Ndugu Rais, wakati mwingine ninapoandika
moyo wangu hujaa simanzi
kuzidi uwezo wa kifua changu kuihimili.
Huacha kuandika na kwenda
ukutani ilipo picha tuliyopiga mimi na Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, nyumbani kwake
Msasani. Moyoni huiambia ile picha,
“Baba,
saa yako ilipofika ya kurudi kwa Muumba
wako ulituahidi kwenda kutuombea.
Waombee Watanzania sasa!”
Kama kuna kitu kinachousononesha moyo
wangu siku zote ni kukosa uwezo wa
kwenda kupaona mahali alipolala Baba wa
Taifa kule Butiama. Lakini amtegemeaye
Mungu hapungukiwi na kitu, kwakuwa
kwake hakuna lisilowezekana.
Ndugu Rais, maneno ya kichwa cha habari
si yangu. Yangekuwa yangu ningeuliza,
“Kwanini Mtanzania afe sababu ya
uchaguzi?” Hayo nimeyaazima kwa Raila
Odinga wa Kenya. Aliyatamka katika
mkutano waliouita,
‘The National Breakfast
Prayer’. Mkutano uliowakutanisha viongozi
wakuu wa vyama vya siasa wa nchini
Kenya kwa ajili ya maridhiano.
Wakiwa mbele ya wananchi walijutia kashfa
walizokuwa wakitoleana wakati wa kampeni
za uchaguzi mkuu. Wakaombana
msamaha. Kwa pamoja wakaahidi kuijenga
Kenya yao kwa ajili ya masilahi ya Wakenya
wote! Uhuru Kenyatta akijipangusa machozi
alimwita Odinga,
“ndugu yangu!”
Ni kweli Kenyatta ni Rais aliyeuonja
uchungu wa Mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu dhidi ya Binadamu (ICC). Kinga kwa
rais mwovu kwa dunia haipo. Alisimama
kizimbani pamoja na urais wake! Makamu
wake pia, William Ruto, aliijua nguvu ya
dunia kwa aliyefanya ukatili dhidi ya
binadamu wenzake.
Baada ya kuonja joto ya jiwe, Rais Uhuru
Kenyatta alianzisha vuguvugu la kuzitaka
nchi za Kiafrika zijitoe ICC. Akaungwa
mkono kwa nguvu kubwa na baadhi ya
marais kama Yoweri Museveni, Paul
Kagame na Pierre Nkurunziza.
Tuna marais saba wanaotuzunguka. Sijui ni
kwanini wengine wanatudhania hawa
watatu ni marafiki zetu zaidi. Mbunge
mmoja wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka
Kenya amewakemea vikali wabunge
wenzake akiwaambia kuwa mikutano mingi
wanayofanya haina tija kwa sababu
wanaongea mambo ambayo kidemokrasia
si ya msingi.
Mambo kama pasipoti na soko la pamoja
hayana umuhimu zaidi kama vile kulinda
utawala wa sheria katika nchi zetu,
kuhakikisha haki za binadamu katika nchi
zetu zinaheshimiwa kwa kuwa na utaratibu
wa pamoja.
Akatamba kuwa japo Kenya kidemokrasia
haijawa kamilifu, lakini wanajivunia kuwa na
demokrasia ya kweli. Bunge lao liko huru na
linaonekana kwa kila mwananchi. Hakuna
mpinzani anayewekwa ndani kwa kisingizio
cha kuwa eti anapinga maendeleo. Vyombo
vya habari vina uhuru mpana.
Wabunge na wananchi wako huru kutoa
mawazo yao bila kuogopa kukamatwa.
Hakuna mikutano ya wanasiasa inayozuiwa.
Alikuwa anaongea kwa Kiingereza.
Baadaye akabadili, akasema kwa Kiswahili:
“Nawaambieni, Mungu akitupatia maisha
huko mbele, tukawa na mamlaka ya
maamuzi katika nchi, hatutajali wewe ni
kiongozi wa nchi gani. Kama wewe ni
dikteta unayewafunga jela wapinzani wako
tutakutenga. Kama unanyanyasa vyombo
vya habari visifanye kazi zake kwa uhuru
hatutakuwa nawe. Kama unawafanya
wananchi wako wasiwe na uhuru wa
kusema na kutoa mawazo yao,
hatutashirikiana na wewe. Kama unapora
mali ya nchi, hatutakubali uwe pamoja na
sisi.
“Kama utakuwa ni kiongozi wa kiimla
unayezuia wanasiasa wasifanye mikutano
yao ya kisiasa, tutakueleza wazi bila
kukuficha kuwa hatutaki kushirikiana na
wewe. Tutakutenga! Na haya ndiyo mambo
ambayo sisi kama wabunge wa Bunge la
Afrika Mashariki tunapaswa kuyapa
kipaumbele.”
Sijui ni kwanini aliamua maneno haya
ayaseme kwa Kiswahili. Lakini Baba sisi si
ndio Waswahili zaidi katika Afrika
Mashariki? Alitaka ndiyo yatuingie vizuri?
Aliposema wao ni wamoja japo ni katika
siasa, iliniuma sana kwa sababu
alinikumbusha miaka 43 iliyopita, 1975, sisi
Watanzania ndiyo maneno yaleyale
tuliyokuwa tunawaambia Wakenya kuhusu
umoja wetu dhidi ya ukabila wao tulipokuwa
kule Mbagathi – Nairobi tukiwa wafanyakazi
wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ndugu Rais, wakati Rais Thabo Mbeki
alipolazimika kujiuzulu kwenye sherehe za
kumuapisha makamu wake, rais wetu
alihudhuria. Aliporudi nikaandika makala
kumwomba rais wetu baada ya safari hii ya
Afrika Kusini, amwahi mzee Nelson
Mandela kabla hajafumba macho,
amwombe aje atufanyie maridhiano watoto
wa rafiki yake marehemu Nyerere. Au
hakunisikia au hakunielewa.
Ndugu Rais, wewe ndiye baba yetu.
Fanyeni maridhiano kama Wakenya. Wewe
kama baba ndiye mwenye jukumu la
kuyafanikisha. Tambueni kuwa kati yenu
wote viongozi wetu wa kisiasa hakuna aliye
muhimu zaidi kuliko mama yetu Tanzania!
Ugomvi wenu hakuna atakayeibuka mshindi
bali wananchi wanaumia na wengi
wataangamia! Kwa hili wote mtahukumiwa
sawia!
Novemba 13, 2012, Mwenyekiti wa Chama
Cha Mapinduzi (wakati huo) Jakaya Kikwete
akifunga Mkutano wa Nane wa chama
chake alisema: “Sasa mnataka wakisema
Serikali ya CCM haijafanya kitu polisi
wawafuate? Au wakisema Kikwete nchi
imemshinda wawakamate? Kama
wakisema hatujafanya kitu ni kazi yenu
kusema kwamba tumefanya kitu.
Waonyesheni barabara, shule na mambo
mengine. Nataka mfahamu ndugu zangu
kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi
kufanikisha mambo yetu tutakwisha na
tutakwisha kweli?”
Sisemi CCM na Serikali yake inategemea
polisi kufanikisha mambo yake mpaka sasa,
lakini mwenye macho haambiwi tazama.
Ushindi wa CCM 2015 ulipatikana kutokana
na nguvu kubwa ya watu watatu. Kazi
kubwa iliyofanywa katika ujenzi wa
barabara. Hakuna wa kubisha, zilikuwa ni
jitihada binafsi za Waziri wetu wa Ujenzi,
John Magufuli, ambaye sasa ndiye Rais
wetu.
Na kazi kubwa iliyofanywa katika elimu na
hasa katika ujenzi wa shule za kata.
Hakuna wa kubisha, zilikuwa ni jitihada
binafsi za Waziri Mkuu wetu, Edward
Lowassa. Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana alipounganisha nguvu
za hawa wawili na kuizunguka nchi
kushindilia, ushindi ulipatikana.
Baba ninong’oneze mwanao, au na polisi
mliwategemea? Simjui aliyemuua Akwilina,
lakini ni polisi waliowathibitishia wananchi
kuwa Akwilina aliuawa kwa risasi
iliyofyatuliwa na bunduki. Wakawakamata
baadhi ya waliokuwa na bunduki ambao
wote walikuwa polisi. Wamewaachia bila
kuwaambia wananchi kama kuna mtu
tofauti na wale aliyekuwa na bunduki.
Wamewaacha wananchi wasemee tumboni.
Ogopa sana watu wanapoanza kusemea
tumboni. Baba, kwa nini Mtanzania afe kwa
sababu ya uchaguzi?
PASCHALLY MAYEGA
SIMU: 0713334239
Mwisho