Ndugu Rais, tangu tulipojipatia Uhuru kutoka kwa wakoloni, zimepita awamu nne. Hii tuliyomo ni awamu ya tano. Kama nchi tumo katika mwendo. Hivyo ni busara kwetu kugeuka na kutazama nyuma kuzichambua zile awamu nne ambazo tumepitia ili tupate kuihukumu awamu hii ya tano kwa mema yake na kwa mabaya yake. Na kwa kufanya hivyo tutajua kule tunakoelekea kama ndiko au siko!

Awamu ni rais, hivyo tunapoongea juu ya awamu tano, tunaongea juu ya marais watano. Rais Julius Kambarage Nyerere, Rais Ali Hassan Mwinyi, Rais Benjamin William Mkapa, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, na sasa Rais John Pombe Magufuli.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa awamu ya kwanza alikuwa mtu mcha Mungu ambaye leo tunaishuhudia dunia ikihangaika ili atangazwe kuwa ni mmoja kati ya Watakatifu wa Mwenyezi Mungu.

Alikuwa Mkatoliki aliyeishi katika Ukatoliki wake bila kutangatanga katika nyumba tofauti tofauti za ibada. Hata Muumba wake alipomwita arejee katika makao yake ya milele alikufa akiwa Mkatoliki asiyetiliwa shaka.

Baba yetu alitukuza katika imani, akatulea katika njia ifaayo nasi hatukuiacha mpaka walipokuja mafarao! Nyerere alitufundisha sala ya umoja ya kwamba sisi ni ndugu na binadamu wote ni sawa. Tuliaminishwa kuwa Afrika ni moja kama ilivyo Tanzania. Waliopo na wengine wengi wajao hakuna wa kufananishwa naye!

Aliwaumbia uadilifu viongozi aliotaka watuongoze kwa kuwawekea kidhibiti mwendo – Azimio la Arusha. Wakaipenda nchi yao na kuitumikia kwa uzalendo wa kweli siyo huu wa sasa wa watu kujitangaza wenyewe.

Wananchi tukajisikia kuwiwa. Tukaweka sentensi katika wimbo wetu wa taifa kumwomba Mwenyezi Mungu awabariki viongozi wetu. Sentensi hii sasa wengi hawaiimbi wanapoimba Wimbo wa Taifa. Afadhali kumwombea shetani kuliko kuwaombea baadhi ya wezi, watekaji na watesi wa watu!

Tulistawi katika umoja, tukajengeka katika mshikamano na kama walivyo ndugu, wote tuliitana ndugu! Baraka za Mwenyezi Mungu zikatamalaki kati yetu na katika nchi yetu!

Ndugu Rais, alipokuja Mzee Mwinyi kipya hakikuonekana kwa maana mning’inio wa Nyerere ulimfunika katika miaka yake yote kumi. Alikuja bila alama, akaondoka bila alama! Lakini dhambi kubwa iliyotendwa na awamu ya pili ambayo kwa ukubwa wake itakumbukwa na vizazi vingi vijavyo ni kuliua Azimio la Arusha! Nasema ole wao watu hawa!

Nawaachia jua la Mwenyezi Mungu liwaakie utosini! Wanawema msikate tamaa, Mungu yupo. Iko siku atawapatia kiongozi amchae naye atawarudishia urithi wenu mliodhulumiwa na mafisadi ‘Azimio la Arusha!’

Kwa kuiongezea ukubwa dhambi yao wakaukana ‘undugu’, wakajiita ‘waheshimiwa’! Leo hata baadhi ya wahuni wanaitwa waheshimiwa. Kujiita mheshimiwa mbele ya wananchi waliokuajiri wewe HUNA ADABU!

Awamu ya tatu ilikuja na ubabe. Dosari kubwa lilikuwa ni pale Serikali ilipoamua kuua kwa kisingizio cha kuzima upinzani. Kwa mara ya kwanza Tanzania ikawa na wakimbizi nchi za nje. Dosari lingine kubwa ni jinsi Serikali ilivyojitahidi kuvimaliza viwanda vyote na mashirika ya umma, kwa kasi ya ajabu. Vingine iliviuza kwa bei sawa na bure huku vingine ikivibinafsisha kwa mkopo. Vingine iliamua kuvitelekeza tu huku vingine wakijigawia wenyewe viwanda hivyo na mashirika yaliyokuwa ya wote!

Baadhi yao wakaanza kujaa mali wao na familia zao. Wakaanza kuishi peponi katikati ya jehenamu ya masikini!

Katika maadili na miiko ya uongozi vilivyokuwako ndani ya Azimio la Arusha dhambi hii isingefanyika. Hata hivyo, haitawaacha salama.

Itabaki juu ya vichwa vyao siku zao zote za maisha yao! Atakapokuja kutokea mtu kati ya wale wale akasema ataifanya Tanzania kuwa ya viwanda timamu watakaposhindwa kumwelewa asiwakasirikie. Awaeleze kwanza ujinga ulifanywa lini, ni wakati ule wa kuviua au ni sasa tunapojaribu kufufua maiti?

Ndugu Rais, Serikali ya awamu ya nne ilikuwa ni janga kwa Taifa hili.

Uporaji ulioanzishwa na awamu ya tatu sasa ukaruhusiwa na kufanywa kuwa ni rasmi. Baadhi ya viongozi wakawa wanashindana kuiibia nchi hii! Wengine wakawa wanashinda mawinguni huku wengine wakikesha kwenye makasino ya wazungu Ulaya!

Wananchi waliumia kuona nchi yao inavyoporwa na baadhi ya viongozi wao, lakini waliishia kuugulia katika vifua vyao wasimwone wa kumlilia!

Hivyo haikushangaza kuona wananchi walioumizwa kwa miaka mingi wakimkumbatia mwana wa mtu aliyewaahidi mabadiliko! Baba uliwapoza wengi ulipowaahidi Watanzania kuwa hutakuwa pamoja nao! Ni nini hii sasa inayotokea?

Ndugu Rais, ujio wa awamu ya tano ulikuwa kinyume na matarajio ya wengi, lakini mipango ya Mungu nani aijuaye? Kuihukumu awamu ya tano kwa mema yake au kwa mabaya yake kwa sasa kunaweza kuonekana kama kutoitendea haki kwa sababu ndiyo kwanza iko katikati ya muhula wake.

Lakini ni haki vilevile kusema wakati inaanza, ilionyesha kutojiamini, ikautumia woga kama msingi wa siasa zake.

Wakati awamu ya nne itakumbukwa kwa wizi na uporaji na kupenda anasa kupindukia kwa baadhi ya viongozi, sisi tunaweza kuja kukumbukwa kama awamu iliyopandikiza chuki kubwa miongoni mwa wananchi tangu kupata Uhuru. Vitendo vya kikatili, watu kuvamiwa, kutekwa, kuumizwa na wengine kupotezwa visipodhibitiwa, haviwezi kuja kutuachia kumbukumbuku nzuri kwa wananchi.

Kuwakamata waliochangishana fedha kuwapa rambirambi wafiwa wa watoto wa shule ya Lucky Vincent kuchukuliwa na Serikali kwa amri ya mkuu wa mkoa kunakuchafua wewe baba mbele ya watu wako! Busara ilikosekana.

Ndugu Rais, marehemu Philemon Ndesamburo angeagwa katika Uwanja wa Mashujaa kungedhuru nini? Uwanja ulijengwa kwa nguvu ya wananchi zikiwemo nguvu za marehemu mwenyewe. Aliyezuia anataka Watanzania wakueleweje? Vijana wako wanakutengezea chuki na visasi kwa Watanzania! Wanachotaka Watanzania ni amani na upendo kati yao kwa kuwa hivyo ndivyo walivyolelewa na Baba yao wa Taifa!