Ndugu Rais, tafuteni kwanza ufalme wa mbingu, ya dunia mtayapata kwa
ziada! Tangu kutangazwa kwa Septemba mosi, nchi imekuwa ni ya mijadala isiyokwisha huku wapofu wakionesha nguvu zao. Mnagombania kuwatawala waja wa Mwenyezi Mungu kwa kudhani mnaweza kwa nguvu zenu!
Kati yenu nani ambaye kwa jitihada zake mwenyewe anaweza kuongeza hata unywele wake mmoja? Tamaa ya kutawala imewatia upofu!
Ndugu Rais, Septemba mosi iwe isiwe lazima itafika kwa sababu ni tarehe kama tarehe nyingine! Tarehe si kama miaka, zinazunguka. Kinachotisha na kuhofiwa na wengi ni je, itafika na ujumbe gani? Kuwahamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi katika maandamano na mikutano hiyo si jukumu langu; kama ambavyo si jukumu langu kuwahamasisha wananchi wasiandamane na kuhudhuria kwa wingi katika mikutano hiyo.
Jukumu langu ni kuwahamasisha wananchi kutambua kuwa amani ya kweli inakuwapo pale tu viongozi wanapoiheshimu na kuilinda Katiba ya nchi. Katiba inapovunjwa na yeyote, wawe tayari kuitetea amani ya nchi yetu kwa nguvu zao zote; iwe ni kwa maandamano ya amani au mikutano iliyoruhusiwa na Katiba na sheria za nchi!
Wakati wa uhai wake, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akihutubia kule Mbeya, hakuwaambia Watanzania kuwa iwapo watakuja kutokea viongozi wanyang’anyi wa haki zao walizopewa na Katiba ya nchi, wafanye nini. Kwa kuwa hakuwaambia wafanye nini, siwezi kumsemea leo.
Ninachojua ambacho najua na Mwenyezi Mungu anajua angewaambia msikubali kunyang’anywa haki yenu. Angewaambia wakatae kunyang’anywa haki zao! Iwe ni kwa maandamano ya amani au mikutano halali.
Lakini kwa viongozi aliweka msisitizo mkubwa! Aliirudia sentensi yake mara tatu akisema: “Viongozi, hamna haki ya kunyang’anya haki za raia!
Waziri, hamna haki ya kunyang’anya haki za raia! Ndugu waziri, hamna haki ya kunyang’anya haki za raia!”
Uongozi ni karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu, unahitaji busara na hekima na kamwe siyo nguvu! Hakuna kiongozi yeyote katika kumbukumbuku za ulimwengu huu aliyetawala kwa kunyang’anya haki za raia wake aliyeishia salama! Yawezekana baba hukumsikia Rais Nyerere wakati ule.
Alichosema ni kwamba, huna haki ya kunyang’anya haki za raia!
Ndugu Rais, jihadhari na matapeli waliokengeuka na sasa wanataka kuzichafua dini zao. Waislamu wasujudu misikitini. Wakristu wasujudu makanisani. Waliotoka nje wakijifanya ni viongozi wa dini huku wakifanyia ‘mishemishe’ zao kwenye mbawa za wanasiasa waogope kama ukoma! Watajitambulisha kwa majina ya kujitafutia ulaji. Wengine watajiita kamati ya maridhiano na wengine kamati ya amani.
Kama hawa wangekuwa ni watumishi wa kweli wa Mwenyezi Mungu wasingekuacha baba peke yako, ufike hapa ulipofika panapotishia ustawi wako! Wangekuwa sambamba na wewe kwa ushauri kama sisi mawe tulivyosambamba na wewe kuhakikisha baba unabaki katika kweli.
Wakikuambia ukae na wapinzani mjadiliane ili mfikie mwafaka, ukiwaona ni wapuuzi halafu ukawapuuza nakuhakikishia, hakuna timamu atakayekupuuza! Baba mwenye busara anaposuluhisha tofauti za wanae, atamwita kwanza mwanaye mkubwa aeleze wanagombea nini na mdogo wake.
Kwa baba mwenye busara aliyewalea watoto wake katika njia ifaayo kama Baba wa Taifa alivyowalea Watanzania, maelezo ya mtoto wake mkubwa yanatosha kumfanya atoe uamuzi wa busara utakaoridhisha pande zote mbili bila kukaa na kujadiliana na watoto wake.
Kiimani wewe ni muumini wa kanisa. Makatekista, mapadri na maaskofu ndiyo viongozi wako. Kama wanaona umetoa amri iliyolikwaza Taifa wanashindwa nini kukuita madhabahuni ili mjadili vipengele vya Katiba ambavyo waumini wengine wanasema umevunja Katiba ya nchi? Ikionekana hujavunja Katiba, wawakemee wanaowachanganya wananchi wakisema umevunja Katiba na kwamba Kanisa la Mungu halina nafasi kwa watu wanaotaka kuleta fujo au uhuni! Ikionekana umevunja Katiba wakuamuru urekebishe hali hiyo mara moja. Usipowatii historia ya kanisa iko wazi.
Walikuwako wafalme waliokuwa na nguvu za kupindukia nao walitengwa na kanisa na mwisho wao unakumbukwa kwa uchungu hadi leo!
Ndugu Rais, tunapoelekea Septemba mosi, neno uchochezi ndilo linatawala nchini! Yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu, yaliandikwa zaidi ya miaka 10 iliyopita. Neno uchochezi lilileta maangamizi makubwa katika nchi ambayo leo neno hilo hilo linaielekeza nchi katika mdomo wa mamba! Timamu wanasema uchochezi na wapumbavu nao wanasema uchochezi! Wachovu kwa ujinga wao wamelifanya neno uchochezi ndiyo ngao na sababu ya kuwatesea watu wa Mungu! Madhara ya neno uchochezi tunayasoma ukurasa wa nane. Baba soma kitabu hiki ili ukubalike!
Imeandikwa: “Maandamano yalijumuisha watoto, vijana, wazee, akina mama na hata vilema na ulemavu wao. Waliendelea mbele na kukata kushoto…Hapo ndipo… Lahaula! Walikutana na askari wa kutuliza ghasia waliojisheheneza silaha nzito nzito. Basi, bila onyo wala hadhari yoyote, na kwa nguvu kubwa ajabu, askari wale wa kutuliza ghasia walianza kutuliza ghasia ambayo kwa kweli haikuwapo!
Walifyatua risasi za moto, walifyatua risasi za mpira, wakafyatua na mabomu ya machozi. Walitumia virungu na silaha nyingine nyingi dhidi ya ule umati. Kwa kufanya hivyo, askari wa kutuliza ghasia wakawa wameanzisha ghasia kubwa!
Ilikuwa tafrani kubwa. Patashika nguo kuchanika. Traa…traa..bunduki zilifyatuliwa ovyo! Walioyapoteza maisha yao, waliyapoteza!
Waliojeruhiwa walijeruhiwa! Watu walikimbia ovyo kusalimisha maisha yao! Umati ulitawanyika huku na huko, nao moshi wa risasi ukazagaa ovyo hewani.
Patashika yake ilikuwa kubwa na matokeo yake yalimtoa machozi kila aliyeyakumbuka baadaye! Aliyesimuliwa alishindwa kuelewa ni kwa kiasi gani binadamu anaweza kuwa mkatili kwa binadamu mwenzake!
Askari wa kutuliza ghasia walianzisha ghasia ambazo mwisho wake ulikuwa ni vifo, majeruhi, mateso na vilio vya wale waliokuwa wakizitoa roho zao!”
Nasema ole wao watakaotufikisha huko! Ingelikuwa ni bora kwao kama wangeutafuta kwanza ufalme wa mbingu!