Ndugu Rais, Yusufu Makamba alipokuwa anahutubia Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma aliwaambia Watanzania kuwa, “Jakaya Mrisho Kikwete aliwabatiza kwa maji, lakini huyu (wewe baba), atawabatiza kwa moto!”
Wanasema Bunge lililipuka kwa kushangilia wakati Rais mstaafu Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete alipoingia bungeni akiambatana na mwanaye. Wabunge wote, mawaziri wako wote pamoja na Waziri Mkuu wako, walisimama wakamshangilia! Hakika huu ulikuwa ujumbe mzito kwako! Baba, jitathimini!
Baba niliwahi kusimulia aina mbili ya vicheko vya marehemu mama yangu.
Alikuwa akicheka kicheko, kama unamsikia tu humwoni ungedhani anacheka. Lakini alipocheka kicheko kama hicho, kama unamwona ungejua kuwa huyu hacheki. Ana uchungu mkali katika kifua chake kinachomfanya atoe sauti iliyofanana na kicheko na kumbe alikuwa akilia kilio kisichokuwa na machozi! Hili Baba lisikudhoofishe!
Wabunge wangapi wenye hofu ya Mungu wangeweza kushangilia Kikwete na mwanaye wakimshuhudia mkewe akiapa kuwa mwakilishi wa wananchi huku akiwa hana hata mwananchi mmoja anayemwakilisha? Uwepo wake bungeni kama walivyo wengine wa kuteuliwa ambao hawakupewa uwaziri au Unaibu Spika, tena yeye akiwa na walinzi na wasaidizi wengine ni mzigo wa hasara tupu! Bwana Yesu aliposema aliyenacho ataongezewa na asiye nacho kama masikini wa nchi hii alivyo, hata kile kidogo alichonacho atanyang’anywa, alisema kweli! Wawakilishi wa wananchi washangilie kuona wananchi wao wanaongezewa mzigo usio na faida yoyote kwao?
Ndugu Rais, Ndugu Kikwete alipoingia katika urais uliwaambia wananchi wote, huku dunia ikisikia kuwa Mzee Mkapa alimwachia uchumi nyumbulifu kwa maana ya fedha za kutosha. Ulipoingia si uliitangazia dunia kuwa amekuachia nchi ambayo kila ulipogusa palikuwa ni jipu! Timamu gani amshangilie! Wewe na Waziri Mkuu katika kuwahangaikia watu wako, mmekwenda kutumbua majipu makubwa ya kutisha kule bandarini mara ngapi? Madudu ya TRA yalikuwa yanalindwa na nani kama si uongozi wake? Haya ni ya kumshangilia?
Je, siyo Rais Kikwete aliyesimama hadharani tena bila aibu kabisa akasema zile fedha za ESCROW ziliibwa kwa sababu wezi hawakumwona mwenyewe? Alipolizindua Bunge la Katiba hotuba yake si ndiyo iliyouvuruga mchakato wote wa kupata katiba mpya kwa kuyafanya maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Ndugu Warioba yaonekane ni upuuzi? Leo kuna matumaini gani ya kupata katiba mpya? Wakati Ndugu Warioba anakabwa na vijana wa kihuni alipokuwa anatetea maoni ya wananchi Rais wa nchi alikuwa nani? Aliwachukulia hatua gani wahuni wale? Baba, nani wa kumshangilia huyu?
Ndugu Rais wa kumshangilia Ndugu Kikwete ni wale wale waliokuwa wanamsusia Bunge na kutoka nje kila alipoingia? Ni wale wale waliokuwa wanalalama kuwa Kikwete alitumia muda wake mrefu wa urais kushinda kwenye mahoteli ya kifahari ya Wazungu huko Ulaya kwa fedha iliyotokana na kodi ya masikini na wanyonge wa nchi hii? Ni wale wale waliosema aliwaleta wageni wa kuipora nchi hii ambao sasa wanakufanya baba uhangaike usiku na mchana uokoe japo kidogo kilichoko katika mchanga?
Ndugu Nape akisema tunaku-miss, inaeleweka, lakini Henche kusema aliwapa uhuru wa kufanya mikutano na Bunge lilikuwa linaonekana ‘live’ amepotoka. Uhuru huo umetolewa na katiba ya nchi hii siyo na Rais yeyote. Na kama kuna Rais ameufuta uhuru huo mwambieni bila kumuonea aibu kuwa anavunja katiba ya nchi aliyoapa kuilinda! Kiongozi aliyepata madaraka kwa njia halali, mamlaka yake inatoka kwa Mungu mwenyewe! Nanyi mtamtambua kwa namna anavyowasikiliza watu wa Mungu aliopewa kuwaongoza!
Lakini mwanamwema aliposema malipo ya wabunge yalikuwa hayacheleweshwi nikakumbuka kuwa ni wakati wa Kikwete (kabla hujawa baba) ukiwa mbunge na waziri, Bunge liliamuru wastaafu wote waongezewe pensheni kwa Sh 50,000 ili ifike Sh 100,000 moja kwa mwezi. Wengine wamekwisha ongezewa! Baba unamaliza mwaka wa pili umeshindwa kutuongezea Sh 50,000 tu wastaafu wa TTCL? Kununua ndege ni jambo jema sana, lakini baba wastaafu tunapukutika kwa kushindwa kununua hata panado tu!
Kumbuka fedha hizo za kununuliwa ndege hazikuridhiwa na Bunge! Iweje usitukumbuke wastaafu wa TTCL kwa hamsini elfu yetu? Ah! Aggrey Mwanri ungekuwako, wazee tungevuta japo kwa siku chache! Lakini kwa hawa ni ngumu kuiona kesho yetu!
Ndugu Rais, wanaposema Serikali kuingilia mihimili mingine kiasi cha kuwafanya hata baadhi ya viongozi wa kamati za Bunge wasuse nyadhifa zao ndiko kunakoonesha kuwa walikuwa hawamshangilii mtu! Walikenyua meno yao tu, wakapigapiga meza huku wakitoa ukelele uliotafsiriwa kuwa ni kumshangilia. Ashangiliwe kwa lipi! Walikuwa wanalia kilio kisichokuwa na machozi! Ila hapa ndipo baba ulipowafikisha viongozi wenzako! Wanaonekana kama watoto!
Ndugu Rais umetumia hekima kubwa kuamuru kijana Emmanuel na wimbo wake waachiwe huru kwa sababu hukuona maadili yaliyovunjwa! Sasa anasema anaambiwa kuna watu wanamfanyia kazi wampotezee maisha!
Watishi wake ndiyo wale wale wanaojiita maprinsi.
Baba hebu kwa pamoja tumtangulize Muumba wetu, tuyatafakari baadhi ya mashairi ya huyu kijana wetu kwa pamoja! Anasema, “Unachokipanda leo ndicho utakachovuna kesho! Imeandikwa mwanaume kula kwa jasho, najiuliza hivi ni nani kaiona kesho? Chapa mwendo na ukilala hauna chako. Hivi uhuru wa kuongea kwenye nchi hii bado upo? Usije ukaongea vitu kesho ukajikuta uko sentro!
Kiongozi mwenye busara anapokea ushauri. Anapokea mawazo haweki mbele kiburi. Hey! Samahani mheshimiwa hivi unamjua Bashite? Hili ni jipu jipya kutoka Koromije. Limeisha iva, usaha limeisha tunga. Nakukabidhi sindano kulidunga. We si dokta wa majipu, tumbua hakuna kuvunga. Kuvamia ofisi za watu kumbe nayo ni kazi. Hakuna noma wanangu pigeni kazi…Hahahaha! Wewe mtu gani sasa hutaki kushauriwa, hutaki kukosolewa…umerogwa wewe…unajiona ndugu yake na Yesu ee… Oya wanangu eeeh! Round hii mtanyooka haki ya Mungu. Naona kichaa kapewa rungu.”
Anauliza, “Hivi uhuru wa kuongea kwenye nchi hii bado upo? Usije ukaongea vitu kesho ukajikuta uko sentro! Na kweli ameongea vitu kesho yake akajikuta yuko sentro. Anaposema kiongozi mwenye busara hupokea ushauri ni kweli kwani mpaka Yesu anapaa mbinguni, hakusema amemwacha ndugu yake yeyote hapa duniani!