Ndugu Rais, Jumatano ya majivu zamani tuliita sikukuu ya majivu. Kumbe ndiyo mwanzo wa mfungo wa Kwaresma. Kabla ya Kristu waliofunga walivaa magunia. Badala ya kujipaka majivu usoni, walijimwagia mwili mzima. Kila walipopita walijulikana kuwa wamefunga. Wote walihesabiwa kuwa ni wacha Mungu.

Imeandikwa; usiibe, usizini, usishuhudie uongo, lakini haitashangaza kama siku moja waumini wa kweli wakaja kuwashuhudia wezi, wafifishaji wa haki za raia, watekaji, makahaba, watesaji na wauaji wakijijumuisha katika kujipaka majivu usoni. Majivu si muhimu. Muhimu ni kubadilika moyoni na kuwa watu wema baada ya kupakwa majivu kama alivyotuasa marehemu Baba Askofu Marc Chengula!

Majivu kwa imani ni kama njiwa. Ni ishara ya unyofu na unyenyekevu. Anayekubali kupakwa majivu anakiri mwenyewe kuwa ametenda dhambi na kama si mnafiki kwa majivu haya anatafuta toba asamehewe.

Wako watu ambao wanadhani wanaweza kumfanyia unafiki hata Mwenyezi Mungu. Wanasogeza nyuso zao zipakwe majivu lakini hawabadiliki chochote katika mioyo yao. Wanaigiza ili watu wengine wakiwaona wawadhanie kuwa ni wacha Mungu. Hao hawamdanganyi Mwenyezi Mungu, wanajidanganya wenyewe! Ole wao kwa ujinga wao!

Katika maungamo tunaambiwa, ili usamehewe dhambi zako lazima kwanza ujutie kwa kuzitaja mbele ya Muumba wako dhambi zako hizo ulizozitenda. Kama ulimkosea jirani useme na umwombe akusamehe. Kama uliiba, rudisha kwanza mali uliyoiba. Kama uliua, mjutie Mungu wako ukawaone viongozi wako wa dini. Kisha ujiapize kuwa umebadilika na kwamba hautatenda tena dhambi hizo.

Kama aliyepakwa majivu na kubadilika katika moyo wake ni baba au mama, basi upendo katika nyumba yao utatamalaki kuliko mwanzo. Kama ni daktari, basi wagonjwa wake wanaweza kupona hata kwa kufarijiwa tu. Kwa kiongozi wa jamii katika nchi aliyekubali kupakwa majivu usoni na moyoni akabadilika, nchi nayo hubadilika. Upendo, amani, umoja na mshikamano vitaijaza nchi. Kiongozi ana nafasi ya kipekee. Baada ya majivu ni kubadilika na kuwa mwema, vilio, maumivu na mateso ya wananchi vilivyotamalaki katika nchi, vyote vitakoma.

Atawatua mzigo wa simanzi na maswali waliokosa majibu kwa muda mrefu. Watamuomba achunguze nani aliyeamuru ipigwe risasi ndani ya daladala lililokuwa limesheheni abiria.

Aliyekuwa Rais wa Kenya, Daniel arap Moi, hakujipaka majivu usoni. Lakini alipojua kuwa urais una mwisho alibadilika. Kwa mdomo wake mwenyewe alisema: “Mimi sasa nitastaafu. Nitakwenda kuishi huko kama raia mwema. Kama kuna mtu alitukana mimi, ninamsamehe. Na kama kuna mtu nilisema kitu kwake kikamuumiza, ninaomba anisamehe. Mimi naondoka lakini msiweke siasa zenu kwa chuki.” Baba Moi akawausia Wakenya, akastaafu. Na sasa ametangulia mbele ya haki.

Sisi siku zetu zikimalizika, tutawausia nini Watanzania ambao mioyo yao katika kipindi hiki chetu imepondekapondeka?

Si jukumu la yeyote kumlaani yeyote aliyepakwa majivu naye akabaki bila kubadilika. Mwachie Muumba wake kwa sababu yeye ndiye mwenye neema au laana juu ya kichwa chake. Kristu Yesu alipokuja ndiye aliagiza kuwa mnapofunga acheni kujionyesha kuwa mnafunga kwa sababu mkifanya hivyo thawabu zenu mtakuwa mmezipokea mkiwa hapa hapa duniani. 

Akasema baba yenu anaiangalia funga yenu ndani katika roho zenu. Sijui zilitumika kilo ngapi za majivu Jumatano ya majivu iliyopita, lakini ni kilo ngapi za majivu yaliyobarikiwa walipakwa ambao hawakustahili?

Bashiru Ali ameiongezea ‘kiki’ kauli ya Baba Askofu Bagonza. Baba Askofu Bagonza alisema: “Kuna watu walipata elimu ambayo haikuwaongezea maarifa yoyote.” Elimu bila maarifa ni sawa na bisi zinazokaangwa kisasa. Hata ujaze mdomo wako vipi, ukitafuna unga unaopata ni kidogo mno. Elimu yako haina maana kwa jamii.

Hakuna timamu ambaye alimtegemea Bashiru Ali naye akapakwe majivu. Si imani yake. Lakini kubadilika katika moyo na kuwa mtu mwema ndiyo mawaidha na mahubiri mema ya kila dini iliyo njema. 

Bashiru atabadilika? Tunaomfahamu vizuri Mwalimu Nyerere, angetokea leo kwa hakika angesema Katibu Mkuu wa chama chake, CCM, Bashiru Ali, hana lolote la maana analolifanya kwa ustawi wa Wana CCM na wananchi kwa ujumla. Amebaki kujishughulisha na vijitu vidogovidogo tu, yeye anaviita madiwani.

Hapa ndipo inapojidhihirisha elimu bila maarifa. Madiwani ni wapigiwa kura, wafa maji kama yeye Bashiru na chama chake. Unatumia rasilimali nyingi kuwarubuni wapigiwa kura. Elewa Bashiru, katika Uchaguzi Mkuu ujao hata wote wakikipigia kura chama chako, kura utakazopata kwao hazitazidi kumi na moja. Kwa nini usitumie hizo rasilimali nyingi kuwafuata wananchi wenyewe wanaotoa hizo kura?

Sijui kwenu, lakini kaskazini hii ni biashara kichaa. Bashiru Ali, baba alisema Watanzania si wajinga. Hata wakinyamaza mioyo yao si ‘clear’ (safi). Msione wananchi hawasemi mkadhani ni mabwege. Wapelekeeni shilingi milioni 50 mlizo waahidi wakati wa kampeni. Kama hamkuwapelekea mtayaona matunda ya kuwapatia wananchi ahadi za uongo mwezi wa kumi. Kuwaambia mmewachimbia matundu ya vyoo kwa hizo shilingi milioni 50 ni sawa na kuwatukana wananchi.

Katika ziara zenu mnazojitwisha viroba vya mapesa mengi, ni kijiji gani mlipita mkakuta wananchi hawana shida ya maji? Ni wapi mlisimama kulitatua tatizo hilo? Mwezi wa kumi ni pua na mdomo. Hivi kweli kupata watu kumi kutoka Mbeya ambao Kinana angewaita makapi, unaweza kuitisha vyombo vyote vya habari vya nchi hii na kulitangazia taifa? Aliyoiita mizigo Bashiru Ali anaona kivuno. Hii ni kazi mufilisi.

Wana CCM na Watanzania kwa jumla walimwita Kinana ‘jembe’ kwa sababu aliacha kitanda chake cha thamani nyumbani kwake, akaiacha hata familia yake kwa miezi kadhaa, akaenda vijijini kule waliko wananchi wanyonge na maskini. Alikula nao matembele, kauzu na mlenda huku akiwasikiliza kero zao. Alijua kuwa hawa ndio wapiga kura.

Bashiru mtaji ni wapiga kura, si wapigiwa kura. Nao wanyonge na maskini walimpenda Kinana, wakamwamini, hivyo wakarudisha imani yao kwa Chama Cha Mapinduzi ambacho walikuwa wamekitoa katika vifua vyao. 

Tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu tujiepushe na ukuwadi, ushabiki wa vyama na ufuasi wa mtu kivuvuzela. Tuitangulize amani ya nchi yetu. Wote tuimbe: “Nchi yangu kwanza.” Fahari ya kiongozi mwema ni kupendwa na wananchi anaowaongoza!