Ndugu Rais ni kweli kwamba ukiwa mkweli sana unaweza ukafika mahali
ukasema, bora baba yangu angekuwa ni huyu mzee jirani yetu kuliko huyu
baba niliyenaye! Kuna baba wengine ni kero kwa watoto wao. Na wengine
kama mkosi!
Tunaziona nyumba nyingi na kina baba tofauti tofauti. Utakuta
baba wengine ni walevi wa kupindukia. Wengine wamepagawa kwa michepuko huku wengine kwenye uzezeta hawako na kwenye utimamu nako hawako.
Baba wengine ukikuta amekaa na watoto wake anaongea nao, na wanacheka, wewe hesabu siku hiyo umekutana na mkosi! Hakuna chochote utakachofanya kifanikiwe! Baba wengine hakuna wanachokijua zaidi ya kufoka tu kwa kila kitu na kwa kila jambo. Utakuta hata mtoto wake yule mdogo kitinda mimba anamdharau baba yake! Hakuna mtoto yeyote atamtaka mzazi wa kufokafoka tu kila wakati!
Tujifunze kwa mfano huu. Baba mmoja alipigiwa simu ikisema, “Mtoto
wako ameanguka. Yuko hapa amezimia. Hii namba alinipatia akasema ni ya baba yake kabla hajapoteza fahamu…” Yule baba alikuwa ndani ya
daladala. Waliomuona akiongea na simu ile wanasema hakungoja mpiga
simu amalize kueleza. Mara moja alianza kuhangaika huku na huko
akijisemea hovyo. Mara oh, mwanangu, mara oh, hapa niko wapi? Mara we konda nimekulipa? Mara dereva si usimamishe gari! Mzee wa watu
alifadhaika kweli kweli! Wengine kwa kufadhaika kwake wakatamani
angekuwa ndiye baba yao! Anajali sana watoto wake!
Lakini kuna baba mwingine alipigiwa simu saa nane usiku. Mpiga simu
akasema, “Mimi ni daktari wa zamu. Niko hapa Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwenye meza ya mapokezi ya wagonjwa wa dharura. Mwanao Kangi amepata ajali. Hali yake ni mbaya sana kwa sababu amevunjika miguu yote miwili!…” Baba huyu pia naye hakungoja mpiga simu amalize. Alijibu kwa kifupi tu tena kwa haraka sana, akasema, “Naye huyu mtoto,…
alikuwa anatafuta nini huko usiku wote huu?” Akakata simu. Kati ya hao
wawili ni nani baba, ungependa awe baba yako?
Ndugu Rais, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, kwetu wengine ni mtoto wetu.
Lakini busara anayoonyesha katika kuwaongoza Wakenya wenzake ni
kubwa kiasi kwamba inatufikirisha sana. Anapokaripia huwezi kujua kama
anakaripia! Ni kweli huyu ni rais ambaye ameuonja uchungu na adha ya
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Dhidi ya Binadamu (ICC). Muulizeni
nani alisema rais ana kinga ya kutoshitakiwa? Alisimama kizimbani pamoja
na urais wake! Hakuwa na ulinzi wa kufa mtu? Kenya haikuwa na madege
ya kivita kama haya ya kwetu yanayozagaa huku Mbagala? Akiwa na
naibu wake walipata kuijua nguvu ya dunia dhidi ya kinga! Pamoja na
kuungwa mkono kwa nguvu nyingi na marais wa nchi mbili zilizoko
Kaskazini/Magharibi mwa nchi yetu kutaka nchi za Kiafrika zijitoe,
bado Burundi wameambiwa ili waachane na mahakama hiyo ni lazima wakae miaka miwili baada ya kutimiza masharti yote ya kujitoa.
Ndugu Rais, ‘National Breakfast Prayer’ ni mkusanyiko uliofanywa kati ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa nchini Kenya.
Alikuwapo Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake mkuu, Raila
Odinga. Pamoja nao, alikuwapo Naibu Rais William Ruto na Kalonzo
Musyoka.
Wakiwa mbele ya wananchi kila mmoja alijutia uovu alioufanya
hasa kwa kuwakashifu wenzake wa upande wa pili wakati wa kampeni za
uchaguzi mkuu uliopita. Wakaombana msamaha katika hadhara ile. Halafu
kwa pamoja wakaahidi kuijenga Kenya yao kwa ajili ya maslahi ya
Wakenya wote! Nilimwona Rais Kenyatta akijipangusa machozi.
Ndugu Rais tumepungukiwa nini sisi Watanzania katika ujumla wetu? Hawa ndugu zetu wa Kenya wanatuzidi nini katika kufikiri namna na wakati wa kutenda? Nilimsikia Rais Kenyatta akimwita Raila Odinga,
‘Ndugu’. Katika kuitana ndugu sisi si zaidi ya Wakenya? Mnashindwa
nini kuitana ‘ndugu’ enyi mliokuja kwetu kama ndugu kutuomba kura mpate
kututawala? Uheshimiwa wa kujidhalilisha mbele ya wananchi unapoomba
kura, una heshima gani? Huyu aliyempiga mgombea ubunge mwenzake rungu la kichwa mpaka kuzimia, ana heshima gani katika wadhifa wake kama siyo ufedhuli mtupu?
Ndugu Rais, wananchi wamekosa elimu ya uraia. Watakapoipata watawatimua wote waliokosa adabu na kuwaweka waadilifu! Tukubali, wamewakosea wananchi adabu! Katika mageuzi haya ni baba wa nyumba ndiye anayepaswa kuyaongoza na kuyasimimia. Lakini kinachotokea hivi sasa katika nchi yetu ni malumbano yasiyokwisha yanayosababisha vurugu, ugomvi na vifo vya kusikitisha. Nchi imekuwa kama haina wazee au viongozi watangulizi wenye busara.
Ndugu Rais, Watanzania wataendelea na mateso haya mpaka pale fahamu zitakapowarejea wakawalazimisha viongozi wao kuurejea wosia wa Baba wa Taifa! Baba wa Taifa aliusia, “Mkilifuta kabisa kabisa Azimio la
Arusha, mtakuja kupata taabu sana baadaye!” Baadaye yake ndiyo leo na
taabu sana aliyoitabiri ndiyo hii ya kutekana, kutesana hata kuuana
kinyama na kushambuliana kwa ‘masasi’! Wanadamu kuitwa kama wanyama wasiojulikana ni laana ya kuupuuza wosia wa Baba! Ole wao watu hao!
Tukisema baba, usiache kutupenda. Unajua vizuri kuwa tumekongoroka,
‘tumezeeka’ sana na hatuna tena nguvu za kuendelea kujikimu baada ya
kustaafu kutoka TTCL. Unaposema kwa msisitizo mbele yetu kuwa Serikali
ya Awamu ya Tano haina tatizo na hela huku ukiwa hujatulipa Sh 50,000
katika pensheni yetu moyoni tunaumia sana! Lakini baba si unaona wanao
bado, tunakupenda?
Ndugu Rais, ‘National Breakfast Prayer’, iwafungue fahamu viongozi wetu
wa pande zote mbili – watawala na wapinzani – watambue kuwa kati yao wote hakuna aliye muhimu zaidi ya Tanzania! Nchi yangu kwanza. Wenzetu Wakenya hawakuwa na mahali pa kuanzia, lakini sisi tunahitaji maboresho kidogo tu katika Azimio la Arusha. Viongozi wetu wajue, hata
wakiwashushia Watanzania mwezi wachezee, bila Azimio la Arusha,
wanachemsha mawe! Miradi ya ajabu inazidi kuwafukarisha masikini!
Lakini ni wewe baba yetu leo ndiye unayepaswa kuongoza katika
kuwarejeshea Watanzania urithi wao, Azimio la Arusha! Ukiwa kimya
watajua na wewe utamu wa ngoma, bila Azimio la Arusha umekukolea!