Ndugu Rais, sasa siyo tena kwa kificho, ni jambo lililowazi kuwa matumaini yaliyorejewa sasa yanaanza kuyeyuka. Kadri siku zinavyozidi
kwenda ndivyo giza linavyozidi kuingia. Watu japo kwa kunong’ona wanaanza kuulizana; tulichodhani ndicho, ndicho?
Muhula wetu ni miaka mitano. Na huu mwaka ndiyo wa kwanza na bado tuko katikati. Ghafla matarajio yanayeyuka kama barafu iyeyukavyo mbele ya joto. Nini kimejiri? Bado hatujajua. Huku ni kuchoka, kuogopa au ndiyo kuchemka kama wasemavyo Waswahili. Kasi imepotea nayo haionekani tena. Ama kweli mvua za uhakika ni za masika; mvua za kiangazi zinaacha shaka nyingi.
Ndugu Rais, yameanza kusemwa maneno mengi. Hawa, ‘kadhibitiwa’, wale ilikuwa nguvu ya soda na maneno mengine mengi, lakini kubwa ni la yule
aliyesema nchi inapita katika mhemko wa muda. Hapa tulipofikia yatulazimu kukubali kusikiliza yanayosemwa na wengine, vinginevyo tutaachwa peke yetu.
Walioingia kwa kufuata mvumo wa “Hapa Kazi Tu”,
wataanza kugwaya. Watakapogundua kuwa kumbe mvumo ule ulikuwa ni wa upepo uvumao, watajitenga nasi. Ukiona upepo unavuma hata kama ni kwa kasi ya kutisha sana, jua kuna mahali ulianza na kuna mahali utakoma.
Mwanamwema Faustine kutoka Mwanza ameniandikia ujumbe akisema: “Mwalimu Mkuu nimekusoma! Nimekusikia tena kuwa uliwahi kumtaka JPM awe rais wetu! ‘(Nasikitika sana)’ Ila, Mungu alisikia ombi lako!
Kulalamika ni kumdhihaki Mungu! Kwani mlimtaka awe rais, afanye yapi..! Je, utakubaliana nami kuwa ipo tofauti kubwa kati ya ‘uchapakazi na kuamua kwa busara?’ Binafsi sikupendezwa…, lakini
ntafanyaje! Ngoja tukione!
“Mwalimu Mkuu nimekusoma wiki jana. Kwa ilivyokuwa, ilinifanya nikae kimya, lakini moyoni nikawa namshukuru Mungu kuruhusu wewe kuendelea kuwepo katika taifa hili! ‘Busara hainunuliwi!’ Hivi majeshi yetu ni imara kuliko ya Gadafi, Mubarack na Saddam? Je, rushwa, ufisadi, wizi na upuuzi katika awamu zilizopita vilishamiri kwa sababu ya wapinzani kuandamana na kufanya mikutano? Kweli amani hupatikana kwa vitisho?
Mungu amjalie maisha marefu F. Mbowe!”
Ndugu Rais, wahenga walisema akili ni nywele, kila mtu ana zake! Lakini mimi baba, pamoja na yote haya yanayozungumzwa bado niko na wewe! Bado
niko na wewe kutokana na lile neno ulilosema, “Watu waliofanya madudu katika utawala uliopita…hawatachomoka kwa kuwa nimejipanga
kuwashughulikia wote bila kujali uwezo wao wala vyeo vyao. Nawaomba Watanzania muendelee kuniombea”.
Naamini baba umejipanga. Kazi iliyoko mbele yako ni kubwa, lakini Watanzania wanaihitaji sasa. Mwingine wa kuifanya simwoni. Ndiyo maana
kwa unyenyekevu mkubwa nakwambia kwa neno lako hilo mimi nitatupa wavu. Siamini katika kushindwa kwako. Ni ukweli ulio wazi kuwa
Watanzania wengi wanajua kuwa wewe hukuwa chaguo la chama chako ila kilipotokea chakutokea ukajikuta umeteuliwa wewe.
Waliosema uliokota embe chini ya mpilipili wengi hawakuwacheka kwa upuuzi wa maneno yao. Ni maneno yaliyokuwa yanaelekeza kule ukweli uliko.
Watangaza nia katika chama chenu mlikuwa zaidi ya 40. Baadhi yao ni watu waliokuwa wamejitayarisha kwa muda mrefu sana. Baadhi yao walikuwa na nguvu nyingi sana tena ya vyote, watu na pesa. Baadhi ya wajumbe walisikika wakisema hadharani kuwa Mwenyekiti wako na familia yake na viongozi wengine wa juu wa chama chako walikuwa na wagombea wao. Bila kutokea uonevu, upendeleo na umamluki kwa baadhi ya watangaza nia, baba kati ya hao ungemshinda nani? Mungu kakunyoshea na
sasa wewe ndiye Rais wetu. Hivyo tunapokuambia tusikilize, tusikilize.
Unatarajia upewe ushauri gani kutoka kwa watu hao ambao kimsingi walikuwa washindani wako? Mshindani wako wa kweli angependa kuona
unashindwa toka siku ya kwanza. Na hapa sitabiri, lakini nakwambia ukiendelea kuwasikiliza hao ambao kama wangekuwa vyuma wangeitwa
chakavu, wewe ndiye mwisho wa utamaduni wa kumwachia Rais aliyeko madarakani muhula wa pili bila upinzani ndani ya chama chako.
Ndugu Rais, siku ile ulipotangazwa kuwa mgombea urais kupitia chama chako, ndiyo siku ile ile ugumu wa kazi ya urais kwako ulipoanza. Kuna wale waliokushangilia kwa machozi ya uchungu. Hao maumivu yao yangali mpaka leo.
Ukitaka kulithibitisha hilo tazama mikakati yao. Uliyempa mamlaka ya mazingira akaanzisha operesheni ya kinyama kabisa. Operesheni
bomoabomoa ili wananchi wakuchukie. Uliyempa habari kazi ya kwanza alizima televisheni bungeni ili wananchi wenye haki ya kutazama kile wanachofanya wawakilishi wao bungeni wakuchukie! Hata ulipokaribia kutumbua majipu yao wenyewe wakubwa ndipo zikaanza mbinu za kukupoteza kwenye lengo.
Wanasema busara hainunuliwi kwa kuwa hakuna inakouzwa. Kama nchi ina sheria madhubuti, ina vyombo madhubuti vya kusimamia sheria zisivunjwe kuna busara gani kuruhusu asiye na busara kuwazuia wananchi kutimiza haki yao ya kukutana na kujadiliana kama hawavunji sheria?
Kwa maoni yako baba, haya yote na mengine unadhani yanawafanya wananchi wakuoneje? Sifa iliyo njema ya kiongozi mwema, mcha Mungu ni
kupendwa na watu wake. Mwenyezi Mungu anamwongoza kiongozi anayemcha, kuwaongoza vema waja wake na siyo kuwatawala na kuwaibia.
Kama limetolewa wazo kuwa kiongozi wao aliyepita afikishwe mahakamani halafu mtoa wazo akashangiliwa na wote waliokuwa ukumbini wewe usiende katika ukumbi huo huo na kusema, “Nitamlinda.”
Wananchi wakiwaweka kwenye kundi moja, hapo alaumiwe nani? Kwanini usimpoze hata kwa simu
tu kuwa usiogope nipo? Hakuna makali anayoweza kukumbana nayo Rais wa nchi kama kuchukiwa na watu wake!
Ndugu Rais, haya yanapojiri na huku kasi uliyokuja nayo inafifia watu wako waliokuwa wamejawa na matumaini juu yako kuwa wamempata mkombozi wa kuwaokoa kutoka katika makucha ya manyang’au wakueleweje? Simamia kauli yako na mimi baba, kwa neno lako nitatupa wavu!