Ndugu Rais ulipoingia tu madarakani uliwaambia masikini na wanyonge wa nchi hii kuwa nchi yao hii ni tajiri sana, hata inaweza kuwa mfadhili wa kuzifadhili nchi masikini.

Lakini kwa uchungu ukasema nchi hii imeliwa vibaya mno kwa muda wa miaka yote kumi. Nakwamba, “Kila ninapogusa ni jipu!”  Ubarikiwe baba kwa kusema ukweli!

Kwa kuwa kwa miaka yote kumi masikini walikuwa wanaambiwa kuwa nchi yao ni masikini, kumbe huku viongozi na familia zao wakikusanya vyote vilivyotolewa kwa ajili ya wote na kuvifanya kuwa vyao peke yao, ukaonekana kama Nabii uliyetumwa na Mwenyezi Mungu kuja kuwang’atua watu wake kutoka katika makucha ya manyang’au! Na ulipojiapiza kwa kujiamini kuwa, “Walidhani nitakuwa pamoja nao!” Masikini na wanyonge wakabwaga moyo! Wakaulizana, “Ni huyu tuliyekuwa tunamsubiri au tumngojee mwingine?”

Mwanamwema Costantino kutoka Shinyanga akaniandikia akasema, “Waambie wewe ni sauti ya wasio na sauti (Sauti iliayo Jangwani-mtengenezeeni Bwana njia yake). Kama ni yeye ndiye tulikuwa tunamsubiri, basi atambue kuwa wewe ndiye mtangulizi wake! Naamini umeishatimiza wajibu wako.

Uwe na amani, wawe wanayasoma au la tayari umeishawasemea wasio na sauti. Mungu akubariki!”

Ndugu Rais, Taifa hili tangu lipate Uhuru limeongozwa na marais wengi wewe ukiwa watano. Katika wote waliokutangulia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete- Taifa halikuwahi kushuhudia mmoja wao akidhalilishwa na mwananchi au wananchi hadharani kiasi cha kufikishwa mahakamani! Iweje mambo haya yatokee wakati huu? Busara itumike ulitafakari kwa kina ili Taifa litoke hapa lilipo kwenye dimbwi la aibu!

Wako Watanzania waliokwishafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumdhalilisha Rais hadharani ikiwamo na kwenye mitandao. Jambo hili halikubaliki hata kidogo! Heshima ya Rais wetu lazima ilindwe na wananchi wote! Ni kweli baba, heshima ya mtu yeyote yule, haitoki kokote kule, bali kwake yeye mwenyewe. Kwa wananchi inaenda kudunda tu kama mpira unavyodunda ukutani baada ya kurushwa na kumrudia mrushaji!

Wananchi ni kama ukuta, heshima tunayowapa ndiyo hiyo hiyo wanayoturudishia. Ndiyo kusema kama lawama ni kwa mrushaji, siyo wanaomrudishia.

Ndugu Rais, wanadamu wengi tumeumbwa kuwa wepesi kuona yale tunayodhani ni udhaifu kwa wengine bila kwanza kujitathimini wenyewe. Baba ndani ya nyumba anapotahamaki na kugundua kuwa hana heshima tena hukimbilia kuwalaumu wanafamilia wengine. Hatazami yale anayoifanyia jamii.

Hotuba za Zanzibar zimewafarakanisha Wazanzibari badala ya kuwaunganisha.

Ambacho hakikuzingatiwa hapa ni ukweli kuwa baba unapokemea usisahau kuwa wanaokusikiliza ni wananchi wote. Elewa kuwa walengwa wako ni kakundi kadogo sana katika jumla ya Watanzania zaidi ya milioni 45. Mzee Joseph Butiku amesema usiseme sana. Ukisema huwezi kusaini ili kumwezesha mwananchi mgonjwa kupewa fedha zake kwa mujibu wa Katiba ili akatibiwe, kwa sababu tu alitofautiana na wewe katika kukushika mkono, unawapa sababu ya msingi wale wanaosema siyo kila mamlaka inatoka kwa Mungu. Watasema zipo zinazopatikana kwa hila!

Ndugu Rais, inaogopesha sana kwa aliyepatikana na hatia ya kumdhalilisha Rais wetu halafu hukumu inakuwa akatafute faini kisha ailipe kwa awamu, halafu wanatokea watu wanamchangia faini yenyewe!

Hii maana yake ni kwamba wale wote waliona alichokifanya mwenzao ni sawa sawa! Hapana, hii si sawa sawa! Wananchi kuonesha dhahiri chuki yao dhidi ya Rais wao, haikubaliki hata kidogo. Tutafakari; kuenenda kwetu huenda, siko!

Mwenye uwezo wa kuiweka sawa hali hii ni wewe baba peke yako. Hao viongozi wa dini achana nao. Kama wanaliona hili ni jambo muhimu kwa nini hawalizungumzii huko kwenye viwanja vyao?

Ndugu Rais, wanachofanya polisi ni kuzidisha hasira ndani ya mioyo ya wananchi dhidi yao wenyewe! Matokeo yake ndiyo haya tunayosikia sasa kuwa ndugu Nassoro anatuhumiwa na polisi kuwa baada ya kupata habari za kuuawa polisi wanne kule Mbande aliandika katika mtandao kuwa,

“Safi sana aisee. Naona wangekufa kama 20 hivi, halafu Simon Siro tumuulize mazoezi wanafanya kwa ajili ya wake zao?” Ole wake mtu yule awategemeaye polisi kwa maana anajiandalia visasi kwa mikono yake mwenyewe!

Naye Mtagwa anatuhumiwa na polisi kuandika katika mtandao kuwa, “JPM sijui anawaza nini…hata samahani hajui, au nilikosea hajui, nchi imefika hapa kwa sababu ya mtu mmoja aliyeamua…kujilipua…ajifunze kushindana kwa hoja si mtutu wa bunduki na mazoezi yasiyo na kichwa wala miguu ya polisi.”

Ndugu Rais, tukubali kuwa haya ni matokeo ya hasira kubwa iliyomo katika vifua vya wananchi. Wasiojua hasira ikizidi itatokea nini, wasome ukurasa wa 21 wa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu, imeandikwa, “Ni ishara ya hali yetu ya kawaida kama wanadamu kwamba pale hisia chafu zinapoleta ukatili juu yetu na juu ya dunia, hali ya ubinadamu hujitokeza na watu kuungana pamoja kusaidia kujenga upya. 

Hakuna nguvu yoyote duniani inayoweza kuishinda nguvu ya wananchi waliokata tamaa na kuamua kuwa sasa basi, liwalo na liwe! Nguvu ya wananchi wenye haki hushinda vita yoyote duniani.”

Baba wa Taifa katika urais wake wa miaka zaidi ya 23 kila aliyemwona kwa matendo yake na maisha yake, aliiona ile hofu ya uwepo wa Mungu iliyokuwamo ndani ya kifua chake. Leo anaitwa Mwenyeheri Julius Nyerere! Hofu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu inapaswa ikae ndani mwako! Uwe pamoja Naye! Mungu si wa kumtanguliza mbele!