Jaji Joseph WariobaNdugu Rais wiki iliyopita nilikuomba unijalie nimzike Wilson Kabwe! Katika mrejesho nimepokea simu nyingi na ujumbe mwingi wa kutia moyo. Pamoja na upungufu wote tulioumbwa nao kama wanadamu, lakini tunapoandika tunachagua maneno kwa sababu lengo letu kubwa ni kujenga, si kubomoa.

Tumeapa kuisema kweli ili kuilinda amani ya nchi yetu,

hata kama kwa kufanya hivyo kunaweza kuwafanya wengine watuchukie au watupende.

Hatuandiki hapa kwa kumpenda mtu wala hatuandiki hapa kwa kumchukia mtu! Ukweli unauma ila tutaendelea kuusema kwa sababu ni kweli peke yake ndio itasimama mpaka mwisho wa nyakati.

Marehemu Shaaban Robert alisema: “Kweli itashinda kesho kama leo haitoshi.”

Msomaji wa maandiko haya akiwa katika kutafuta kweli hatapata shida kuelewa kilichoandikwa. Kuku huchakurachakura ili avile vilivyo juu ya ardhi na vilivyofichwa chini ya udongo, lakini bata huishia kula vile tu vinavyoelea. Usomapo fanya kama kuku.

Ujumbe mmoja kutoka kwa mwanamwema ulisomeka, “Mwalimu Mkuu siku zote nakuelewa, lakini leo sijakuelewa. Unamtetea mtu muovu! Mwalimu unatetea ufisadi?” Kwa kuwa aliuliza kwa nia njema nikamwomba atulie kwanza. Nafsi yake itakapojiridhisha kuwa siwezi kutetea ufisadi asome tena polepole. Aliposoma akaniletea ujumbe uliosomeka: “Mwalimu Mkuu ubarikiwe sana kwa andiko la leo.”

Mwingine sijamjibu, naogopa kufanana naye. Kwa kuwa ujumbe wake ulikuwa mrefu sana siwezi kuuandika wote hapa, lakini sehemu nyingine Ulisomeka: “Hata Mobutu na Idi Amini walipofariki kuna watu waliwatetea…zaidi unaonyesha ulivyo na chuki binafsi na rika la vijana wachapakazi kama..(akataja jina)…huyo binti kutompa mkono….(akamtaja tena)….ni ujeuri wa kipumbavu ambao hakuna ujumbe wowote wa maana…”.

Sikuona nijibu nini maana kama binti angeulizwa naye akajibu: “Huo ujumbe ni ujeuri wa kipumbavu ambao hakuna ujumbe wowote wa maana…” sisi tutakaosoma tutaweza kuwatofautisha na kujua nani ndiye mpumbavu halisi!

Ndugu Rais, ujumbe kutoka kwa Mama Alex wa Malamba Mawili ulinifikirisha sana! Nilisita, Lakini nilipokumbuka kuwa wewe ni mcha Mungu naye ameandika kuegemea imani ya madhehebu yako, nimeuandika ili baba uusome!

Aliandika: “Enyi nyinyi mlioko mbele yetu mliojaliwa kusema, unganeni kwa pamoja mkamwone mkuu wetu, mkamwambie kuwa kipigo cha yule mzee ndicho kinaitafuna nchi hivi sasa. Kunyamaza kwake siyo kukubaliana.

Joseph Sinde Warioba alipigwa akitetea haki za watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Bwana wetu Yesu Kristu! Alirudishe Taifa katika maadili. Maandiko katika kitabu chake kitakatifu yanasema kuwa Mfalme Daudi alipolala na mke wa Uria, baada ya kuombewa msamaha, Mungu alisema nimemsamehe, lakini nitamuadhibu kwa kizazi chake. 

Haijalishi umetumwa au umejituma, kama umenyoosha mkono wako kumpiga mtu mzima, hiyo ni laana umeibeba. Wazee walipolala barabarani hatukutubu, ile ni laana juu ya nchi. Asipowasikia, ondokeni kwake.

Yakung’uteni mavumbi katika mavazi yenu! Kuyabeba maovu makuu yaliyofanyika wakati wa kizazi cha nyoka kilichomuasi Mwenyezi Mungu kwa kuipora nchi na watu wake, ni kuitafuta laana. Laana ya Mfalme

Daudi ilikuja baadaye kwenye kizazi chake. Kama waliweza kutumwa kumdhuru yule mzee aliyekuwa anatetea haki za masikini, kesho wale wale watamtuma kwake. Kipigo kile kitakitafuna mpaka kizazi kijacho.”

Ndugu Rais, kwanini makabila yote katika nchi yetu yalikuwa na matambiko? Ilipotokea mtoto kampiga mzazi wake au mzee yeyote, alisuswa na jamii nzima hadi alipojutia kosa lake akaomba radhi ndipo alipofanyiwa tambiko kumrudisha katika jamii. 

Anapotokea kijana amekosa adabu kwanini asifundishwe kuomba msamaha? Tunapomtuza tunawafundisha nini vijana wengine? Kuwa uhuni unalipa? Kwanini kutaka kujenga Taifa la wahuni? 

Ndugu Rais, matumaini ya masikini na wanyonge ni wewe! Walipokuja wakuja wakatwambia mila zetu zote ni ushenzi. Kwa ujinga wetu tukaziacha zote. Taifa lililokosa utamaduni wake lina tofauti gani na mtoto aliyeokotwa?

Ndugu Rais, kama ni ukimya umekuwa kimya sana kwa baadhi ya maeneo. Kati ya maeneo ambayo umekuwa kimya sana ni safari za nje na Katiba mpya. Angalau Rwanda ulienda, hata Uganda. Lakini Katiba mpya

hujatembelea hata siku moja hata kwa maneno tu! Baba bwana! Kama limekwisha vile! Lije jua, ije mvua, hili la Katiba mpya na bora halitakuja kwisha mpaka itakapopatikana.

Ndugu Rais, Katiba bora katika nchi yoyote ndio mzizi wa ustawi wa nchi na wananchi wake. Hitaji la Katiba bora ni mali ya wananchi. 

Ni kosa kwa chama chochote cha siasa kudhani kuwa kina jukumu la kusimamia mchakato wa kupatikana kwake. Katiba bora ni ile tu itakayopatikana kutokana na maoni ya wananchi wenyewe. Kwa sababu mpaka sasa hakuna mabishano wala malumbano yoyote kuonesha kuwa maoni aliyoyaleta Jaji Joseph Sinde Warioba hayakutoka kwa wananchi basi hayo ndio yawe msingi ambao juu yake yajengwe yote yatakayowezesha kupatikana kwa Katiba mpya iliyo bora.

Tulipungukiwa busara kuwaingiza wasiostahili na wenye maslahi binafsi katika Bunge Maalumu la Katiba. Uwakilishi uwe mpana, lakini ilikuwa ni kosa kuwaingiza Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wote ambao kwa nafasi zao walikuwa wameapa kuilinda na kuitetea Katiba iliyopo. Kushiriki kuunda Katiba nyingine ulikuwa ni usaliti kwa viapo vyao.

Wanaoshiriki lazima wawe ni wale ambao wataapa kutojihusisha na uongozi na hasa wa kisiasa angalau kwa miaka mitano tangu kuanza kutumika kwa katiba mpya.

Ndugu Rais, kufikishwa hapa ndipo unapolazimika kuchagua bega!

Imeandikwa kuwa huwezi kuwatumikia mabwana wawili. Au ubaki nao walioyapinga maoni ya wananchi aliyokuwa nayo Joseph Sinde Warioba au uungane na maoni ya masikini na wanyonge wa nchi hii aliyonayo Joseph Sinde Warioba. Elewa, Baba kuwa, lila na fila kamwe hazitangamani!