuwa zinamilikiwa na shirika letu la ndege la Air Tanzania wakati huo? Nazikumbuka Boeing 737 mbili – Serengeti na Kilimanjaro, Fokker Friendship mbili na idadi kadhaa ya ndege aina ya Twinwater.
Baba, hizi ndege zilimalizikia wapi kama siyo kwa haohao wanaoitaka TAZARA yetu? Hakuna mtu aliyewahi kuchukuliwa hatua zozote. Najua sasa wamekaa mkao wa kula wakiimezea mate Ikulu yetu si walisikia uliposema mwaka huu unahamia Dodoma?
Ndugu Rais, wanaoshauri kuwa mradi wa ujenzi wa daraja lingine la Salenda ungesimama kwanza kupisha fikra mpya, hawakosei. Uamuzi wetu wa kuhamia Dodoma umeleta tofauti kubwa sana kati ya busara iliyotumika wakati ule na hali halisi ya sasa. Iko baadhi ya miradi katika Jiji la Dar es Salaam inatakiwa isimame kwanza. Tuliuza nyumba za serikali tukajenga nyingine. Kwa uamuzi wa kuhamia Dodoma nyumba hizi tunazihitaji kule. Kuzisafirisha hatuwezi na wala hatujui tutamwachia nani. Kinachogomba hapa ni kasi yakuhamia Dodoma. Mombasa ilihamia Nairobi kama vile Blantyre ilivyohamia Lilongwe. Lagos ilihamia Abuja, lakini kwa siku ngapi?
Ndugu Rais, kinachotuondolea sababu ya kutambia mambo makubwa tunayoyafanya ni huu uozo katika elimu uliotapakaa nchi nzima. Mfano, wanafunzi 108 kati ya 266 wa Shule kongwe ya Msingi ya Nakalola kata ya Mkundi, Masasi mkoani Mtwara iliyoanzishwa mwaka 1946, wanasomea chini ya miembe kila mwaka kutokana na upungufu wa madarasa. Ina chumba kimoja tu ambamo mwalimu mkuu hubanana na walimu wengine. Ina vyumba vinne vya kudumu na tisa vya muda mfupi vyenye nyufa na vilivyobomoka hata kuwaweka wanafunzi ni hatari hasa kipindi cha mvua. Wanafunzi wanaathirika kisaikolojia. Mvua ikinyesha husitisha masomo sababu hakuna sehemu ya kukaa. Hiki ni kilio nchi nzima. Kutarajia wataalamu wa kuja kuturushia Bombadier zetu au kutuendeshea treni zetu za umeme kutoka katika hawa ni sawa na kutarajia embe chini ya mpilipili.
Tutaishia kuwashwa.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutuambia kuwa tunapoililia jumuiya ya kimataifa kuitaka waiwekee vikwazo Afrika Kusini ili iachane na siasa zake za ubaguzi wa rangi, utetezi wa makaburu ni kwamba hilo likifanyika watakaoumia ni wananchi wa chini.
Utetezi wa kikaburu. Lakini Mwalimu Nyerere alisema, ikiwa makaburu wataachana na siasa zao za ubaguzi wa rangi watakaofaidika zaidi ni makaburu kuliko weusi wa Afrika Kusini. Leo ni wapi ambako kaburu hayupo? Walikula ndege zetu za Air Tanzania sasa wanaitaka reli yetu ya uhuru -TAZARA – kwa kisingizio kuwa wanaikodisha! Baba watu wako wana imani kubwa sana na wewe. Wanaamini kwa ujasiri ulionao hili halitawezekana. Kemea hadharani uovu huu na usambaratishe mara moja mipango yao hii ya kinyang’anyi huku ukimtaka waziri wako akupe maelezo yanayojitosheleza.