Ndugu Rais, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa mimi si mwanasiasa.

Sijawahi kujiunga na chama chochote cha kisiasa tangu kuzaliwa kwangu.

Na nitabaki hivi nilivyo. Nitaisema kweli kwa ajili ya amani ya nchi yangu na kwa ajili ya ustawi wa Watanzania wenzangu huku nikimwombea afya njema Rais wangu. Muumba wangu anijalie mwisho mkamilifu!

Siasa ni kazi njema. Lengo la chama chochote cha kisiasa ni kutawala.

Na ndiyo malengo ya wanasiasa. Kipaumbele cha kwanza cha kila mwanasiasa ni yeye mwenyewe na familia yake na wanaomzunguka, lakini siyo shida za wananchi. Ndiyo maana haishangazi kuona hata mgombea ubunge tu, yuko tayari hata kumpiga mshindani wake rungu la kichwa hadi kuzimia. Mroho anagombea maslahi binafsi.

Mavuvuzela wanaamini kuwa siasa ni uongo. Zamani walikuwapo walioamini kuwa hakuna mwanasiasa atakayeuona Ufalme wa Mbingu. Ndiyo maana ulipotolewa uamuzi wa kumuenzi Baba wa Taifa atangazwe kuwa mtakatifu imani za wengi zilitikisika. Ikiwa itatokea Julius Kambarage Nyerere akatangazwa kuwa mtakatifu atakuwa ni mwanasiasa wa kwanza mwandamizi wa nyakati zetu hizi kutangazwa kuwa mtakatifu. Hapo ndipo unaona ukaribu wa neno siasa na neno uovu na umbali wa neno siasa na neno wema.

Hivyo waliodhani kuwa hakuna mwanasiasa atakayeiona pepo wanaweza kuwa walikosea, lakini kwa kuwa Zitto alisema siasa ni mchezo mchafu hawa hawakukosea sana. Mimi siyo Paroko, lakini toka lini mchezo mchafu unaweza kumpeleka mtu mbinguni? Maandiko yanasema, “Katika mji ule hakuna chochote kinyonge (kichafu) kitakachoingia!’’

Ninachosema hapa ni kwamba kwa baadhi ya wanasiasa wakubwa walioko katika nchi zetu hizi hasa katika bara hili la Afrika, kuingia kwao mbinguni ni kugumu zaidi kuliko ngamia kupenya katika tundu la sindano. Mpaka Mungu mwenyewe apende kwa kuwa kwake hakuna lisilowezekana. Kwanini niwe mwanasiasa niiweke pepo yangu katika uvuli wa shaka? Muda wa maisha yetu hapa duniani ni mfupi sana. Sisi wote ni wapitaji tu. Nyumbani kwetu kwa kweli ni kule juu aliko Baba!

Wote wakiwamo wanasiasa wakubwa kwa wadogo, tujutie makosa yetu, tufanye kitubio ili tubadilike na kuwa watu wema! Kama kuna uovu tulimfanyia yeyote kati ya watu wake, tulimfanyia Yeye, asema Bwana!

Majina yetu yameandikwa na hukumu yetu iko palepale!

Tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, baba tuongoze katika njia ifaayo nasi hatutaiacha. Mapito yetu kuelekea mwaka 2020 yanafanana na yale ya wana wa Israel walipokuwa wakielekea Canaan. Mbele yetu kuna mto Jordan. Hatuna mwingine wa kutuvusha kwani baba tulienaye ni wewe Ndugu Rais peke yako. Tuvushe utufikishe mwaka 2020 kwa amani. Walipofika Canaan walikunywa divai na mvinyo wakasherehekea. Sisi 2020 uwe ni mwaka wa kufunguliwa kwa waliofungiwa nafsi zao. Mwaka wa kupona kwa wale waliouguza nafsi zao kwa muda mrefu.

Naiona nuru nyembamba mwaka 2020. Hakika viwete watapata mbio, viziwi watasikia na vipofu watauona mwanga. Muumba wangu ameniambia, “Nyamaza, usilie Ee, mwanangu, nimesikia kilio chako! Amani ya nchi yako itarudi. Nanyi mtakuwa tena ndugu kama zamani. Nami nitaitoa hofu iliyoijaza nchi yako ili mlio wangu mpate kuishi katika upendo wa kweli!’’

Mchungaji Lyimo aliposema pale Ikulu kuwa kwa kazi unayoifanya wananchi hawatachagua maneno, watachagua kazi, alisema vema kabisa.

Akaongeza kuwa kama kuna uwezekano waachie pumzi wazungumze. Huu ulikuwa ushauri wa busara kubwa. Ukiwaachia sasa wazungumze, watatuonyesha kona zote, mashimo yote na hata makorongo kama yapo katika njia yetu ya kuelekea Canaan mwaka 2020. Tutakuwa na muda wa kutosha kuyasawazisha. Alisema ninajua hawawezi kukushinda kwa maneno yao kwa kuwa utawashinda kwa kazi zako. Kuendelea kuwaziba pumzi ni kwa hasara yetu wenyewe.

Mwanamwema Katibu Mkuu Ndugu Bashiru Ally alisema neno jema, “Hatutakuwa na kitu cha kuhofia mwaka 2020. Kama tutakuwa tumejenga zahanati za kutosha, zenye madawa [dawa], vifaa tiba, madaktari na wauguzi walioshamiri wito na kuridhika, zinazoonekana kwa wananchi; na kama tutakuwa tumejenga shule zinazojitosheleza kwa madarasa, madawati, vitabu vilivyo bora, vifaa vya kufundishia na walimu wenye ari, tutahofia nini 2020? Wananchi wataona’’

Baba, hakuna timamu yeyote anayeweza kubeza jambo kubwa na jema kama ununuzi wa ndege. Tunachotakiwa kuelewa sisi tulionunua ndege ni kwamba, asilimia kubwa ya wananchi wetu walioko vijijini kule mashambani, kabisa kabisa hawajawahi kuiona ndege ikiwa imepaki juu ya ardhi. Wanaziona zikipita juu mawinguni kule wanakodhani ndiko anakoishi Mungu. Siyo kosa lao. Hatujawapatia elimu ya kuwawezesha kuelewa uhusiano uliopo kati yao walioko ardhini na ndege zipitazo juu yao bila kusimama. Tutakapowaendea mwaka 2020 na labda tutakuwa hatujawaendea tangu 2015 halafu tukawaambia tumewaletea maendeleo kwa kuwanunulia ndege, tutafanana na mwalimu anayewauliza wanafunzi wa darasa la pili maswali wanayopaswa kuulizwa wanafunzi wa kidato cha pili, watatushangaa.

Tunaweza tukajisikia vibaya tukadhani wanatupuuza kumbe maskini wa Mungu hawaelewi tunachowaambia.

Imetangazwa kuwa wanafunzi 133,747; sawa na asilimia 18.24 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana wamekosa nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali kwa mwaka 2019 kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Kama tunaona tulifaulu kuwafanya wananchi wasione yanayotokea bungeni kwa kulizima Bunge sasa tutambue kuwa tumefeli kuwazuia wananchi wasijue yanayotokea humo. Wanajua Wizara ya Elimu ilitumia mabilioni ya fedha kuchapisha vitabu vya shule ambavyo havikufaa. Zikatumika bilioni nyingine kuviteketeza. Wizara ya elimu ikatumia mabilioni mengine ikachapa vitabu vingine, navyo makosa ni yale yale vingine zaidi. Mabilioni mengine ya kuviteketeza na mengine ya kuchapa vingine.

Mwaka unaisha watoto shuleni hawana vitabu. Vitabu bora vilivyothibitishwa na wizara yenyewe vinajaa katika mabohari ya wachapishaji. Ni kuwaambia tu pelekeni vitabu shuleni.

Halafu mwaka 2020 tuwatokee wananchi maskini walioko mashambani wakiwa wanahuzunika wanapowaona watoto wao wamekalia mawe na kuandikia chini, tuwaambie tumewanunulia ndege. Tuwe wakweli, watatuelewa? Uhaba wa madarasa, madawati, vifaa vya kufundishia sasa ni janga la nchi nzima.

Lakini ni nani anajali? Haya mabilioni yanayofujwa hovyo na Wizara ya Elimu, baba, yasingeweza kutatua tatizo hili? Nani anawafanya wananchi wasiyathamini haya makubwa tunayoyafanya?