Ndugu Rais, nakupongeza kwa kuwaumbua akina ‘Grace’ wetu wanaokupigia chapuo uongezewe miaka ya urais. Wangekuwa ni watu wa kuona aibu wangetafuta mahali pa kuzificha sura zao. Lakini wauza utu sawa na wauza miili. Aibu waipate wapi?
Kama Mugabe angempuuza Grace wake kama ulivyowapuuza hawa ‘Grace’ wetu, nina hakika Robert Mugabe angekuwa bado ni Rais wa Zimbabwe. Siyo kwamba wana mapenzi na wewe, la hasha, wanataka tu wakutumie kufanikisha malengo yao. Hawa ni watu wa kuogopwa kama ukoma.
Tunauguza, hatuuguzi sitosita kukupongeza pale unapofanya vema. Na wala sihitaji ujasiri wowote ili nikutie moyo. Kumpokea Edward Ikulu kwa mazungumzo, pongezi nyingi sana kwako. Umetukumbusha busara kubwa za marehemu Gandhi aliyeleta uhuru wa India bila mapambano ya kumwaga damu.
Julius Kambarage Nyerere alituletea uhuru wa nchi hii ambao leo tunaukanyaga, kwa busara tu ya mazungumzo. Busara yake iliiepusha nchi isipitie katika mapambano ya kumwaga damu. Baba kumpokea Edward Ngoyai Lowassa hapo Ikulu kwa mazungumzo unastahili kupongezwa na kutiwa moyo.
Niliandika zaidi ya mara moja baada ya uchaguzi kukushauri ufanye jambo jema hilo la wewe kukutana na mshindi wa pili. Mshindi wa pili ndiye kipenzi cha wananchi wengi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote ukimwacha Rais aliyechaguliwa. Ndugu Rais, sijui ni nani aliyemwita T.B. Joshua nchini mwaka 2015.
Yawezekana ni kweli mtu huyu akawa ni mtu wa Mungu kwa kuwa alionesha kuipenda haki. Tofauti na baadhi ya viongozi wetu wa dini ambao wamejiundia kamati za siasa wakiziita za amani ambao Watanzania waliwashuhudia wakiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wakiwa wameinua mikono yao wakitazama juu mawinguni, eti wanauombea uwanja wa ndege.
Kwa akili yao Mwenyezi Mungu anakaa juu zinakopita ndege. Huyu mtumishi wa Mungu alipokewa uwanja wa ndege na mwingine, lakini wakati wa kuapishwa alienda kuiombea haki nyumbani kwa Edward. Wengi wangetarajia angeenda kwenye siasa lakini alienda kwenye maombi. Baadhi yao viongozi wetu wa dini wametambua kuwa kwenye siasa kuna anasa na mali nyingi.
Wako radhi kuwaunga mkono wanasiasa hata pale wanapowaumiza waumini wao; waja wa Mwenyezi Mungu. Kwao makanisa na misikiti ni ofisi kama zilivyo ofisi za watu wengine. Wanajaribu kupita njia mbili kwa wakati mmoja.
Ndugu Rais, hatujasikia lawama dhidi yako kwa uamuzi wako mwema wa kumpokea Edward huko Ikulu, hata kama hukukishirikisha chama chako. Wanaweza kuwa siyo wote lakini hii ni ishara ya ukomavu kisiasa. Lakini upande mwingine yamesemwa maneno mengi butu yanayoashiria mgando wa fikra.
Anasema, “kosa la Lowassa lilikuwa ni kuibuka na kauli ambazo kwa namna moja au nyingine ziliumiza wengine”. Fikra muflisi kabisa. Atuambie, tangu lini kwinini ilikuwa tamu? Mwingine anasema, “viongozi na wanachama wetu wanashambuliwa hadharani kwa mapanga na hata kwa risasi, kumsifia Rais ni kumuunga mkono yeye…kazi nzuri inayofanywa ina maana gani kama si kuhalalisha ukandamizaji tunaofanyiwa….” Umbali mrefu anaoona ni urefu wa pua yake.
Kumwita mpinzani wako kisiasa, ‘adui’ ni kukosa busara. Huu ni wakati wa kuwa na mtazamo mpya kwa pande zote mbili. Ni wakati wa upande mwingine kuona kama uliwaumiza wengine kwa mapanga au kwa risasi, ufanye kitubio na kuanza upya. Ujeuri na ujivuni mwisho wake ni majuto. Hawa viongozi wetu wawili wametufungulia njia ya mazungumzo, tuitumie.
Aliyosifia yote Edward aliyataja. Kama Edward alimsifia Rais wetu sifa asiyostahili, ithibitishe. La, anastahili kwanini kumpinga kote huku? Walisema busara ni kutazama pande zote mbili za shilingi. Sasa bila kutumia njia ya mazungumzo wakimaliza kuuguzana watashika mtutu wa bunduki?
Yawezekana Edward katika kundi lake ni sawa na mti mmoja mrefu ulioota jangwani. Kuna njia mbili za mapambano. Kupambana kwa hoja kwa njia ya mazungumzo na kupambana kwa kutumia mtutu wa bunduki. Edward kukubali kwenda Ikulu, amechagua njia ya mazungumzo. Alikwenda kuisaka suluhu kwa njia ya amani.
Tunahitaji amani ya kweli katika nchi yetu. Walishikana mikono huku kila mmoja akiwa na tabasamu pana usoni mwake. Tazama ilivyopendeza ndugu wawili kuishi pamoja kama wana wa baba mmoja. Wakuamua kutumia mtutu wa bunduki, nasema ole wake! Imeandikwa kuwa atumiaye upanga, atakufa kwa upanga!
Ningejaliwa uwezo wa kumlaani mtu, ningemlaani mtu huyu ili alaaniwe hapa duniani na juu mbinguni aliko Baba yetu wa kweli. Edward aliomba kukutana na wewe Rais wake ili ikikupendeza baba, myasawazishe mambo haya ya kinyama yanayotokea katika Taifa letu hivi sasa, kwa njia ya majadiliano.
Na kwa sababu na wewe nia yako kwa nchi yako na watu wako ni njema, ukamwita Edward hapo Ikulu mpate kuzungumza. Umewaambia Watanzania kuwa Edward ni mstaarabu sana ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita alifanya kampeni za kistaarabu. Pamoja na changamoto nyingi alizopitia yeye na wafuasi wake, lakini umesema baba, kuwa haikutokea hata mara moja, mahali popote ambapo Edward alitoa tusi au alikutukana!
Ndugu Rais, kwa sifa hizo ulinikumbusha siku yangu ya kwanza kukutana na Edward uso kwa uso. Mwenzangu alikuwa waziri, mimi nilikuwa hivi hivi nilivyo, lakini Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na watu wengine, alituita nyumbani kwake, Msasani. Wakati Baba wa Taifa akiwaonya viongozi wetu wasilitupe Azimio la Arusha alimkazia macho Edward na kumwita;
“Na nyinyi wengine!” Tulipoingia katika kiofisi chake, Mwalimu Nyerere tulikaa kwa kubanana. Bega langu la kushoto liligusana na bega la kulia la Edward. Mwalimu Nyerere kwa mkono wake wa kulia, alimshika Edward mkono wa kushoto sehemu tunapovalia saa, akamwambia, “nchi inauzwa”.
Kila mahali panauzwa. Tumesema sana lakini hakuna anayetusikia. Lakini wewe unasikia! Nenda kawaambie wenzako msiuze nchi”. Kuanzia siku hiyo, nilianza kumsoma mtu huyu! Iweje hata Baba wa Taifa aonesha kuwa na imani naye? Baba, najivunia uamuzi huu wa Edward sawa ninavyojivunia uamuzi wako kwa jambo jema hili kwa maana nilitangulia kuliona jua kabla yenu!
Tusiichezee amani ya nchi yetu.
PASCHALLY MAYEGA
SIMU: 0713 334239