Ndugu Rais, tumwombe Mwenyezi Mungu atufundishe kunyamaza kwa sababu katika kunyamaza kuna kutafakari ili tusije tukamuudhi Muumba wetu katika kujibu.
Hakuna hata mmoja kati yetu aliyeomba azaliwe katika nchi hii. Tumekutana hapa kwa mapenzi ya Mungu mwenyewe tu. Hivyo, hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine katika nchi hii. Nchi hii na vyote vilivyomo ni kwa ajili ya sisi wote katika ujumla wetu. Kusigana kumeumbwa, hatuwezi kuukwepa lakini utu wa mtu unakamilika unapowasikiliza wengine.
Ndugu Rais, yanayoendelea katika Bunge letu yanatia aibu kwao wote. Tunasikia sasa hawasalimiani tena. Ni ujinga kusema ni utoto. Mtoto gani anakuwa mbunge! Kiongozi kama umesusiwa na wengi busara siyo kukomaa.
Kuwa ngangari ni kupungukiwa hekima. Waite mkae nao mjadiliane, lengo likiwa ni kufikia maridhiano. Kuendelea kukauka kama mti mkavu kunaweza kuwapa wananchi ushahidi usioacha shaka wanaoweza kulazimika kukuwekwa katika kundi mojawapo kati ya yale mawili – ama katika kundi la walevi aliosema Spika Job Ndugai, au katika kundi la wapumbavu aliosema Mwalimu Nyerere.
Upuuzi unaofanyika bungeni ndugu Rais unauangalia kwa macho matupu. Ili usije ukasema vijana wako wanaokupenda hatukukwambia, tunakwambia sasa kuwa ujinga unaofanyika bungeni hivi sasa utakapoipasua nchi, dunia itasema Rais Magufuli ameipasua Tanzania kwa sababu ndiye aliyekuwa Rais wake.
Ndugu Rais, tuukubali ukweli kuwa ujio wa vyama vingi umetuongezea mfarakano katika jamii yetu. Tuliishi katika amani na upendo zaidi wakati wa chama kimoja lakini sasa tunaishi katika uhasama na mashaka zaidi.
Ukabila na udini vimeangamiza watu wengi katika nchi nyingi lakini kwa kumtumia mtumishi wake, Julius Kambarage Nyerere, hapa kwetu Mwenyezi Mungu alituepushia. Sasa wahuni wachache wanataka kutupeleka huko. Tusiwakubalie.
Vyama vya siasa vimetuletea ukabila mpya ambao ni Chama Cha Mapinduzi dhidi ya upinzani. Vimetuletea udini mpya ambao ni Upinzani dhidi ya Chama Cha Mapinduzi. Wananchi wamegawanywa kwa misingi ya vyama vyao.
Hawana wa kuwatetea kwa maana viongozi wao wote ni mali ya vyama vyao. Wanapotetea wanatetea maslahi ya vyama vyao siyo maslahi ya nchi yao wala wananchi wao. Mkosi unakuja pale wale wa Chama Cha Mapinduzi wanapong’ang’ania kubaki madarakani huku wale wa Upinzani waking’ang’ana kuingia madarakani.
Wanadhani wanafanya siasa kumbe wanafanya upuuzi kwa sababu ujenzi wa nchi sasa umesimama.
Ndugu Rais, Awamu ya Kwanza ilitujengea upendo, umoja na mshikamano; Awamu ya Nne ilikuja kuyafuta yote. Kazi kubwa iliyofanywa tena kwa nguvu kubwa na Awamu ya Nne, huku wakitumia fedha za nchi, ilikuwa ni kupandikiza chuki katika nchi.
Na kwa hili, Awamu ya Nne itakumbukwa na vizazi vingi vijavyo. Jenerali Ulimwengu aliposema Jakaya Mrisho Kikwete afikishwe mahakamani alishangiliwa na ukumbi mzima.
Ile ndiyo iliyoonesha ukubwa na uzito wa chuki waliyonayo wananchi katika vifua vyao. Adhabu kubwa anayoweza kuipata Rais ni kuchukiwa na wananchi wake. Wayakubali matokeo kwa kuwa wanavuna walichopanda wenyewe kwa mikono yao.
Walisema mwisho wa ubaya ni aibu. Lilitokea kundi mfano wa panyarodi likasema linapigana vita dhidi ya ufisadi, leo wao ndiyo wanaotawala vichwa vya habari kwa ufisadi wao wa kitapeli.
Wengine wakajifanya mbwa mwitu,wakasema mwanadamu ana gamba lazima avuliwe. Yote hii ni kutaka Watanzania wachukiane. Sasa mwosha huoshwa.
Ndugu Rais, Taifa siyo moja tena. Watu wake wamegawanywa katika vipande vipande. Nchi inahitaji kiongozi wa kutuweka katika meza ya maridhiano. Wananchi hawana mahali panapowaleta pamoja. Wamekosa sehemu au jukwaa wanapoweza kukutana wakajadili mustakabali wa nchi yao bila kuingiza itikadi zao za kisiasa, kidini, kikanda au kikabila.
Ni jukumu lako baba kama mkuu wa nchi kuwajengea jukwaa hilo watu wako sasa. Wanaopigana sehemu nyingine za dunia hawakuzaliwa wanapigana.
Wabarikiwe wanawema waliolipokea Jukwaa la Mwalimu au MWAFO, wakajitolea kwa hiari yao kuwatengenezea Watanzania mahali watakapoweza kuurudisha undugu wao uliovurugwa na hawa wapanda sumu.
Walianza akina Mbarak, Juvenalis, Ndemfoo, Namelock, Mahmood, Gora na wengine. Nakutajia hawa wachache ili ndugu Rais ujue kuwa katika nchi hii wako wanawema ambao linapokuja suala la ‘nchi yangu kwanza’ hawatafuti kazi ya mshahara. Baba, watengenezee jukwaa hili ili uwape masikini wa nchi hii sauti ambayo baadhi ya viongozi wao manyang’au, wezi na walaghai wanaiogopa sana. Baba, anzia hapa.
“Mwalimu Forum au kwa kifupi MWAFO, ni jukwaa lililodhamiria kutoa elimu ya uraia kwa wanajukwaa na jamii kwa ujumla, kwa lengo la kuamsha ari ya uzalendo na mapenzi ya mtu kwa mtu, na mtu kwa nchi yake. MWAFO inalenga kuwapa Watanzania jukwaa watakapopata fursa ya kuzungumza na kujadili mambo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii bila kuingiza itikadi zao za kisiasa, kidini, kikabila au ubaguzi wa aina nyingine yoyote.”
Kama itakupendeza baba, mtumishi wako nisiyestahili niko tayari kukutumia maelezo ya kina.
Ndugu Rais, kazi ya kutumbua majipu ni kazi njema sana na imewafanya masikini wengi wakupende. Lakini nchi haiwezi kujengwa kwa kutumbua majipu peke yake. Nchi inajengwa kwa kuiwekea utaratibu madhubuti ambao unaifanya isitawi kwa kuwa majipu hayaoti tena.
Kelele za kutumbua majipu zilizokuwa zinaitikisa anga ya nchi yetu zinazidi kuyeyuka kama mshumaa uwakao unavyoyeyuka. Tunakuombea zisizimike kabisa kama zilivyozimika kelele za ufagio wa chuma aliokabidhiwa mzee Mwinyi, maana kitakachofuata kinaweza kuwa ni majanga makubwa.
Lakini baba, kumbuka kauli yako ulipowaahidi wananchi kuwa, “Watu waliofanya madudu katika utawala uliopita…hawatachomoka kwa kuwa nimejipanga kuwashughulikia wote bila kujali uwezo wao wala vyeo vyao. Nawaomba Watanzania muendelee kuniombea.”
Kauli hii iliwajaza masikini na wanyonge wa nchi hii matumaini makubwa sana. Wananchi walichokuwa wanataka ni mabadiliko. Kama kutumbua majipu ili kuleta mabadiliko hayo kunakuwa kugumu, ndugu Rais tengua kauli yako.
Najua wataaminika wale waliosema msitu ni uleule na nyani ni walewale, mabadiliko yatatoka wapi? Tunawatukuza waliosema nchi inapita katika mhemko wa muda kwani sasa wataonekana ni wenye busara na hekima kubwa.