Ndugu Rais, kwetu tunaamini kuwa ukizushiwa kifo au hata ugonjwa tu, unatabiriwa maisha marefu. Imani hiyo kwetu bado ipo. 

Hivyo, kusema fulani kafa au ni mgonjwa hatari, wakati si kweli, yalikuwa ni maneno yakutia faraja na matumaini kwa anayezushiwa hayo. Najua hapa si kwetu, tuko kwenye jiji la Makamba. 

Ila huyu aliyezusha hili la kuzusha, ingekuwa kwetu, angekuwa amemtengenezea faraja kubwa mzushiwa na wananchi wote.

Rais wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika vipindi vyake vyote hakuna siku wananchi walitangaziwa kuumwa kwake. Nyerere alithamini sana utu wa wananchi aliowaongoza. Hakuwa na kiburi cha kujiita mheshimiwa kwao. Alijishusha mpaka akafanana na watu wake. 

Kwa pamoja wakawa ndugu, wakaitana ndugu. Alipowaambia mimi ni mtumishi wenu, alisema kweli hawakumwona laghai. Aliwatibia wananchi wake wote kwa kodi zao bila malipo ya ziada. Akawapa watoto wao elimu iliyo bora kabisa, mpaka ile elimu ya juu, vivyo hivyo bila malipo ya ziada. 

Alikuwa mcha Mungu mtu yule. Hakuwahi kusikika hata siku moja akiwadanganya wananchi kuwa alitoa matibabu au alitoa elimu bure. Bali kwa moyo wa dhati kabisakabisa, aliwaambia Watanzania: “Mkiona tumejizidishia ulinzi jueni tunawaibia!” Alale pema mwanamwema huyu! 

Yaliyotokea kama ni uzushi au ni ukweli, mimi siko huko. Niko kule iliko maana ya haya yote mawili! Iweje upepo uvume kwa siku tatu mfululizo kusitokee kauli yoyote ya kukiri au kukana kutoka serikalini, Ikulu, katika chama na hata kutoka kwa wale ambao mzee Butiku anawaita makuwadi? 

Yawezekana ni kwa sababu ya usiri mkubwa ndiyo maana waliokuwa na huzuni hawakuonekana. Waliokuwa wanacheka walionekana kuwa wengi. 

Mpaka sasa wananchi hawana uhakika kama baba yao alikuwa anaumwa kweli au ni uzushi tu kama wanavyoambiwa. Tusiwaachie wengine, tutafakari wenyewe! 

Kama ni kweli baba alikuwa anaumwa, cha ajabu kilikuwa kipi? Watangulizi wake waliumwa na nchi haikuona ajabu. Rais Benjamin William Mkapa alilazwa hospitalini nje ya nchi kwa zaidi ya miezi mitatu. Haikutokea taharuki kama hii. Watanzania bila kujali tofauti ya vyama vyao waliungana pamoja kumuombea! Alipona na akarudi kujumuika na watu wake tena. Nchi haikutikiswa!

Watanzania tena Rais wao, Jakaya Mrisho Kikwete, aliumwa, alilazwa na kufanyiwa upasuaji katika hospitali nchi ya nje. Naye Watanzania walimuombea, akapona na kurudi, akajumuika na watu wake na nchi haikutikiswa. Kwanini  sasa hali hii? Si kwamba hakukuwa na baadhi waliowachukia marais hawa, bali katika ugonjwa taifa lilikuwa moja!

Kifo cha Baba wa Taifa kililiza Watanzania wengi! Kusema kweli mpaka leo wapo Watanzania, nikiwamo, ambao bado tunamlilia! Katika matukio yote haya taifa lilisimama likiwa moja. Makuwadi kuanza kutaja majina wanaweweseka. Wanatafuta mbinu za kumzuga mfadhili wao. Hapa hatetewi mtu. 

Wawaambie wananchi wakati ule wa siku tatu za ukimya wa mashaka walikuwa wapi? Kati ya hao watu milioni tatu wanaodai wanawamiliki kwa nini hakutuma hata mia tu waje kumpigania wakati wa majaribu? Rais wa nchi ni baba yetu wote. Makuwadi wanataka kuonyesha kuwa baba anachukiwa na wananchi wengi ila wao ndiyo wanampenda zaidi kuliko wanavyowapenda wazazi wao. Mbona walimwacha peke yake apambane na hali yake? 

Wananchi wana matumaini na rais wao. Fumbo mfumbe mjinga, hapa hatetewi mtu. Wanatetea matumbo yao. Jamaa hawa, ni waoga ajabu. Walijaa hofu wakaenda mafichoni. Wakawa wanasikilizia kwa mbali kama tayari, wasambae duniani kwenye makazi waliyojiandalia, huku wakibeba vyote vya wananchi walivyojikusanyia.

Lakini kama baba hakuumwa, basi yanayoendelea ni uhuni. Kwa nini tunawatukuza wahuni? 

Lakini na wewe baba ulikuwa wapi? Iweje habari za magumu yetu ziwe faraja kwa wananchi wengi kiasi hiki? Kujitazama upya si ujinga! Lazima kuna mahali tumewakosea wananchi. Tujisahihishe!

Busara ni kujutia makosa yetu! Tuungane na busara ya mwanamwema, Onesmo ole Ngurumwa, aliyesema: “Miaka iliyopita watu hawakuwa wakiombeana mabaya. Kulikuwa na siasa za ushindani kuliko hivi sasa. Turudi kwenye siasa za undugu, umoja na mshikamano kwa sababu sisi wote ni kitu kimoja”. Mwana huyu ainuliwe kwa wazo lake hili jema. Naye malango yake yabarikiwe!

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mpinduzi, Phillip Mangula, alipokuwa Butiama alisema: “Ili kuepuka makosa ya viongozi wa chini, Mwalimu Nyerere alihakikisha viongozi wanafundishwa kanuni, miiko, majukumu na dhamana ya uongozi na malengo ya serikali. Baada ya kutoka chuoni walipelekwa wilayani (vijijini) kuishi na wananchi kujifunza kwa vitendo maisha halisi ya watu kabla ya kupangiwa na kusambazwa kwenye vituo vya kazi. Kwa sasa hawaendi. Kwa hiyo kila mtu anakwenda kwa utaratibu wake. Ana buni mwenyewe namna ya kuendesha shughuli zake za kuongoza nchi. Hakuna utaratibu wa pamoja wa namna ya kuchukua mafunzo”. 

Phillip Mangula anakiri kuwa viongozi wa sasa kwa kutokwenda mafunzoni kufundwa, tangu wakati wa Mwinyi hadi sasa, wanaongoza nchi kwa kupuyanga tu. Kila kiongozi anapuyanga kivyakevyake!

Unamkuta mtoto wa kike kakomaa sura kama dume. Kaishupaza shingo yake mpaka mishipa ya kichwa imemsimama. Hataki waumini wamsujudie Muumba wao kwa siku asizotaka yeye eti kwa kuwa ni mkuu wa wilaya. 

Baadhi ya viongozi wanapopuyanga wanapumbazwa na kelele za vuvuzela wakidhani wanawashangilia. Ukimwangalia, huwezi kujua kama ana dini au la. Mwenzake, madereva wote wa nchi hii hawafai kumwendesha kwa sababu wanayapanda matuta ya barabarani. Dereva akipanda tuta barabarani makofi, kwanini anamwinua mheshimiwa mkuu wa wilaya. 

Mwingine ni mkuu wa mkoa kabisa, huwezi kuamini. Kichwani hana kitu anachowaza. Amefilisika kabisa. Amebakiwa na wazo moja tu, kupiga. Ole wako agundue kuwa hujaoa au hujaolewa. Anasema ni viboko tu. Anajidai kwa sababu wenye roho ya kufanana naye wanampongeza. 

Tuwahurumie wananchi. Wameteseka kiasi cha kutosha. Kwa utendaji huu wa baadhi ya viongozi, wananchi wamejikuta wamebeba serikali ambayo kwao sasa ni mzigo mzito usio na faida yoyote. Maendeleo gani wategemee kuletewa na viongozi kama hawa?

Baba Bashiru Ally nawe malango yako yabarikiwe. Wakati wa kuwapeleka kozi viongozi hawa kama ulivyolitangazia Taifa, NI SASA!