Ndugu Rais mara nyingi katika maandiko yangu hunukuu maandiko
yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Sababu kubwa ni
kwamba sitaki wengine wafikiri ninaandika haya kwa kumlenga mtu au kwa
kuilenga mamlaka yoyote.
Wanaofikiri hivyo wamekosea sana! Lengo la maandiko haya ni kushauri kwa nia njema bila unafiki. Tutasifia pale panapostahili kusifiwa na tutakosoa pale panapostahili kukosolewa. Lengo ni moja tu, kujenga. Tanzania ni moja na ni ya Watanzania wote waliopewa na Mwenyezi Mungu katika ujumla wao!
Ndugu Rais, ukweli husimama kwa nyakati zote. Haubadiliki kama nyakati
zinavyobadilika. Na kwa sababu hiyo, maandiko haya yaliyoandikwa miaka
15 iliyopita yanaposomwa leo yanaonekana kama yanawalenga walio na mamlaka leo, wakati yaliposomwa jana yalionekana kama yaliwalenga waliokuwa na mamlaka jana. Na hivyo ndivyo itakavyokuwa yatakaposomwa kesho. Mwanamwema aliniandikia ujumbe yapata miaka 10 imepita akasema, “Mwalimu Mkuu maandiko haya yakijasomwa miaka 10 ijayo, watu watasema alikuwako nabii, lakini watu walioishi wakati
wake, hawakumtambua!”
Leo yanapotimiza miaka 15 ukweli umebaki vilevile! Dunia iliyaenzi maandiko haya kwa namna tofauti-tofauti tangu yalipoandikwa, lakini tumshukuru Mungu kuwa na nyumbani heshima sasa ya maandiko haya inaonekana kwa wanawema!
Ndugu Rais, ziko kelele kutoka kwa baadhi ya watu wanasema wanataka
watuletee Tanzania mpya. Ni kweli Tanzania tuliyonayo watu wake hawana
furaha nayo! Wamejaa hofu maisha yao ni ya wasiwasi! Hiyo mpya waitakayo si itatisha zaidi? Tanzania waitakayo siyo, tuitakayo!
Watuache tuendelee kupuyangapuyanga hivi hivi, tutafika. Tumwombe Mwenyezi Mungu atuepushe na janga la Tanzania mpya! Hatuitaki Tanzania mpya kama ambavyo hatuitaki hii tuliyo nayo leo!
Ndugu Rais, kama kati yetu kuna mwenye uwezo wa kutubadilishia Tanzania yetu, basi aturudishie Tanzania yetu ya zamani. Aturudishie Tanzania iliyotufanya wote tujione ndugu tukaishi katika upendo huku furaha na amani ya kweli vikitamalaki! Tanzania ya wana ndugu siyo hii ya
waheshimiwa na watwana! Tanzania ya elimu bora iliyolipiwa kwa kodi ya
wananchi na siyo hii Tanzania ya bora elimu ya bure.
Tanzania ya ndugu Julius Kambarage Nyerere mwanaAfrika wa kweli! Mwana huyu ambaye hakuuonja unafiki wala hakutawaliwa na ubinafsi! Tanzania ya Azimio la Arusha ambalo kwalo haki za binadamu ziliheshimiwa na viongozi wote.
Tanzania ya viongozi walioiheshimu katiba ya nchi! Viongozi wetu
walikuwa ndugu zetu na kwa pamoja tuliitana ndugu! Hiyo ndiyo Tanzania
tuitakayo. Tanzania ya leo, siyo! Katiba ya nchi juu ya haki za mtoto iko wazi na inamtambua mtoto kwa umri wake usiozidi miaka 18. Unapokubaliana na mama mtu mzima, umri wake zaidi ya miaka 30, na huenda ni mke wa mtu kuwa ni mtoto na unachukua hatua eti unamsaidia mtoto aliyetelekezwa, unajidanganya mwenyewe zaidi kuliko unavyodhani kuwa unawadanganya wananchi.
Bwana Yesu aliwakumbatia watoto, akasema, “Waacheni watoto
wadogo waje kwangu kwa maana ufalme wa mbingu ni wao!” Kwa ujasiri
ulionao, ungeweza kulibeba lile li-mama ukampelekea Bwana Yesu, na
kumwambia, “Kristu, nimekuletea mtoto!” Mama mwenyewe, ah, samahani
mtoto kwako mwenyewe anapokuumbua na kusema niliyemtaja siyo baba
yangu naomba anisamehe, wananchi wakilichukulia zoezi zima kuwa ni
unafiki mkubwa uliofeli kwa sababu haukupangiliwa vizuri, watakuwa
wamekosea wapi?
Usipokuwa makini utafungwa kwa kosa la kuwatumia wamama wa mtaani walioshindikana ili uwachafue watu wenye heshima zao katika jamii yetu na siyo kwa ajili ya kuwatetea watoto! Anaposema hili ni jambo la kisiasa ana maana kuna watu walimsukuma ashirikiane na waandaaji wa mpango huu kwa lengo la kuwachafua wengine? Siasa za majitaka hazina nafasi tena. Tukiendelea hivi, muda wa kujenga viwanda tutaupata wapi? Au nayo ni kelele sawa na zile za maisha bora kwa kila Mtanzania au Kilimo Kwanza au Elimu Bure?
Ndugu Rais, mwanamwema Warren Buffet alisema, “Kuna mtu amekaa kwenye kivuli leo, kwa sababu kuna mtu aliupanda mti huo miaka mingi
iliyopita!” Leo kuna tambo nyingi. Baadhi ya viongozi wetu wanatamba
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haina tatizo la fedha; inazo fedha
nyingi sana. Kwa matumizi tunayoyaona ni kweli Serikali inazo fedha
nyingi sana, lakini inanunua vitu! Ni kama maisha ya watu hayana
umuhimu sana kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Viongozi wetu kwa mamlaka makubwa na fedha nyingi zilizoko, wako kivulini. Wanafaidi matunda ya nchi! Baba kumbuka, mko kivulini leo kwa sababu kuna watu waliupanda mti huo unaowapa kivuli leo, miaka mingi iliyopita! Watu hao si
wengine ni hawa wazee wetu wastaafu! Hawa ambao tulianza kuitumikia
nchi hii tukiwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ile iliyovunjika!
Tukastaafu baada ya kutoka ‘EAST AFRICAN POSTS & TELECOMMUNICATION CORPORATION tukaja TANZANIA POSTS & TELECOMMUNICATION COPORATION halafu TANZANIA TELECOMMUNICATION CAMPANY (TTCL).
Pamoja na Bunge, wewe ukiwa mbunge wakati huo, kuidhinisha tuongezewe Sh 50,000 katika pensheni yetu, Baba mpaka leo bado unatulipa kiwango kilichopita cha Sh 50,000 kwa mwezi!
Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Wananchi wanataka rais ambaye atawathamini raia waandamizi waliokamilisha wajibu wao na kustaafu katika ujenzi wa taifa ili wasipate shida katika wakati wao wa kutokuwa na nguvu za kuendelea kujikimu. Hivi sasa wastaafu wanaishi katika uchochole wa kutisha. Pensheni yao ni ya kijungujiko.”
Baba, tambua kuwa, ni sisi tuliopanda huo mti ambao leo mnafaidi kivuli
chake. Wakati mkiendelea kufaidi kivuli chake wacha na sisi tuendelee
kupukutika kutokana na dhiki tulizonazo! Kwa kuwa Bunge liliidhinisha,
na kwa kuwa siku hazigandi, kesho tutachagua viongozi wenye moyo wa
utu, watatuhurumia, watatulipa. Kama hawatatukuta sisi watawalipa
watoto wetu na wajukuu wetu! Ila! Kama ni kweli wazee wanapofurahi
hubariki na kutoa baraka watashindwa vipi wanapohuzunika na kukata
tamaa wasitoe laana? Ole wetu sisi!