Ndugu Rais, unyama unaofanywa na baadhi ya polisi katika nchi yetu unazidi kuongezeka kila uchao. Leo tunashuhudia unyama huu ukifanywa na polisi hawa au yule, kesho tunashuhudia unyama mkubwa zaidi.
Habari sasa ni polisi na unyama na unyama na polisi. Polisi wema katika jeshi letu la polisi wapo na hao ndio wengi zaidi. Polisi wenye roho za kinyama wapo, lakini ni wachache sana. Ila kwa kuwa unyama unauma zaidi
kuliko wema hawa wachache wanaonekana kuwafunika wema walio wengi. Na hawa ndiyo wanalichafua Jeshi la Polisi.
Kwa kuwa wananchi hawaambiwi au kuona hatua zinazochukuliwa dhidi ya hawa polisi wachache, basi kupitia Jeshi la Polisi wananchi wanasukumwa kuichukia Serikali yao.
Unyama uliofanywa Uwanja wa Taifa na polisi waliotakiwa wawe polisi wetu umetukumbusha nyuma sana. Umetukumbusha unyama tuliokuwa tunauona pale polisi wa kikaburu wakiwafanyia Waafrika weusi kule Afrika Kusini kabla ya kukoma kwa ubaguzi wa rangi. Kila tulipowaona wakiufanya unyama kama huu, tulibubujikwa machozi mengi! Iweje kwa awamu hii ya tano yale yageuke yawe ya kwetu? Kwa hili tumeinama, kama siyo wewe baba, atatoka wapi wa kutuinua? Hapana baba kwa hili toa
kauli. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “Tuchagulieni mtu atakayetuondolea
upumbavu huu katika nchi yetu.” Watanzania walimsikia? Kama walimsikia walimwelewa? Hapana! Hapana kwa hili baba kauli yako muhimu! Toa kauli watu wako wakusikie!
Mwanasheria Fatma Karume anasema, “Polisi hawana haki ya kupiga watu. Nimeiona video ile, yule mtu hakuwa na upinzani wowote kwa askari wale, lakini waliendelea kumpiga mateke ya kichwani na mbavuni.
Kilichonishtua ni kuona unyama mkubwa kama ule ukifanyika nchini mwetu!”
Unyama gani huu jamani! Wanawema tuukatae unyama huu katika nchi yetu. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alituasa
tumchague mtu atakayetuondolea mambo haya ya kipumbavu katika nchi yetu. Baba Rais usipotuondolea wewe mambo haya ambayo Mwalimu Nyerere anasema ni ya kipumbavu, wa kutuondolea atatoka wapi? Watanzania
wakutegemee wewe baba yao au wamtazamie mwingine? Kwa hili baba toa kauli yako masikini wa Mungu wakuelewe.
Nyerere aliwachukia polisi katili wale wa kikaburu si kwa sababu ya rangi ya ngozi yao, la hasha. Aliwachukia kwa unyama wao waliokuwa wanawafanyia Waafrika weusi ambao leo tunaushuhudia ukifanywa na
polisi wetu ndani ya nchi yetu. Kwa hili, wanawema tukatae tuseme hapana.
Mwathirika wa tukio hili mwandishi wa habari Silas Mbise wa Radio Wapo akisimulia, anasema; “Sitasahau siku ya Agosti 8 Uwanja wa Taifa, umesimama unapigwa, umekaa chini unapigwa, umelala unapigwa sasa sijui
walitaka nipigane nao, kisa hatutakiwi kuingia kwenye ‘press’ wakati tumevaa na kitambulisho, kwani mkiongea hamueleweki hadi mpige? Au kama kuna hatari ya usalama kuna onyo lolote mlitoa?”
Sheria za kijeshi ziko kwa ajili ya wanajeshi wake. Wawe polisi, mgambo au jeshi lolote. Kwa kutumia busara ya wakubwa, wakisharidhika kuwa askari ametenda kosa kinachofuata ni adhabu kwa askari husika. Kwa hili Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa anasema, “Tayari Jeshi la Polisi limefungua faili la uchunguzi kuhusiana na tukio hili ili kubaini ukweli na tayari askari waliokuwa zamu eneo la tukio wameanza kuchunguzwa ikiwemo wawili kuhojiwa”
Kamanda anabainisha kuwa kazi ya polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao na si kuwapiga raia waliotenda kosa ambao hawajakataa kutii sheria ya kukamatwa.
Weledi wa polisi wetu hautiliwi shaka, lakini
kuaminika kwao kwa wananchi kwa sasa ni shaka tupu.
Kamanda lazima akumbuke kuwa wananchi hawajasahau taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi kuhusu mbwa ambaye ilionekana kama vile alienda masomoni bila kuaga. Kilichowachanganya ni pale msemaji huyo alipodai kuwa mbwa aliyeenda masomoni alikuwa mwingine na siyo yule aliyekuwa
anatafutwa na mheshimiwa. Akasema yule aliyekuwa akitafutwa na mheshimiwa alikuwapo palepale bandarini siku ya tukio. Yawezekana ni kweli kuwa mbwa hakujua kama mheshimiwa alikuwa anamtafuta. Labda angejua angenyosha mkono kumwambia mheshimiwa kuwa niko hapa maana hawa siyo mbwa wa kawaida. Lakini ni ukweli kuwa polisi mbwa huwa hakai au kutembea peke yake hata siku moja. Siku zote anafungwa mshipi shingoni ambao daima unakuwa umeshikiliwa na polisi –mtu. Kama polisi-mbwa hakumsikia mheshimiwa kuwa anamtafuta, yawezekana vipi polisi-mtu aliyekuwa amemshika kwa mshipi naye hakumsikia mheshimiwa?
Na kwanini ilichukua muda mrefu hivyo mpaka kuja kuyasema hayo? Lazima wananchi watahisi kuwa uchunguzi ulikuwa ni wa kupikwa. Hali kama hii inapotokea ndiyo inayowasukuma wananchi kupuuza maneno kama ‘faili la uchunguzi limefunguliwa’. Kwao hayaleti maana yoyote zaidi ya kuwafanya
wapoteze imani kwa Jeshi la Polisi.
Akitoa maoni yake, wakili maarufu, Harold Sungusia anasema, “Kuna watu wengi wanapigwa na kuteswa, haki za binadamu zinavunjwa, lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Nchi inapitia kwenye tatizo kubwa la kutokuwapo kwa utawala wa sheria”. Habari zinazozagaa mitaani ni kwamba mwathirika tayari ameshafunguliwa faili huku kukiwa hakisikiki chochote kuhusu askari wale wanne wanaonekana kwenye video wakitekeleza unyama huo dhidi ya mwandishi wa habari Silas Mbise kutoka Radio Wapo aliyekuwa amelala kifudifudi chini, huku wakiwa na silaha na virungu, ambao walikuwa wakimpiga kwa vibao na mateke kichwani na mbavuni huku akiwa hana shati.
Hali hii lazima ikemewe na wenye mamlaka kwa sababu ikiachwa hivi hivi ndiyo
inayowasukuma wananchi kutokuwa na imani na Jeshi la Polisi na kuwafanya waichukie Serikali yao . Ni kweli Baba wa Taifa aliyekuwa
mstari wa mbele katika kukemea na kutaka unyama huu ukomeshwe huko Afrika Kusini amekwisha tutoka, lakini kweli hakutuachia mtu yeyote wa kukomesha unyama huu usifanyike nchini mwetu?
Polisi kutokubalika na jamii wasimtafute mchawi. Kwa matendo ya kinyama kama haya mchawi ni wao wenyewe!
.tamati…