Ndugu Rais, kwa pamoja tujifunge unyenyekevu mbele za Mungu kwa sababu Mungu wetu huwapiga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema yake.

Tunyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari ili atukweze kwa wakati wake kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yetu.

Awamu ya tano imekuja na historia yake tofauti na awamu zote zilizoitangulia. Haikubweteka hata kidogo. Imejaribu kadri iwezavyo kugusa kila mahali kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo. Huku ni kuhangaika.

Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu akamuacha ahangaike mwenyewe. Kwa bahati mbaya sana baadhi yetu tumepoteza maana halisi ya neno ‘maendeleo’. Hata wenye midomo michafu nao leo wanasema wanataka kuwaletea wananchi maendeleo. Tuseme ukweli, awamu ya tano imeuanzisha upya msiba wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wakati wa Nyerere ilikuwa ni nadra sana kuona chozi likimdondoka Mtanzania kutokana na hali iliyosababishwa na Serikali.

Leo wanaosema ni utamaduni ndiyo wanaoifaidi nchi.

Kama ni kulia wanao baba wamelia sana. Kudhani machozi yanakauka kumbe si kweli. Machozi hayakauki. Ndiyo maana hata kabla msiba mmoja haujaisha ukitokea msiba mpya hutokea pamoja na machozi mapya. Na ukija watatu, watu watalia na machozi mengine mapya. Usiniulize kwanini; hivyo ndivyo alivyopanga Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe!

Wasiojulikana ni janga ambalo taifa lilikuwa halijapata kushuhudia.

Baba, umesema kweli kuwa Watanzania siyo wajinga sana. Wana uwezo wa ‘kuanalaizi’ mambo na kuchambua. Wanashuhudia nchi kama Marekani inavyopambana na ugaidi hadi kumuua Osama Bin Laden. Huyu alikuwa anaishi kwa kujificha nje ya Marekani. Leo Watanzania wanaambiwa ka-kikundi tu ambako kapo ndani ya nchi yetu eti Serikali imeshindwa kuwajua. Na haijui wanaishi wapi. Umesema sawa baba, “Watanzania siyo wajinga sana”. Tujiweke kwenye viatu vyao.

Wanatuanalaizi vipi? Wakati mwingine tunaangalia upande wetu tu.

Hatuangalii na upande wa watu wetu. Wanafikiri nini juu yetu kwa yote haya yanayotokea? Je, Serikali kukiri mbele ya wananchi wake kuwa imewashindwa watu hao wanaowateka, kuwatesa na kuwaua raia wake hakuwezi kuwasukuma baadhi wa raia kudhani kuwa huenda baadhi ya hao wasiojulikana ni sehemu ya baadhi ya viongozi wao? Kwanini tuwafikishe wananchi huko? Je, huko siyo kukiri udhaifu?

Haya mambo tulipaswa kukaa pamoja na kujadiliana kama ndugu.

Lakini baadhi yetu tumekuwa kama paka na panya. Siasa zina mwisho wake wanawema. Ona ni kama juzi tu tumetoka kwenye uchaguzi mkuu, lakini ni kama kesho tu tunaenda kwenye uchaguzi unaofuata. Ili kubaki madarakani matarajio yetu ni ridhaa ya wananchi au tunategemea maguvu tuliyo nayo? Kuitia nchi katika hofu halafu wakatokea wa kutokea wakasema tunajitayarishia utawala wa kudumu wanaweza kuwa wamekosea, lakini tukubali kuwa ni kwa matendo yetu na maneno yetu ndivyo vimewajaza fikra hizo! Kufikiria mpango wa kufia madarakani wapambe wetu siyo msaada kwetu. Hawa ni sawa na silaha zilivyo. Ukiielekeza mbele inapiga; nyuma inapiga. Akili kichwani mwako!

Jambo kubwa hapa wanawema ni kujiuliza kwa busara kabisa kuwa ni kwanini mpaka leo Watanzania bado wanamlilia Nyerere? Kuyafanya yale aliyoyafanya Nyerere mpaka leo hata Mtanzania mnyonge anamkumbuka sisi tunashindwa nini? Kwani kujenga reli na kununua ndege siyo mambo ya maendeleo? Au mpaka turushe roketi kwenda mwezini ndiyo tutoshe?

Maendeleo kwa akili ya Nyerere yalikuwa maendeleo ya watu, siyo vitu!

Alizingatia mapambano dhidi ya maadui watatu – ujinga, maradhi na umasikini- maadui ambao leo wanakuwa kama hawatuhusu vile! Na hivi ndivyo vipaumbele vya serikali yoyote ya watu.

Nyerere alipambana na ujinga kwani shule zake zilikwa na vyumba vya madarasa vya kutosha na madawati ya kuwatosha wanafunzi 45 kwa kila darasa na si zaidi.

Vitabu bora vilikuwapo na vifaa vya kufundishia na walimu wenye moyo walikuwapo. Leo wizara ya elimu utadhani ndiyo imeshikilia hirizi ya serikali isipotee!

Alikuwa mcha Mungu ambaye hakuwadanganya Watanzania kwa kuwalaghai kuwa alitoa elimu bure! Aliwatibia Watanzania wote wagonjwa kwa gharama ya kodi zao walizolipa bila malipo ya ziada. Toka mgonjwa wa kidole mpaka aliyehitaji kupasuliwa moyo.

Alijali sana ustawi wa jamii. Hivyo, maendeleo ya Nyerere ni yale yaliyowagusa Watanzania wengi moja kwa moja. Hakuna alipotamba kuwa yeye ni rais wa kikundi fulani. Alikuwa rais wa wote!

Majuzi nilipita na mkweche wangu Temeke! Karibu kila barabara nilikuta inajengwa. Siyo kwa kuwajali wana-Temeke. Kumbuka lile lilikuwa jimbo la CUF. Natamani uchaguzi mkuu ungekuwa unafanyika kila baada ya miaka mitatu; Temeke ingekuwa London ndogo! Leo  CUF kipande kimoja kiko mahakamani, kipande cha pili kinafanya uchaguzi mkuu. Lakini hii ni nchi moja inayoongozwa na kiongozi mkuu mmoja. Tusiwape nafasi wanaosema sisi ni watu wa kazi tu kama mashine ya kusaga, lakini hatustahili hata kidogo baadhi yetu kuwa viongozi wa watu!

Sasa tufanye nini? Baba watengenezee wanao jukwaa ambalo kwalo watakuwa wanakusanyika pamoja kuzungumzia masuala ya nchi yao ni si vyama vyao, dini zao, makabila yao au ukanda wao. Ni hapo tu ndipo patakapowapa faraja Watanzania katika nchi yao! Watakuwa wamoja tena na kamwe hautatokea mfarakano wa aina yoyote utakaoihusu nchi yao!

Walitokea wanawema wakakaa chini ya mwembe na kubuni jukwaa hilo kwa jina la Mwalimu Forum- MWAFO. Likasajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kaulimbiu ya jukwaa hili ni ‘Nchi Yangu Kwanza’. Mwenyewe nilikuletea makabrasha yake ukiwa waziri kwenye ofisi zako zilizokuwa Temeke.

Ni busara baba kuyaangalia makaratasi haya kwa umakini zaidi sasa kwani ukiyabariki utawarudishia Watanzania hali ya umoja, upendo na mshikamano aliowaasisia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye kwa hilo Watanzania wanaendelea kumlilia!