Ndugu Rais, waaminio katika juzuu wanasema chapisha au potea. Najua iko siku sitakuwapo katika ulimwengu huu wa mateso kwa sababu sote tunapita tu hapa duniani.

Sijui Mwenyezi Mungu ametupangia siku ngapi za kuishi, mimi na wengine. Lakini tuzikumbuke siku za ujana wetu ili tumtukuze Mungu.

Ndugu Rais, Mwenyezi Mungu ametuumba na masikio mawili lakini mdomo mmoja tu, makusudio yake ilikuwa tusikie zaidi kuliko tunavyosema. Washauri wetu wote ni wanawema ila ni binadamu kama tulivyo sisi.

Wanaipenda zaidi kazi yao kuliko wanavyokupenda wewe. Pata mshauri ambaye hutamlipa mshahara. Huyo atakushauri ya kweli bila kuogopa kupoteza kazi yake.

Unapita mitaani huku unaitwa Mwalimu, kule unaitwa Mwalimu Mkuu. Unauliza kunani; wanakwambia huyu atakamatwa sasa hivi. Kakosa nini?

Anasema ‘vyuma vimekaza’ wakati umekataza! Unamkumbuka Kambarage! Ndiye Mwalimu Nyerere aliyesema, “Ikulu ni mahali patakatifu…” Ikulu aliyoisema Julius siyo ule mjengo peke yake.

Ni hadhi ya yule aliyekabidhiwa Ikulu, ule mjengo ukiwamo. Popote anapokuwa Rais ni Ikulu. Sijakusikia ukisema vyuma havijakaza wala sijakusikia ukiagiza wanaoona ‘vyuma vimekaza’ wakamatwe.

Baba, haya ni maneno ya huku kwetu Mbagala mbagala. Hayastahili kusikika kutokea Ikulu!

Hujasikia wakisema wapambe wana nguvu kuliko mwenye mali? Walisema ni bora ukutane na Idi Amini mwenyewe kuliko kukutana na Maliyamungu. Watu wasiojulikana ndiyo Grace wetu!

Ndugu Rais, najivuna kusema nimezaliwa kijijini. Kijiji cha zamani. Kijiji ambacho hatukujua maana ya hospitali, zahanati, muuguzi, mkunga sembuse kuwa na simu! Iwe ya kitini, mezani au ya mkononi!

Naona ufahari kuwa sijapoteza asili yangu. Katika familia yangu salamu ni mwakata, mwalinda au mwaomba. Na kila inapotolewa goti lazima lipinde.

Ndugu Rais, nakiri kuwa mlevi aliyelewa kisawasawa huwa hajijui kuwa amelewa. Lakini kesho yake anaposimuliwa vituko alivyovifanya jana yake, mwenye busara hukiri kuwa alikuwa amelewa.

Basi na iwe hivyo kwangu! Baba, mimi huwa naandika lakini sijawahi kujua kama naandika sawasawa. Bado nakumbuka vema baba ulivyokuwa unayakubali maandiko yangu wakati wa uwaziri wako. Na hasa siku ile uliyoamua kunipungia mikono yako yote miwili ukiwa ndani ya gari lako.

Nayakumbuka maneno ya mtumishi wa Mungu, Sheikh wetu maarufu, aliyeniambia kuwa ni kalamu yangu tu ndiyo iliyobaki, inaiambia Serikali ukweli baada ya Kambarage kututoka!

Sijausahau ujumbe wa Mtumishi wa Mungu, Mzee wa Upako, aliniandikia akisema “maandiko yako yana upako”.

Mtumishi wa Mungu, Baba Matumaini, aliniambia, “Maandiko yako yanakuwa kama nyaraka alizokuwa akiandika mtume Paulo, leo kwa Wathesalonike, kesho kwa Wakolosai na wengineo.”

Mwanamwema aliniandikia kuwa maandiko yako yakijasomwa baada ya miaka 20 watajua kuwa alikuwapo nabii, lakini waliokuwa naye hawakumtambua!

Ndugu Rais, niliisikiliza vizuri hotuba yako ulipokuwa unapokea ripoti ya makinikia. Baba, yote yale uliyoyasema yameandikwa vema katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu.

Maandiko hayo yaliandikwa mwaka 2003. Baada ya miaka kumi na minne kupita, baba leo umetokeza na kuyasema.

Ndugu Rais, umesema kampuni ya mawasiliano ya Airtel ni mali ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Sasa sijui nitaitwa mchochezi na hawa akina Grace wetu, lakini wamekunukuu ukisema, “Waziri wa Fedha hakikisha unafuatilia suala la Airtel. Kwa taarifa nilizonazo Airtel ni mali ya TTCL…”

Ukaendelea, “Kuna michezo michafu imefanyika. Sasa sitaki kuzungumza mengi, fuatilia hilo. Nchi ilikuwa na maajabu kweli.”

Ndugu Rais, umekuwa kama umetumwa na Mungu kuja kuyafichua haya kwa ajili ya ustawi wa watu wake.

Katika ukurasa wake wa 39 wa kitabu hichohicho cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “…ndugu yangu, dunia hii ya Mungu ni duara. Ni mviringo. Inazunguka. Tuliachana pale mimi nikiwa Meneja Mkuu wa Kampuni ya Simu.

Kampuni ya Serikali au ‘esiyu’ kama tulivyokuwa tumezoea kuiita. Kila mwaka tulitengeneza faida kubwa kuliko ya mwaka uliotangulia….Wakaamua kuyatoa kafara mashirika ya umma na viwanda. Mengine yaliuzwa, mengine yakakopeshwa, mengine wakasema ubia. Mengine kama langu, Kampuni ya Simu, yakafanyiwa mizengwe.

Haikujulikana mara moja kama limeuzwa, limekodishwa, limekopeshwa au namna gani. Waziri wetu wa kuwasiliana na viongozi wenzake, walituambia kuwa ametokea mwekezaji mwenye madola ya kumwaga.

Ilisemekana kuwa pamoja na kwamba bei ya kuinunua kampuni hiyo alipangia mnunuzi mwenyewe, bado alikubaliwa alipe kwa awamu mbili.

Haikueleweka aliwafanyia nini hao viongozi wetu, lakini amini usiamini, kampuni yetu ya simu aliuziwa huyo mwekezaji kwa kulipia kiduchu tu!

Tulibaki tunasikia tu mitaani kuwa Waziri wetu wakuwasiliana, kafanyiwa hivi, mara alipewa hiki na yule jamaa na maneno mengi ambayo sisi kwa unyonge wetu hatukuweza kuyathibitisha, lakini tuliyasikia.”

Ndugu Rais, nikiyazingatia yote haya na kuona unayoyafanya, najikuta nashindwa kuukabili mbinyo wa wanawema wanaonitaka niandike kitabu kuhusu maisha yangu.

Niliingia Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 1975 nikitokea Ntungamo nilikokuwa nasomea masomo yangu ya filosofia.

Kijijini nilikozaliwa tulijua Dar es Salaam kuna watu wawili tu mashuhuri. Julius Nyerere ambaye kutokana na lugha yetu kukosa herufi ‘R’ tulimwita ‘Nyelele’ na Sheikh Yahya Hussein.

Hivyo, nilipofika Dar es Salaam kitu cha kwanza ilikuwa ni kumuishi Nyerere mpaka alipokwenda kaburini.

Kifikra, Nyerere amenilea ingawa mwenyewe hakujua. Mwaka huohuo (1975) nilikwenda kwa Sheikh Yahya kumtaka anitabirie kuhusu maisha yangu ya baadaye. Kwetu tulidhani Sheikh ni jina la mtu.

Alinitabiria mambo matatu. Mawili yalitimia kama alivyonitabiria na kwa wakati aliosema. La tatu aliniambia litanitokea baada ya kufikisha miaka 50 na kuendelea. Kwa kuwa nilikuwa kijana, miaka 50 niliona ni mbali sana hivyo sikulifuatilia hilo.

Aliniambia baada ya kufikisha umri huo na kuendelea, watu mashuhuri, wenye hekima kubwa na busara nyingi watakuwa wanakuja kwangu kuniomba ushauri!

Ndugu Rais, nitaandika kitabu: MAISHA YANGU NA BAADA YA MIAKA HAMSINI.