Ndugu Rais, abarikiwe sana mwanamwema yule aliyenifanya niione nchi ya ahadi, Israel. Mungu ni mwema naye ana maajabu yake. Kwa miguu yangu isiyostahili nilikipanda kilima nikiifuata njia ile ile ya msalaba aliyoipita Bwana Yesu kituo kwa kituo.

Yesu alibeba msalaba. Mimi sikubeba msalaba. Kama nilibeba msalaba, basi zilikuwa ni dhambi zangu ambazo nimetenda labda hata kwa kutokujua bali kwa udhaifu wangu wa kibinadamu ambao wote tumeumbwa nao. Baba usitufikishe Golgota. Yesu alifia Golgota, lakini alifufuka. Ukitufikisha Golgota sisi hatutafufuka!

Malumbano yanayoendelea hivi sasa katika nchi yetu yana kila viashiria kuwa tunaelekea Golgota. Naukumbuka vizuri sasa wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliposema, “Paolo, Paolo, Paolo, na nyinyi wengine, mkilifuta kabisa kabisa Azimio la Arusha, mtakuja kupata taabu sana baadaye!’’ Baadaye yetu ndiyo hii. Sasa tunashambuliana na kuuana kama wanyama wa porini! Fahamu zetu zimetutoka zimekwenda kwa wanyama. Tunakwenda wapi? Mbele yetu ni ipi?

Wanawema bila Azimio la Arusha au jukwaa, Mwalimu Forum-MWAFO wanaotuambia kuwa tunapuyanga watakuja kuonekana kuwa walikuwa wanasema kweli.

Tukubali, labda Bunge lilipokubali kuzimwa ulikuwa ni uthibitisho wa udhaifu wa Bunge. Kama tulidhani kwa kufanya hivyo wananchi hawatajua kinachoendelea ndani ya Bunge lao, pia yawezekana hatukufikiri sawa sawa. Sasa mengi yanaonekana yanapelekwapelekwa tu na kwa unafiki mkubwa wanasema funika kombe mwanaharamu apite! Kila muswada unapelekwa na kila muswada unapitishwa. Lakini Mwenyezi Mungu ana maajabu yake.

Adhabu zake nyingine huwaadhibu watu wake wakiwa hapa hapa duniani.

Waziri aliyesimama kidete kuhakikisha wananchi hawataona yanayofanywa na waliowatuma ndani ya Bunge lao leo ndiye anaonekana ni muathirika mkubwa wa uamuzi ule. Kuendelea kutembea mbele za watu kunamhitaji mtu kuwa na roho ngumu au unafiki mkubwa. Lengo kama lilikuwa ni kuwafanya watu wetu wasisikie au wasione yanayofanyika ndani ya ukumbi wa Bunge lao, basi hatujafanikiwa kabisa. Ni katika mkutano wa Bunge uliopita tu wananchi wamesikia kauli nzito ikisema, “atakapotumaliza sisi atawageukia nyinyi.” Laiti Bunge lingekuwa ‘live’ na huru Watanzania wangefafanuliwa maana ya maneno kama haya. Lakini watu wa Mungu wanajiuliza, haya yataendelea mpaka lini? Tukumbuke, haya yana mwisho!

Ndugu Rais, labda ilikuwa ni sawa kutomtumbua yule mama waziri aliyetunga kanuni-sumu ya vikokotoo. Kama ungemtumbua nina hakika wale wengine wangesema ingelikuwa haki zaidi kama tungejitumbua wenyewe.

Wananchi wanaambiwa baada ya mama waziri kutunga kanuni-sumu na vikokotoo vyake, alizipeleka katika Baraza la Mawaziri. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri siku hiyo sijui alikuwa nani, lakini alizipitisha.

Kama ilivyo kawaida muswada ulipelekwa bungeni. Yawezekana hii nayo ikawa ni sababu mojawapo ya wengine kuliona Bunge kuwa ni dhaifu kwa kuwa liliupitisha. Muswada ulirudi serikalini ili usainiwe na Rais ili uwe sheria. Kama ulisainiwa au la pia sijui, lakini kelele zake nani hakuzisikia?

Walipotengua walichokitega wenyewe, vuvuzela wakaipuuza ile marufuku njema inayowakataza wananchi kuandamana, wakaandamana. Wananchi wanasubiri wenye marufuku yao waseme chochote.

Unapotokea ukimya kama hivi tunawajengea mazingira mazuri wanaosema tunapuyanga kusikilizwa na wananchi! Bahati mbaya ni kwamba hawa wakisikilizwa sisi tutapuuzwa!

Nguvu kubwa sana imetumika katika kukusanya kodi. Ili walipe kodi inayotosheleza ni lazima wafanye biashara inayotosheleza. Unapowawekea mazingira magumu wafanyabiashara itashangaza kutarajia kukusanya kodi inayotosheleza. Wananchi waliishazoeshwa kuambiwa kuwa walipakodi wakubwa ni watengenezaji wa pombe. Lakini katika saa ishirini na nne za siku unapowapangia saa saba tu za kufanya biashara unatarajia upate kodi kiasi gani? Siku utakapobadili kwa kuziongeza utawazuiaje watu kusema tunapuyanga. Kwetu tunasema, ‘yamleka zipita nga masala yawazana’ yaani kuna watu hawapati akili mpaka mambo yaharibike.

Tunahitaji muda wa kutosha na fikra sahihi tunapopanga mambo tunayodhani yatatusogeza mbele. Tukumbuke tulikoanzia. Madawati na vyumba vya madarasa halikuwa suala la mchezo hata kidogo. Leo ni nani anaweza kutuonyesha wilaya au mkoa ambao hili siyo donda ndugu? Je, zile kelele madawati, madawati ilikuwa ni nguvu ya soda? Mpaka kufika mwisho tutajikuta tumerudi kule kule tulikotoka kwenye bahari ya upungufu. Kama huku siyo kupuyanga basi waambiwe ni kufanyaje?

Tunayapokea kwa masikitiko makubwa mambo ya kigaidi wanayofanyiwa ndugu zetu wananchi wa Kenya. Watu wengi wameuawa na watu wengi zaidi wanaachwa na vilema vya maisha. Kila aliye mwema analaani unyama huu kwa nguvu zote. Hata hivyo inawaletea faraja kubwa wananchi wa Kenya kuona kuwa kila janga linapotokea serikali yao pamoja na Rais wao Uhuru Kenyatta wanalia pamoja! Viongozi wao wanawaambia wananchi wao kuwa wanawajua maadui hao. Na mara kadhaa wamewaua. Wananchi wanafarijika kuona kuwa viongozi wao pamoja na serikali yao wanawapigania, hivyo iko siku amani yao ya kudumu itapatikana.

Haijajulikana wazi kama kuna ugaidi unafanyika katika nchi yetu. Lakini tofauti na Kenya hapa kwetu kila janga linapotokea kama watu kutekwa, watu kuteswa, watu kushambuliwa kwa risasi au watu kupotea na hata watu kuuawa kila aliyepatwa na mkasa wa aina hiyo, hulia na wa kwao. Ukaribu wa serikali hauonekani. Na katika mara karibu zote jitihada za serikali kukomesha unyama huu hazionekani kwa macho matupu. Ni nani aliwahi kusikika hata akiwakemea tu watu wasiojulikana? Zinapita siku au hata miezi na wakati mwingine miaka inapita, juhudi za serikali hazionekani. Wananchi hutumbukiwa nyongo pale serikali na vyombo vyake vinapokiri hadharani kuwa wahalifu wanaoendesha vitendo hivyo vya kinyama, serikali haiwajui. Lakini inajua kuwa ni watu wasiojulikana. Kama awamu ya tano haitachukua jitihada za makusudi kujisafisha katika hili haitashangaza huko tunakokwenda awamu hii inaweza kuja kujikuta imejipatia jina la ubatizo la “watu wasiojulikana”. Hili ni doa kubwa na kulisafisha ni lazima kazi kubwa ifanyike.

Tunafanya au tutafanya mambo mengi mema na makubwa, lakini kwa ukubwa wa hili doa linaweza kuyafunika yote na tukaonekana tulikuwa tunafanya ubatili mtupu!

Ndugu Rais, mlolongo wa haya yote ni viashiria tosha kuwa njia tuliyoichukua inaelekea Golgota. Hakuna wa kututoa katika njia hii ya kutisha, bali ni wewe baba peke yako!  Baba, tuepushe tusifike Golgota!