Ndugu Rais, kati yetu sisi wote hakuna atakayekufa halafu jeneza lake lihifadhiwe darini au juu ya mti kama mzinga wa nyuki. Bila kujali litakuwa na thamani ya kiasi gani, lakini jeneza litafukiwa chini, udongoni!
Na hapo ndipo patakuwa utimilifu wa maneno matakatifu kuwa mwanadamu kumbuka wewe ni mavumbi. Mavumbini ulitoka na mavumbini utarudi! Heri yao waaminio katika uwepo wa Mwenyezi Mungu kwa maana wataivuna pepo!
Ndugu Rais, kumbukumbu za dunia hii zinatukumbusha kuwa hapo zamani, hizi dini zetu na viongozi wake zilikuwa na nguvu mbele ya mwanadamu kuliko viongozi wa kidunia.
Kwa kuzishika dini zao kulingana na matakwa ya Mwenyezi Mungu, wengine hata waliweza kuongea na Mwenyezi Mungu moja kwa moja. Naye Mungu alikuwa karibu nao na karibu ya waja wake.
Tumeona katika mfano wa Shadrack na wenzake wawili waliotupwa katika tanuri la moto. Kwa mshangao wa waliowatupa Shadrack na wenzake wawili, hawakuunguzwa na ule moto. Lakini pia walimwona mtu wa nne ambaye hawakumtupa akiwa kati yao. Huyo alikuwa Mungu mwenyewe. Viongozi wa serikali na wafalme waliokuwa na nguvu za kutisha na walioitawala dunia kwa upanga wa moto walimsujudia Mungu wao kupitia dini hizi.
Lakini hiyo sasa inaonekana ilikuwa zamani. Siku hizi tuna baadhi ya viongozi wa dini wanafiki sawa na baadhi ya viongozi wenye mamlaka za kidunia. Wameingiliwa na shetani kwa tamaa zao za mali na madaraka wakaiuza heshima yao kwa viongozi wa kidunia.
Na tukiendelea hivi muda hautapita sana dini zetu zitakuwa sawa na mzaha upitao. Nyumba zetu za ibada zilipaswa kuwa nyumba za kufanyia utakatifu kulingana na imani za dini husika.
Lakini sasa kinachoonekana kwa baadhi ya viongozi wa dini ni wao kuwatumikia baadhi ya viongozi wa kisiasa na hasa walio na mamlaka. Tulishuhudia kiongozi wa kisiasa mwenye mamlaka akialikwa kanisani akaungane na Wakristu katika ibada ya kumsimika Padre kuwa Askofu. Ikiwa yeye si Mkristu na haamini kuwa Yesu Kristu ni mwana wa Mungu aliyehai atashirikiana vipi katika ibada ya Kikristu kama hii?
Tulimwona tena kiongozi mwingine wa kisiasa mwenye jina la Kikristu akiwa amekaa msikitini huku masheikhe wakiwa wamemzunguka eti wanamwombea dua. Huyu ambaye haamini kuwa Mtume Mohamad (SAW) ni mtume wa Mwenyezi Mungu, dua hizi zinamsaidia vipi kama siyo kumtapeli? Na yeye na Ukatoliki wake akaahidi kuwajengea msikiti. Yote haya yamekuwa kutokana na udhaifu na tamaa za baadhi ya viongozi wetu wa dini.
Kiongozi Mkristu kushiriki ibada ya Kiislamu ni unafiki mkubwa sawa na kiongozi wa Kiislamu kushiriki katika ibada ya Kikristu kwa sababu dini ni imani.
Baadhi ya viongozi wa dini wameonekana kuelekeza fikra zao kwa viongozi wa kisiasa na kusahau kuwa wajibu wao wa kwanza ambao ni kuwahudumia waumini wao kiroho na kimwili.
Viongozi wa dini wakitimiza jukumu lao la kukemea maovu na kuhubiri upendo kwa waumini wao ndipo amani ya kweli inapotamalaki. Na katika hali hiyo, viongozi wa kisiasa wanakuwa wamerahisishiwa kazi ya kutawala. Badala ya kutawala kwa mabavu wakitumia mikuki na mawe au risasi na hivyo kumkosea Mwenyezi Mungu mwenyewe, watatawala kwa baraka za Muumba mwenyewe. Utawala uliokosa baraka za Mungu unapaswa kuwa ni kero kubwa kwa viongozi wa dini.
Dini zinapaswa kulinda usalama wa waumini wao. Katika nchi nyingi mbali na dini serikali ndiyo yenye jukumu la kulinda usalama wa raia.
Serikali makini kote duniani zina vyombo mahususi vinavyoshughulikia usalama wa raia wake. Vyombo makini vilivyoenea kimaadili na kiweledi haviwezi kushindwa kwa namna yoyote na tishio kubwa linalowakabili raia. Vyombo vya usalama wa raia kusimama hadharani na kukiri kuwa watu wanaowateka na kuwatesa raia vimeshindwa kuwabaini ni kukiri udhaifu.
Kukiri kuwa watu hao kwao hawajulikani ni kuifedhehesha serikali. Lazima tuilinde heshima ya serikali. Na serikali nayo lazima iilinde heshima yake kwa kuwachukulia hatua wanaoeneza uchochezi huu kuwa serikali inaweza kushindwa kuwalinda raia wake kwa kuwa na watu wasiojulikana. Serikali makini huwajua watu wake wote.
Ndugu Rais, itakapotokea hali hiyo viongozi wa dini wa ukweli wanapaswa kuchukua jukumu la kuwatetea waumini wao. Waliokaa kimya hadi sasa hawamtumikii Mungu. Ni vibarua kama vibarua wengine wanaohangaikia matumbo yao. Siku inakuja watakapotakiwa kueleza namna walivyolitumia jina la Mwenyezi Mungu.
Na kwa sababu hiyo kauli walizotoa baadhi ya maaskofu katika ibada ya Krismasi mwezi uliopita, zitaendelea kutukuzwa na watu wote wamchao Mungu. Utukufu uwe kwa Mungu juu mbinguni na duniani iwepo amani ya kweli.
Ndugu Rais, tulitoka mavumbini na mavumbini tutarudi. Tutakumbukwa kwa lipi? Leo dunia inapohangaika kutaka Julius Kambarage Nyerere atangazwe kuwa mtakatifu siyo kwa sababu ya majengo au barabara alizojenga.
Ni kwa sababu aliwatunza na kuwatumikia vema watu wa Mungu. Hakuwajengea chuki miongoni mwao bali upendo, umoja na mshikamano.
Nyerere aliwasomesha wana wa nchi hii tangu shule ya msingi mpaka wakamaliza vyuo vikuu kwa kodi tu ya wazazi wao. Leo inafanyika dhambi kubwa katika elimu. Wazazi wanawakopesha wana wao ada ya shule. Akijua kuwa ni haki ya mtoto kusoma mpaka mwisho kwa kodi ya mzazi wake, hakuna mahali Nyerere aliposimama na kujivuna kuwa alitoa elimu bure.
Alimtibia tangu aliyeumwa kidole mpaka aliyepasuliwa moyo kwa kodi yao. Leo waganga wetu wanawaandikia wagonjwa wao dawa za kununua, bila kujali kama wana hela au la.
Baba Mwenyezi Mungu amekutuma uhangaike na makinikia kwa faida ya watu wako. Kama kuna mtu ‘hakuimpresi’ huko usimwongezee mtu. Mwondoe, huyo mweke mwingine badala yake. Tangu aliposema wakuu wa wilaya na mikoa siyo watumishi wa wananchi ‘hajamuimpresi’ mtanzania yeyote.
Alijisemea katibu mkuu, ni mizigo. Ukiangalia ukubwa na wingi wa magogo yanayopita Mbagala kwenda bandarini, utashindwa kuelewa ni aina gani ya nchi tunayowaachia wana wetu! Baba na sisi tunapita. Tulitoka kwa udongo, tutarudi kwa udongo, tutakumbukwa kwa lipi?