Ndugu Rais sitakusahau kwa ‘kiki’ (msemo wa vijana wakimaanisha kukwezwa) uliyonitunuku ukiwa waziri mwenye dhamana ya barabara.

Huku kwetu Mbagala-Kokoto wa zamani wanajua kuwa ni mimi niliyesababisha ujenzi wa barabara mbili kutoka Mbagala-Terminal zilipoishia hadi hapa kwetu Mbagala-Kokoto. Ukiwa msomaji mahiri wa makala zangu, uliposoma tu nilipoandika kuwa gari la mkaa limeiangukia Hiace yenye abiria baada ya kuingia katika shimo mojawapo kati ya mengi yaliyokuwapo Mbagala-Terminal, ulikuja hima ukiwa na mkandarasi.

Ulipomuuliza kwa nini barabara mbili amezimalizia Terminal badala ya Kongowe, alijibu kwamba fedha alizopewa hazikutosha na zilizobaki zingetosha tu kujenga kilomita moja. Kwa ujasiri mkubwa ukamuamuru: “Ukijenga hiyo kilomita moja haya mashimo yataondoka yenyewe. Anza kujenga hiyo kilomita moja sasa hivi.’’

Kwa utendaji wako mahiri, Kokoto tukapata barabara mbili. Kwa kunikweza mwanao kiwango hiki, baba asante na ubarikiwe sana! Nitakuwa mtiifu kwako, nami sitakuacha baba hata katika siku zako za furaha na kusherehekea au katika siku zako za huzuni na kujutia!

 Ben Kiko akiripoti kutoka Dodoma, kwa mshangao aliuliza: “Ah! Sijui vipi mkoa huu!’’ Hiyo ilikuwa ni baada ya kushuhudia wanyama wakali wa mwituni wakiwashambulia wakazi wa Dodoma kwa siku tatu mfululizo! Jana nyati kamjeruhi mtu, na leo fisi kamuuma mtu!

Ndivyo leo dunia inavyolishangaa Bunge la Dodoma. Juzi aibu ya CAG. Jana aibu ya Steven Masele. Leo aibu ya kinyama zaidi! Ah! Sijui vipi Bunge hili! Unganeni wanawema wa nchi hii ili ikimpendeza Muumba wenu awaondolee pepo mchafu!

Sugu ana deni kubwa kwa wananchi. Alisikika akisema kuna ‘mapoyoyo’. Awaambie wananchi, mapoyoyo maana yake nini? Sugu waambie wananchi mapoyoyo ni watu gani? CAG aliwafariji Watanzania aliposimama ngangari kuthibitisha udhaifu wa Bunge.

Akathibitisha kuwa wapo baadhi ya viongozi katika Awamu hii hii ya Tano ambao ni timamu, weledi, wenye utu. Na hawa ndio wengi. Kama kuna viongozi ambao bado wanatumikia vifungo vyao kwa sababu walimuunga mkono CAG katika ukweli wake huu, nina hakika Mwalimu Nyerere angetumia neno lake alilotuambia kuwa ni jema, kuwa ni kwa sababu ya ‘upumbavu’ walionao waliowahukumu.

‘Kalulete’, yaani mzua mambo ya ovyo, akazua la Steven Masele. Steven anagonganisha mihimili. Timamu wakajiuliza nchi hii ina mihimili legelege kiasi gani mpaka Steven aigonganishe, nayo ikakubali kugongana? Simfahamu Steven Masele lakini ni ukweli kwamba Naibu Spika ni Spika.

Huyu yuko juu ya maspika wote linapokuja Bunge la Afrika. Watanzania wanapaswa kujivunia kuwa na vifaa mahiri, vinavyofaa kwa uspika ujao wa Bunge letu, vinavyotumika nje hata kama wao hapa ndani wanatumia vifaa dhalili vya kuokoteza. Vifaa vilivyopatikana kwa  marungu na magongo, baada ya kuishiwa hoja za kichwani!

Kiongozi anayeheshimu utu wa watu wengine hawezi kufikia uamuzi wa utata. Muhimili wa Mahakama umejaa viongozi wengi weledi, washika dini, wanaozingatia sheria wanapotoa haki. Wamekiri kuwa mgonjwa yupo hospitalini. Anayewaambia wananchi kuwa hajui mgonjwa aliko, tuseme nini kuhusu yeye?

Kwa kukosa maarifa anawakusanyia wagonjwa umaarufu na huruma ya wananchi hata wasio na vyama. Kwa akili yao kubwa itakuwa rahisi kuwashawishi wawachague wawe ndio viongozi wao wajao! Tangu tunakua tunasikia: “Ukimtuma mjinga umejituma mwenyewe”, lakini Biblia Takatifu imeandikwa: “Amtumaye mpumbavu, hujikata miguu na kunywa hasara!’’ Kama katumwa aliyemtuma ajue kuwa amejikata miguu na sasa anakunywa hasara!

Viongozi wanaoona ni muujiza nchi yetu kufikia AFCON ni wachanga, tuwapende. Lakini wasiuchukulie ujana wao kuwa sababu ya kukosa busara. Na walio juu yao waelewe kuwa hawa vijana hawawajengi bali wanawabomoa! Tulipofikia huko kabla, baadhi yao walikuwa hawajazaliwa. Badala ya kujiongeza, wao wanaonyesha ushamba walionao! Wakiwaambia Taifa Stars sasa ni mali ya serikali, msiibishie serikali, kwa sababu mkiitwa wachochezi…yajayo hayajulikani! Imekosekana elimu ya uraia. Hawajui nchi ni nini, taifa ni nini au serikali ni nini.

Mpira wa miguu una matatu. Kupigwa, kushinda na kile watu wa Kongo (DRC) wanaita, kutoshana nguvu, yaani sare. Anayekupongeza kwa timu kushinda sawa, na anayekuomba samahani kwa timu kushindwa huyo ndiye mkosi wenyewe. Watasemaje watashinda kama CCM, wakati polisi wamewaacha nyumbani? Mungu naye bwana. Tangu hapo zikawa zinapigwa tatu, tatu tu.

Maneno ya hovyo hovyo hayawezi kuitwa siasa, Fatma Karume kakataa! Tugoli tuwili baba, tunauma kuliko magoli sita. Mambo makubwa yatakayoifanya awamu ya tano ikumbukwe na vizazi vingi vijavyo ni kuchimba korongo kubwa linalowagawa wananchi.

AFCON imewagawa Watanzania. Mwenyezi Mungu atujalie tusiione tena AFCON nyingine mpaka mkosi huu utakapokuwa umepita! Timu siyo mbovu. Nuksi! Mbona tuliwapiga kwao goli moja bila na Edward Waziri Mkuu akawatangazia wananchi kutokea bungeni kuwa goli lile liliwaunganisha Watanzania wote? Ushindi huanzia kwa uongozi!

Kitabu cha ‘The People’s Schoolmaster’ au Kiswahili chake ‘Mwalimu Mkuu wa Watu’, kimeandikwa: “Tatizo la madaraka makubwa yakiambatana na mali nyingi mikononi mwa watu walio wengi, hasa wasio na busara, huzaa kiburi. Wanaamini kwamba magereza, bunduki na mabomu vinaweza kuzima nguvu za wananchi, hivyo kuwafanya watawale milele.

Ngome iliyo imara ya rais ni kuepuka kuchukiwa na wananchi, kuacha ubinafsi, na kujali masilahi ya wengi. Vyombo vya dola vikiegemea upande wa chama tawala, ajue kuwa vinasaidia kujenga chuki na uhasama miongoni mwa wananchi na kwake rais mwenyewe!’’

Kukubali kuitwa mfalme mbele ya wananchi wako ni uchuro! Katika demokrasia ya kweli mwenye moyo wa kutamani ufalme hachaguliki. Timamu hawachagui mtu awe mfalme wao! Lini alimwita mzazi wake mfalme, kama si kutaka watu wahisi anang’ong’wa mtu?

Ah! Kenyatta baba, umefika mpaka Kilimani, Chato? Ulikumbuka kumwambia baba yetu, mliyamalizaje na Raila Odinga? Leo mnaiongoza Kenya kama watoto wa baba mmoja! Wakenya wanastawi na nchi yao. Baadhi ya viongozi wetu kazi kuparurana tu.