Ndugu Rais, maandiko yanasema watu walikuwa wanasafiri katika chombo baharini. Chombo kilisheheni mizigo mingi, lakini kilienda bila tatizo.

Kilipofika katikati ya bahari chombo kikaonekana kulemewa na mizigo.

Kikaanza kuzama. Abiria wakapatwa na mfadhaiko wakaamua kuitupa mizigo baharini, lakini chombo kiliendea kuzama. Nao walipokwisha kata tamaa wakisubiri kuzama pamoja na chombo, walijikusanya pamoja, wakaulizana, “Jamani ni nani kati yetu mwenye shida hii?’’ Ndipo akasimama Yona akasema, “Jamani nitupeni mimi!’’ Wakambeba Yona wakamtupa baharini.

Amani katika chombo ikarejea safari ikaendelea, lakini baada ya gharama kubwa.

Kumbe Yona alizamia kile chombo ili kukwepa amri ya Mungu iliyomtaka aende Dimani kutangaza neno lake. ‘Uswahili’ ulianza zamani hata kudhani unaweza kumdanganya Mungu. Kudhani unaweza kumtanguliza Mungu mbele wewe ukabaki nyuma unafanya vitu vyako unajidanganya mwenyewe. Mungu ni Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi. Huwezi kumtanguliza mbele!

Kumtanguliza Mungu mbele ni maneno yanayokiri udhaifu wetu kama wanadamu tunapotaka kutafuta huruma ya wengine. Wanaodhani wana uwezo wa kumtanguliza Mungu mbele wasome maandiko katika vitabu vitakatifu imeandikwa, “Naye mtamwita Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi.’’

Wanawema tukubali Tanzania ya leo siyo ile tuliyokulia. Jamani hivi sasa dunia imetusema mno. Tumechambuliwa kama karanga. Ingekuwa maneno yanababua hivi sasa tungekuwa hatuna ngozi.

Kusemwa kwa mema au kwa mabaya yetu ndiyo dunia. Watanzania kama wananchi wa nchi nyingine zote tunazo hisia zetu tofauti tofauti. Wapo wale ambao kwa sababu zao

binafsi wanaiona hali hii ni kawaida tu. Wako wale ambao mioyo yao inawatetema kwa hofu kama utete dhaifu unaosukwasukwa na maji ya mkondo kwa kuhofia yajayo. Lakini pia wapo ambao nafsi zao zinawanyonga vifuani mwao, lakini wafanyeje maji yamekwisha mwagika?

Hawa hawatakujaipata furaha ya kweli katika mioyo yao hapa duniani mpaka siku zao za mwisho. Kinachotakiwa sasa siyo kuendelea kutongoana vidole machoni, bali uvumilivu ndilo neno kuu. Kama ni haki hapa ni haki sawa kwa wote.

Kuna baadhi ya watu wamezuka ghafla ambao au wana uelewa mdogo wa lugha ya Kiswahili au wanatumia maneno mema ya Kiswahili kutaka

kupotosha wale wanaowadhania kuwa wanapotosheka kwa maslahi ya matumbo yao. Maneno kama kosoa, shauri, chochea, kemea na ubeberu hayajawahi kuwa kati ya maneno ya kuleta mafarakano katika nchi yetu tangu zamani.

Kwa sababu zao wameyatengenezea maana bandia ili kuwagawanya Watanzania.

Kamusi kuu ya Kiswahili inatafsri neno ‘kosoa’ kama eleza makosa ya mtu baada ya kumsikiliza, kusoma maandishi yake kuyachunguza matendo yake. Kumchambua mtu kuna una ubaya gani mpaka lilete gharika katika nchi.

Ushauri ni kutoa mawaidha nasihi, elekeza, usia au ongoza. Lipi baya katika hili? Sina uhakika na wanaotumia neno uchochezi. Wakati mwingine unaweza ukadhani unamtetea mtu kumbe ndiyo kwanza unamthibitisha kwa uchochezi. Unachochea kile kilichokwisha washwa.

Kamusi Kuu ya Kiswahili inatafsiri kuwa, mchochezi ni mtu mwenye tabia ya kukandamiza wenzie. Mwanaume anayetumia mabavu kufanya jambo.

Neno mabeberu lilivumishwa sana wakati wa Tanganyika. Rais Nyerere kabla hajawa Baba wa Taifa alilitumia sana. Baada ya kuwa Baba wa

Taifa, Julius Nyerere hakuliabudu tena neno beberu mpaka umauti ulipomkuta. Mavuvuzela sasa kwa ufahamu wao mdogo neno hili ni jipya wanadhani wameligundua. Mufilisi hawa hawajui kuwa wanakula makapi na kuwatenganisha Watanzania.

Bahati mbaya wanaoyaonea ufahari ni vijana ambao badala ya wao kuwa nguvu mpya ya taifa katika kuijenga nchi yao iwe na mshikamano, wamekuwa watumwa wa wanasiasa wazee wakitegemea kushibishwa na makombo wanayo watupia. Na kwa sababu hawaijui siasa nini wanachofanya ni kuleta mafarakano katika nchi. Waliopaswa kuwadhibiti na kuwaelekeza katika njia ifaayo wanaonekana nao ni wale wale. Kinachosumbua ni uroho wa madaraka wa baadhi ya viongozi wetu. Kwa wasiomkiri Mwenyezi Mungu madaraka ni matamu, madaraka ni ufalme.

Wameingia madarakani wakiwa na makaratasi lukuki wenyewe wakiyaita vyeti. Huyu ana vyeti vinavyomwonyesha kuwa anaweza hata kutengeneza injini ya ndege ikiharibika. Mwingine cheti chake kinaonyesha kwa anaweza kupasua moyo wa mtu na akaufunga tena. Haya yote hayana maana yoyote ya kumfanya mtu awe kiongozi bora wa watu. Nchi inaongozwa kwa busara na si kwa makaratasi.

Julius Kambarage Nyerere kabla hajawa Baba wa Taifa alijikita sana kusoma historia. Historia ni kama nahodha wa jahazi. Anaendesha ya mbele akiwa amekaa nyuma. Ya nyuma ndiyo yanakupa dira uelekee wapi.

Nimemtafiti kwa miaka mingi Julius Nyerere. Nikagundua kuwa pamoja na elimu nyingi kubwa mbalimbali alizofuzu Nyerere, lakini alikuwa mbobezi katika historia. Julius Nyerere alifanikiwa sana katika kuongoza nchi kwa sababu alichokuwa anafanya ni kile wanaita kukopi na kupesti.

Alikuwa anakopi na kupesti tawala za zamani za Afrika Magharibi kama zile za Oyo Empire na zingine. Wanawema wanaotaka kuwa viongozi wetu mwaka 2020 wasome kwanza tawala zile za Afrika Magharibi. Mtamkuta Mfalme aliyepachikwa jina la, ‘Impartial Judge’. Alipendwa na wananchi wake wote kwa kuwa hakuna alichowafanyia cha kuwaudhi. Si kwamba kila alichofanya kiliwapendeza wananchi, bali alikuwa na mtu wake aliyemtumia kufanya yale ambayo alijua yatawachukiza wananchi. Ndipo mtajua kwanini Nyerere alikuwa na Rashid Mfaume Kawawa kwa maisha yote. Siku zote alimwita Rashid, lakini alipokuwa anang’atuka pale Diamond Jubilee Nyerere alimwita Rashid kwa jina la Kawawa.

Akasema, “Tuna deni kubwa kwa Kawawa’’ halafu akamwaga machozi mengi! Kawawa aliwakopesha nini Watanzania mpaka Nyerere aseme wana deni kwa Kawawa?

Wanawema someni historia. Huko tuendako mnaweza kuja kupata viongozi ambao utaalamu wao ni wakwezi tu wa kuangua nazi.

Tunaambiwa tunapelekwa kwenye uchumi wa kati. Uchumi wa viwanda. Bila uwekezaji hili haliwezikani. Tunawahitaji wawekezaji wema wengi wa aina zote wakiwamo Wazungu. Unamhitaji mtu akuwezeshe halafu unamwita

beberu, wewe uko sawa sawa kichwani kweli? Tukubali chombo kinazama.

Tumeitupa mizigo karibu yote, lakini chombo kinaendelea kuzama. Yuko Yona ameingia ndani ya chombo chetu. Tujikusanye wanawema katika umoja wetu tuulizane ni nani mwenye shida hii? Bila kumtupa Yona baharini, tutaangamia wote. Yona hata kama ni mimi, Baba nitupeni mimi!