Ndugu Rais, imeandikwa kuwa Yesu Kristo kabla ya kuondoka, aliwaambia wanafunzi wake, “Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu kamwe hayatapita!’’

Miaka zaidi ya 2000 imepita tangu kifo chake, lakini ulimwengu unashuhudia maneno yake yangali yamesimama vilevile nukta kwa mkato mpaka leo. Na hivyo ndivyo zitakavyodumu fikra sahihi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere! Awamu zitakuja, awamu zitapita, lakini fikra za Mwalimu Nyerere hazitapita!

Tujiulize, viongozi wetu wanamuenzi Mwalimu Nyerere kutoka katika vifua vyao? Wanaitukuza siku aliyokufa. Siku mshumaa wa uzima ulipozimika! Siku nuru ilipochomoza katika nchi hii, siku aliyozaliwa haina umuhimu kwa fikra zao! Ah! Fahamu zimetutoka.

Zipo nchi nyingi sana zinazotamani Julius Kambarage Nyerere angezaliwa kwao na wapo watu ambao wanatuona Watanzania hatumuenzi hayati Julius Kambarage Nyerere kwa namna na kiasi anachostahili. Viongozi wetu wengi wamekuwa hodari wa kutumia nguvu nyingi kwa visivyo na tija. Mazoezi yao sawa na kufyatua matofali. Fikra za kuboresha matofali hayo zikikosekana wanaishia kujenga mapiramidi, majengo ambayo faida zake wananchi hawaelezwi mpaka wakazielewa. Hivyo kwa makubwa haya tunayoyafanya, wananchi wakituona tunapuyanga tu, tusikimbilie kuwalaumu. Je, wameelimishwa mpaka wakaelewa kuwa hayo siyo mapiramidi, bali ni mashamba tunalima na iko siku tutavuna? Nguvu nyingi kupita kiasi, fikra kidogo ndiyo kupuyanga.

Kwa hofu ya uwepo wa Mungu aliokuwa nao, Nyerere alikiri mwenyewe mbele ya Watanzania akasema, “Wakati tumechukua uongozi wa nchi hii, tulifanya ujinga. Tuliitazama ‘Europe’ Ulaya, tukaiona inameremeta kwa madege yao. Tulipoitazama ‘North’ Amerika na matreni yao tukaona ina- ‘glitter’, inawaka! Tukadhani yale ndiyo maendeleo. Kumbe yalikuwa maendeleo ya vitu. Maendeleo ya kweli yanapaswa kuwa ya watu.’’

Kama Mwalimu Nyerere angefufuka leo hakika angehofia kufanyika kosa lile lile walilolifanya wao wakati wamechukua nchi la kushupalia maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu. Hivyo wakija kutokea viongozi baada ya sisi kupita wenye fikra sawa na za Baba wa Taifa, hakuna atakayeyaendeleza haya makubwa tuyafanyayo. Na kwa uamuzi huo masikini na wanyonge hasa wa vijijini watamkumbatia mtu huyo kwa maana ndiye ataonekana kuwa mkombozi wao wa kweli.

Vijijini masikini wameongezewa umasikini wao na wanyonge wamekuwa wanyonge zaidi kuliko tulivyowakuta. Badala yake viongozi hao, hayo mabilioni yanayotumika kwa maendeleo ya vitu watayapeleka kwa wanafunzi 150 wa kijiji cha Kwakibuyu huko Muheza, Tanga, wa darasa la nne, tano na sita wanaotumia darasa moja wakiwa wamegeuziana migongo na wengine katikati huku wakifundishwa na walimu watatu kwa wakati mmoja.

Badala yake watayatumia hayo mabilioni kwa watoto wa masikini 342 wa Shule ya Msingi Msowola wilayani Kilosa, kwa mwalimu Elizabeth aliyewarundika chini kama mifugo katika darasa moja. Badala yake watayatumia hayo mabilioni kwa mama Anita Chavite na wajawazito wanaoishi katika kijiji cha Pangamlima, Kata ya Makole wilayani Muheza mkoani Tanga wanaodai kujifungua watoto wakiwa njiani kutokana na umbali wa kufuata huduma za afya. Watawaongezea matundu ya vyoo watoto 242 wanaotumia tundu moja.

Kwa hakika Sh milioni 50 za kila kijiji kama ahadi ingeheshimiwa zingewatoa kutoka majalalani, watoto wengi wa masikini wanaojishibisha kwa uchafu na makombo yanayotupwa humo! Kudhani baada ya sisi kuna mtu atakayeyaendeleleza haya tuyafanyayo katikati ya dhiki kuu hii waliyonayo masikini, wakati nchi ina fedha za kumwaga, tunajidanganya wenyewe.

Mwanamwema Barnabas Maro amehoji, ‘’Kumbe ahadi ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji ilikuwa ya kuomba kura kwa watu wa vijijini eh?’’ Maandiko yanasema, ‘’Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki na kwa maneno yako utahukumumiwa!’’

Kuukubali ukuu ni kuukubali ulezi wa wote. Wapo watakaokutukuza hata kukuita mfalme na wapo watakaokuona ni baba tu, lakini hukuwazaa. Wakitokea wa kukutukana wadhibiti kwa vyombo ulivyonavyo. Epuka kabisa kuwaambia wananchi kuwa unatukanwa. Wananchi hawana cha kukusaidia. Hawatakuelewa!

Baba Bashiru Ally ulipolitamka Azimio la Arusha ndani ya CCM, wengine ulitukumbusha siku ile Baba wa Taifa alipotuita nyumbani kwake Msasani. Akiwa amesimama chini ya mkungu na kwa uchungu mkubwa uliotufanya wote tuamini kuwa moyoni mwake Baba wa Taifa alikuwa analia japo kwa mdomo wake alisema, “Sijaja hapa kuzungumzia siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Najua mmekwisha iacha! Kuizungumzia kunahitaji uwe na moyo mpana kama wa mwendawazimu. Lakini, Paolo, Paolo, Paolo na nyinyi wengine (akimkazia macho Edward Lowassa), mkilitupa kabisa kabisa Azimio la Arusha…mtakuja kupata tabu sana baadaye!’’

Tumelitupa Azimio la Arusha kabisa kabisa. Tabu sana aliyotutabiria Baba wa Taifa ni huu mkosi wa watu wasiojulikana!

Ndugu zetu wanaowataka wananchi wasiwachague waliopo, bali wawachague wao watawapa maziwa na asali, walipaswa wawe ndiyo tumaini la masikini na wanyonge waliojazwa hofu hata wasiijue kesho yao.

Lakini ni yupi kati yao anayelihubiri Azimio la Arusha? Hawajitambui! Wajue kuwa bila Azimio la Arusha nao ni wale wale, hawatufai! Azimio la Arusha liliyapaka uchungu madaraka, lakini kwa kutupwa kwake, madaraka sasa ni matamu kuliko chochote. Uroho mkubwa wa madaraka unaoonyeshwa na baadhi ya viongozi wetu wa vyama vyote vya siasa, unalielekeza Taifa katika machafuko ya kumwaga damu!

Wanawema tunapoelekea Uchaguzi Mkuu 2020, vyama vyote vizingatie fikra za Baba wa Taifa alizozitoa Mbeya alisema, “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata ndani ya CCM (vyama vyao), watayatafuta nje ya CCM. Tupeni mgombea (2020) atakayekidhi matarajio ya wananchi. Tupeni mgombea anayetambua kuwa nchi hii ni nchi ya wakulima na wafanyakazi ambao wote ni masikini. Mgombea ambaye atakuwa anaelewa hivyo. Watanzania wanataka mgombea atakayeshughulika na umasikini wao. Atakayeshughulika na hali zao za afya mahospitalini. Watanzania wanataka uhuru wa kutembea na kutoa mawazo yao. Hawataki kuishi maisha ya hofu. Wakisikia mtu anagonga mlango katika nyumba zao wanahisi amekuja kuwachukua akawafunge gerezani. Tupatieni mgombea atakayetuondolea mawazo haya ya …katika nchi yetu.”