Ndugu Rais, kila anayebipu huwa hajajipanga cha kusema mpaka atakapopigiwa. Kama uliibipu Ikulu ulikuwa hujajipanga nini cha kuifanyia Ikulu endapo ungeipata. Hivyo, busara baada ya kuipata Ikulu ilikuwa ni kutulia. 

Kujinyenyekesha kwa Muumba wako, hakika naye angekupa haja ya moyo wako. Lakini ulianza kwa kutumbua. Jumapili ijayo tutakuwa tunaufunga mwaka 2016 na kesho yake tutaufungua mwaka 2017. Mwaka 2020 kwa uzoefu hakuna kitu kipya anachoweza kukifanya Rais anayemaliza muda wake. Na mwaka 2019 ndani ya CCM kutakuwa na pilikapilika za kufa mtu, kugombea uongozi ujao.

Hivyo miaka yako ya kutenda imebaki miwili tu. Ndugu Rais kama kupanga ni kuchagua basi maisha ni mahesabu. Kwa hiari yako mwenyewe unapanga kujumlisha mbili na tatu hata na nne, lakini huna hiari ya kuchagua jibu, lazima iwe tisa. Ilipotolewa ahadi kuwa mkinichagua nitaigeuza nchi yenu kuwa ya viwanda, wengi walihoji

inawezekana vipi mambo haya? Tuliishi na Baba yetu Mwenyeheri, Julius Kambarage Nyerere, mpaka kaenda ahera na hakuigeuza nchi hii kuwa ya viwanda.

Kiwanda kinachoitwa kiwanda hujengwa kwa miaka. Kipindi chetu cha uhakika ni miaka mitano. Tutajenga viwanda vingapi vitakavyoijaza nchi? Mpaka hapa hatujasema kuwa tuliahidi kisichowezekana.

Wamejitokeza watu wa kuleta za kuleta. Ofisa Biashara Mkuu wa Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo, Wilfred Kahwa,  wakati akitoa mada kwenye mkutano mkuu wa Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) mjini Morogoro, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais John Pombe Magufuli, viwanda 1,423 katika mikoa mbalimbali nchini vimejengwa huku miradi mingine 19 ya ujenzi wa viwanda hivyo ikiendelea katika maeneo tofauti.

Baba, hakuna mwenye mamlaka ya kukuambia huyu mkweze na huyu mtumbue, lakini tulio nyuma yako bila unafiki, tungesema huyu ni wa kumtafutia kazi nyingine. Hatuwezi kukubali baba yetu aonekane ni mtu asiyejua kitu kinachoitwa kiwanda kinafananaje! Viwanda zaidi ya elfu nani angekosa ajira?

Ndugu Rais, kuna mahali kulikuwa mbali kama China? Leo wote Wachina na wasio Wachina kiguu na njia kuifuata gesi yetu. Si Wamarekani si Waingereza – wote wakija wanasaini mikataba juu ya gesi yetu. Mikataba yote ni siri. Siri anafichwa nani? Anafichwa mwenye mali, mwananchi mwenye gesi? Sijui itakuwaje hiyo siku atakayokuja kujua alichokuwa anafichwa!

Ndugu Rais, huko nyuma, baada ya miaka miwili kupita tangu awamu ya nne kuingia madarakani, Jenerali Ulimwengu alinukuliwa akisema tuweke utaratibu ili kuanzia sasa (wakati ule) kila anayetaka kugombea urais apimwe uwezo wake wa kuandika hata makala moja tu katika gazeti.

Shughuli anayoijua ni kuandika. Leo tunaposema maisha ni mahesabu yafaa tuwe na utaratibu wa kumdahili mgombea urais uwezo wake wa kumudu biashara hata kama ni kumiliki banda la kuku. Haiwezekani tuwe na utajiri unaowavutia watu wa mataifa yote duniani halafu viongozi wetu wapo wapo tu. Utajiri wa gesi ni mkubwa mno. Unatosha kuuondoa umasikini wa watu wetu lakini baadhi ya viongozi wetu akili wanayoifanya ni kujaza polisi barabarani kukusanya kodi kwa nguvu kwa wenye magari.

Ni sawa na nyumba imejaa mali halafu kutwa baba na mama wanatangatanga kwa majirani kuomba misaada watoto watibiwe au waende shule. Lazima tatizo litakuwa kwa wazazi kwa sababu ndiyo viongozi. Ndiyo kusema viongozi wetu hata kama siyo wote ndiyo chanzo cha umasikini wetu. 

Na ndiyo sababu ya umasikini wa wananchi. Na kwa sababu hiyo, waliokuja na kaulimbiu ya kutaka kuleta mabadiliko waliungwa mkono na wananchi wengi masikini. Hali hiyo bado ipo mpaka leo. Wananchi ambao ndiyo wapiga kura wataendelea kudai mabadiliko. Uchaguzi mkuu hauko mbali.

Tukiendelea hivihivi tujue kabisa kuwa tunabeep kutoka na tutatoka kweli.

Tunao waswahili wenzetu ambao wamefunguka kibiashara lakini viongozi wetu hawataki kuwatumia au kujifunza kutoka kwao. Wakati wa kampeni, Edward Lowassa alisema kama kuna Watanzania wenzetu ambao wamefanikiwa ‘kutoka’ kimaisha  kwanini hatuwatumii kama ‘modo’ (watu wa mfano) wetu? Alimtaja hadharani Regnald Mengi na wengine. Kijana wetu Mo Dewji ni mmoja kati ya matajiri wa bara hili. Sisi kama nchi tunautumiaje ubunifu wake ili kuikwamua nchi yetu na sisi wenyewe?

Yaonekana kitu ambacho baadhi ya viongozi wetu wanajua katika utajiri mkubwa tulionao wa gesi ni kuwasainisha mikataba watu wakuja bila kufahamu kuwa wanaubinafsisha utajiri wetu kwa wageni.

Ndugu Rais, habari inayoufunga mwaka huu ni hii ya ununuzi wa ndege mpya. Wanaodharau ununuzi wa ndege hizi unazonunua wapimwe akili. Ila na sisi kinachotupasa kujua ni kwamba kila hotuba ina watu wake na mahali pake. Kama watu wako msibani wamefiwa na baba yao usiwahutubie jinsi ulivyofanikisha upatikanaji wa madawati.

Kama unadhani ndege zako zitaweza kuumua uchumi wa nchi kawahutubie maprofesa wa uchumi kama ndugu Ngowi na wenzake wa elimu ya juu. Huko mtajadiliana kwa kuelewana mkitumia hoja zenu za kiuchumi. Lakini uchumi huu wa ndege tukienda kuwahutubia wazee wetu walioko katika kijiji nilichozaliwa, kwa mfano, watatushangaa sana. Hawana uhakika wa dawa katika zahanati yao. Hawana maji katika kijiji chao.

Hawana uhakika wa chakula wakati mwingine kwa ukame wakati mwingine kwa mazao yao kukopwa na serikali yao. Haohao unawaambia naomba kura zenu kwa maana nimewanunulia ndege. Wewe unabipu kutoka!

Wanaweza wasituambie tukapimwe akili lakini wakanong’onezana wao kwa wao maneno yenye maana ileile ya kututaka tukapimwe akili. Katika vijiji vingi vya nchi hii, mtoto anazaliwa, anakua mpaka anakufa kwa uzee hajawahi kuiona ndege ikiwa imesimama juu ya ardhini (ikiwa

imepaki).

Wanasikia milio tu juu mbinguni aliko Mungu ndege zikipita

kwenye mawingu. Tuache kujisifia ndege kwa watu wasiojua ndege. Kama ‘hatubipu’ kutoka tuwasikilize wapiga kura. Tuzitatue kero zao kabla hatujawarudia.