Ndugu Rais, alianza waziri akasema ameshangaa kuona baadhi ya Watanzania wakishangilia kuzuiwa kwa ndege ya ATCL nchini Afrika Kusini. Hajawahi kuona sherehe msibani. Ashibae hamjui mwenye njaa – lazima ashangae.

Inapotokea hata Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally, naye ameshangazwa na kitendo cha baadhi ya Watanzania kufurahia kukamatwa ndege ya serikali inayotumiwa na ATCL, hapo lipo tatizo.

Hakuishia hapo, akaongeza kuwa alitamani wananchi eti wao ndio wachukue hatua kushinikiza kuachiwa kwa ndege hiyo hata kwa kufanya maandamano! Hatuwezi kumpuuza huyu kwa sababu wengine bado tuna imani kubwa sana na yeye.

Lakini kuwataka wananchi wao ndio waikwamue ndege ni kuchochea ghasia katika nchi. Kiongozi makini hawezi kuwa na fikra mufilisi kama hizo. Sheria za nchi na za kimataifa zipo. Na vyombo vinavyosimamia sheria hizo vipo. Yawezekana tumepewa jukumu la kuiongoza Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tukiwa njiti, yaani kabla hatujakomaa. Kuwa Mwenyekiti wa SADC unapaswa kufahamu kuwa Tanzania ina mkataba na Afrika Kusini, kama mwanachama wa jumuiya hiyo, wa kutekeleza hukumu za mahakama za nchi wanachama.

Afrika Kusini inawajibika chini ya mkataba huo kutekeleza hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyosajiliwa kwenye mahakama za Afrika Kusini. Hivyo, kuwachochea vijana wasio na uelewa huu, hasa unaweza kuwafanya wakadhani kushinikiza hasa hasa ni kuuchoma ubalozi wenyewe na mali zake zote moto. Hawajui kuwa kwa wenzetu kuna utawala wa sheria. Serikali zao zinaheshimu sheria za nchi.

Lakini alijua kuwa pale alipokuwa anasemea ni Ubungo? Wako wananchi waliokuwa wanamsikiliza ambao walikuwa na nyumba zao wenyewe nzuri zenye hadhi, lakini leo wako vibambazani wakilia vigaeni baada ya serikali kuwavunjia nyumba kupisha upanuzi wa barabara na kukataa kuwalipa fidia.

Hajawaamsha hawa kuwa kumbe nao wakienda kusajili hukumu yao kwenye mahakama za Afrika Kusini watalipwa madai yao? Unawahakikishia wananchi kuwa katika hili atakayeanzisha vita atashindwa, baba Bashiru kasome maandiko katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Imeandikwa: “Ndugu Rais, ujuzi ni mwalimu mzuri kuliko elimu. Ushindi wa nguvu hauwezi kuisuluhisha mioyo ya wananchi, bali utazidi kuivimbisha na kutafuta kisasi. Vita yoyote ni mbaya kwa aliyeshindwa, maana hupata hasara kubwa. Pia vita yoyote ni mbaya kwa anayeshinda, maana huandamwa na kisasi siku zote za maisha yake.”  Ushindi wa magomvi na ubabe muungwana hajivunii hata siku moja. Ingeonekana ni busara kubwa kwa mkubwa kulikemea hili.

Kuna kumbukumbu nyingi za ununuzi wa ndege katika nchi hii. Alitokea Waziri wa Fedha akasema ni afadhali wananchi wale majani, lakini ndege ya rais lazima inunuliwe! Ndege ilinunuliwa. Alipokwisha kupita alihukumiwa. Akawa anafagiafagia barabarani kule Sinza kama hukumu yake ilivyoandikwa. Leo habari zake na ndege zake hakuna anayejua.

Imeandikwa: “Tatizo la madaraka makubwa yakiambatana na mali nyingi mikononi mwa watu walio wengi, hasa wasio na busara, huzaa kiburi. Ndiyo maana utashangaa kuona watu waliopokea utawala wa nchi hii kwa ridhaa au kwa udanganyifu kutoka kwa waasisi, wamejijengea imani potofu, kama waliyokuwa nayo wakoloni kwamba magereza, bunduki, vifaru na mizinga vinaweza kufuta au kuzima nguvu za wananchi, hivyo kuwafanya watawale milele.”

Baba Rais wangu, kama kuna wananchi imewalazimu kula majani ili kuwezesha ununuzi wa ndege hizi, mimi sijui. Lakini naona wagonjwa wakiandikiwa dawa wakanunue kwa sababu dawa hazipo katika hospitali zetu. Watoto wao wanasoma kwa kugeuziana migongo, madarasa matatu katika chumba kimoja wakifundishwa na walimu watatu. Iko haja baba kukaa mezani tukubaliane maana moja ya neno maendeleo. Waje wanaosema ndege na treni ya kisasa ni maendeleo na wanaosema maendeleo ni ustawi wa watu, kuondoa ujinga, maradhi na umaskini kwa watu wetu!

Tunakuwa na maumivu makali moyoni kila tunapolazimika kuurudia mara kadhaa wosia aliotuachia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lakini hatuna namna nyingine. Tutaurudia na kuurudia mpaka hapo utakapokuwa umeenea katika vifua vya watu wake wote ili wajue kuwa hakuna wa kuwakomboa, bali mkombozi wao wa kweli ni wao wenyewe. Haya ya watu wasiojulikana ni utimilifu wa laana ya Baba wa Taifa. Wakataeni wote wenye uhusiano nao.

Tuliobahatika kumwona na kumsikia mwenyewe siku alipokuwa akiwosia, tunalazimika kuwaeleza wengine ambao hawakuwapo siku hiyo nini kilijiri. Tusipofanya hivyo tutakuwa hatuwatendei haki maskini wa nchi hii ambao walipewa Julius Kambarage Nyerere bila wao wenyewe kujua nani aliyewapa.

Kwa hilo tutaulizwa na ikilazimu tutahukumiwa kwalo. Baba, na mimi Mwalimu alinialika nyumbani kwake Msasani. Alisimama chini ya mkungu kwa hisia kali akamnyoshea mkono Ndugu Paul, aliwosia: “Paolo, Paolo, Paolo’’, akamkazia macho Edward Lowassa, akamwita: “Na nyinyi wengine, mkilitupa kabisa kabisa Azimio la Arusha, mtakuja kupata tabu sana baadaye!’’

Leo viongozi wa wananchi wanasema hawawajui watu wasiojulikana. Lakini kama ni kweli hawawajui na wamejitahidi kuwajua wameshindwa, kwanini bado wanakalia ofisi ambazo zinapaswa kukaliwa na wenye uwezo wa kuhakikisha usalama wa wananchi?

Kwa ukatili wa watu wasiojulikana kupitia Bunge la Ulaya, dunia imetuhukumu na sasa tuangalie ulimwengu usitutenge! Tumetangazwa duniani kuwa Tanzania haifai kabisa kwa uwekezaji, biashara hata kwa utalii.

Wanasema siku ilipotangazwa watalii zaidi ya mia moja walifuta safari zao. Sisi tunapanga kuongeza ndege nyingine tatu. Shirika limeishatiwa nuksi. Nani atapanda ndege zinazoweza kukamatwa wakati wowote? Tukubali, asiyetaka maridhiano sasa hatufai, tumkatae.

Tusione aibu kufikiri mara mbili.