Ndugu Rais kazi ambayo unaifanyia nchi hii ni njema sana. Na kwa hili Mwenyezi Mungu akutangulie! Lakini, baba, tambua kuwa katika kuifanya kazi hii njema, uko peke yako!
Na maadui wako wakubwa wako nguoni mwako! Kumbuka methali ya kikulacho…
Baba haya makaburi unayofukua yana wenyewe; unadhani wanapata usingizi? Wale ulioshindana nao katika kugombea kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama chako katika mbio za urais na wenyewe wana makaburi yao.
Wanavyokujua, wanajua iko siku utayafikia. Unadhani wanapata usingizi? Lakini je, wamekwambia kuwa urais wa 2020 hawautaki tena?
Pamoja na hao lipo jeshi la polisi. Kuna ufisadi mwingi umefanywa na polisi, Lugumi ikiwagusa vigogo wengi. Wanajua machungu yatakayojiri juu yao na wana wao utakapolifikia kaburi la Lugumi!
Hata hawa uliowaondoa, unadhani huko walikokwenda wanapata usingizi? Hawa wote na wengine lazima wanajipanga kukabiliana na janga linalotishia shingo zao!
Ndugu Rais kubwa kabisa wanaweza kulifanya ni kuchezea akili za wananchi ili wananchi wengi zaidi wakuchukie! Lakini kwakuwa wewe unafanya kazi iliyo njema endelea! Mungu wa Eliya atasimama upande wako! Baba ukweli utabaki ukweli hata baada ya nyakati kupita! Atakuwa ni mjinga sana atakayesema hakuna mtu aliyeko juu ya sheria bila kuweka kichwani mwake kuwa sheria hutungwa kwa ajili ya watu na si watu kwa ajili ya sheria.
Ndugu Rais matokeo ya urais katika uchaguzi mkuu wa 2015 yaliyokupa ushindi yalionyesha kuwa Edward alikuwa mshindi wa pili akifuatiwa na dada Ana Mghrwa. Kwa matokeo hayo imethibitika bila kuacha shaka kuwa, baada ya wewe Rais wetu, Edward ndiye raia wa nchi hii anayependwa na wananchi wengi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote!
Na hii inadhihirika zaidi anapoonekana hadharani, wananchi humfuata bila yeye kuwaita! Kwa mwenye haki angependa kujua na kujifunza kutoka kwake ni kipi kinamfanya awe kivituo cha watu? Ukibaki na mawazo kuwa anaandamanisha watu au anafanya mikutano bila kibali jua ndugu yangu akili yako ni fupi! Hufai!
Katika marekebisho ya katiba mpya kwa mujibu wa kitabu cha Mwalimu mkuu wa watu ukurasa wa 110 imeandikwa, “Mshindi wa pili katika kinyang’anyiro cha urais atakuwa mbunge moja kwa moja, naye ndiye atakuwa mkuu wa kambi ya upinzani bungeni.” Unamuachaje huyu nje ya Bunge?
Ndugu Rais wako wanafiki ambao wanajua kuwa kumtingisha huyu ni kugusa mboni za wananchi wengi. Ili kuwafanya hao wengi wakuchukie, wakati wengine walikuwa wanaserebuka katika kumalizia sikukuu ya Idd, Edward alikuwa akihojiwa na polisi.
Ndiyo, inawezekana ilikuwa ni lazima mahojiano hayo yafanyike wakati wa sikukuu lakini kwa yeyote anayefikiri sawasawa kitendo hicho kilimvutia mtuhumiwa huruma kutoka kwa watu wema. Si hivyo tu kilileta hisia ya kukomoa ambayo haikuwa ya lazima!
Baba tunaumia tunapowaona wanafiki wachache wanavyojaribu kuharibu nia njema na utendaji mahiri wa Rais wetu! Wanataka wananchi wasitilie maanani kazi njema inayofanywa na Rais wetu!
Ndugu Rais fikra hizi zisingejitokeza kama wangemkamata siku ileile anayodaiwa kufanya huo uhalifu kama kweli ni uhalifu! Au hawa ndiyo walewale wamleka zipita nga masala yawazana?(watu wanaopata akili baada ya mambo kuharibika). Kwa waliopungufu kila neno hata la kumsifu Mungu, katika awamu ya tano linaweza kuwa uchochezi!
Ndugu Rais siku iliyofuata gazeti moja, (Harrison, siyo hili) liliandika habari kuu ikisomeka, ‘Ni ulinzi wa kufa mtu’ mahojiano ya Lowassa. Tunaulizwa, alikuwa analindwa nani? Mfungwa akiwa gerezani halindwi, linalindwa gereza. Mfungwa analindwa akiwa nje ya gereza asitoroke. Banki au mali ya thamani inalindwa isihujumiwe. Edward kwa ulinzi wa kufa mtu alikuwa analindwa asitoroke, au kama kito, asihujumiwe? Hapana! Kulikuwa na bunduki na risasi nyingi za kuulia binadamu!
Kulikuwa ulinzi angani na magari ya maji ya kuwasha. Bunduki na risasi hizi pamoja na maji yakuwasha vilielekezwa kwa Edward? Hapana! Vilielekezwa kwa wananchi ambao hawakuwa hata na silaha yeyote! Kumbe ulinzi mwema wakufa mtu walikuwa ni watu wa Mungu!
Ndiyo ulinzi huu wa kufa mtu alionao Edward, ambao nami natamani baba ungekuwa nao! Watu wenye hofu ya Mungu!
Ndugu Rais wakati hayo yakijiri watu wawili kule Kibiti waliuawa na mmoja kutobolewa jicho baada ya kupigwa risasi kichwani! Kwanini huu ulinzi wa kufa mtu haukupelekwa Kibiti? Wauaji waliondoka na mwili wa marehemu mmoja na kutokomea nao kwenye kijiji au sijui mji unaoitwa ‘kusikojulikana’!
Yawezekana vipi kuwe na sehemu isiyojulikana iliko katika nchi hii? Hizo maiti wanazoondoka nazo wanazisafirishaje kama siyo kwa gari? Leo wananchi wanaambiwa polisi imeua wauaji wanne. Waliwakuta wanaua? Wananchi watajuaje kama ni kweli waliouawa ni wauaji au ni ndugu zao wengine? Kwa ujinga wetu tunawachekea mgambo na Bashite wanaotutengenezea Kibiti yetu nyingine itakayokuwa chungu zaidi!
Ole wake atakayewalinda wasaga sumu hawa!
Baba tuliandika huko nyuma kuwa hizi bunduki na risasi za moto haziwezi kukomesha mauaji ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji! Au ubabe ambao labda hatuuoni au kufokafoka na kuzuia kila kitu kunaweza kuwa ndiyo chanzo cha yote haya! Katika ujumbe wao waliowasambazia wananchi wamesema, “Tunawatangazia wananchi kuwa, tumewaua polisi kwasababu wanadhulumu watu kwa kutumia kazi zao na yeyote atakayefanya kazi hapa au nje ya hapa tutamtafuta hata nyumbani kwake. Sisi tumejitolea kufa kuliko kuishi. Hakuna njia yakumaliza dhuluma isipokuwa chuma tu, hapa ni chuma tuu!”
Diwani mmoja amenukuliwa akisema, “Kundi hilo linaonyesha bado lina uwezo mkubwa wa kufanya mauaji na kutokomea kusikojulikana!”
Baba yawezekana hofu kubwa tuliyonayo, inatusukuma kutumia nguvu kubwa mahali isipohitajika na kuonekana kupwaya kule nguvu hiyo inakohitajika!
Ndugu Rais yatupasa kusikiliza! Ili tusikilize tuwaache waseme. Hawa wanaozuiwa wasihutubie sasa wanatengenezewa mazingira mazuri na wanatayarishiwa umati mkubwa wakati wakuhutubia utakapofika! Wananchi watataka kuwasikiliza wao, kwa maana watakayoyasema kwa wananchi yatakuwa yote mapya!
Hawa wanaohutubia sasa wananchi watakuwa wamewasikia yote na hata wengine watakuwa wamekwisha chokwa! Nani atakwenda kuwasikiliza?
PASCHALLY MAYEGA
SIMU: 0713 334 239