Ndugu Rais umewaita wafanyabiashara Ikulu tambua makundi mengine nayo yanasubiri uwaite. Uamuzi wako wa kutumbua papo kwa papo uliwajengea baadhi matumaini. Ninakuunga mkono. Lakini uliowabadilishia wana tofauti gani na uliowaondolea? Mojawapo lililomuondoa Mwigulu Nchemba si Lugumi Enterprises? Mbadala wake kafanya nini? Bungeni hakusema Rais mwongo. Lakini kama baba kasema nguo hazipo, yeye anasema hajawahi kuona mwongo kama wanaosema sare hazipo, maana yake nini? Baba, la Lugumi tuikubali aibu!
Ili lengo la kuwastawisha wafanyabiashara liwe endelevu, yakupasa ufanye mambo makuu mawili. Usipoyafanya tena sasa, watakaokuja kusema tulikuwa tunapuyanga tu, wataitwa wenye haki. Wafanyabiashara walifurahi. Mmoja akasema hakutarajia kukanyaga Ikulu katika maisha yake. Sasa amekanyaga na kuku kwa gharama ya masikini kala, muulizeni, amebadilika nini? Hakuelewa aliitiwa nini.
Baba ulichosikia kutoka kwa wafanyabiashara ni kwikwi tu baada ya kilio cha muda mrefu. Baba bwana! Wakati mwingine unanikumbusha marehemu mama yangu. Tukiwa watoto wadogo tukilia baada ya kuonewa, mama yangu alikuja na maneno ya kubembeleza. Atasema, ‘Ah! Nani? Kakupiga? Tema, tema mwanangu tumpige’. Tulipotema, hakupigwa mtu, lakini tulisikia tu, ‘pa’ yakaisha!
Nani hajawahi kusikia vilio vya wafanyabiashara? Baba bwana, akawawahi wafanyabiashara na kuwauliza, ‘’Ah! Nani kawapiga? TRA? Waziri wa Viwanda na Biashara? Temeni, temeni wanangu niwapige! Wafanyabiashara wakatema, hakupigwa mtu, lakini walisikia, tu ‘pa’, wakatoka Ikulu wanacheka. Baba akawaambia TRA hakuna nchi duniani inayoendeshwa bila kodi. Kusanyeni kodi. Halafu baba na wewe, haya maneno ya swela, kajinyonge na huko tutakutumbua yanaingia vipi hapa? Uliisha mtumbua achana naye!
Nakuungamia baba, sikumfahamu marehemu Wilson Kabwe. Lakini kovu aliloliacha katika mioyo ya watu wa Mungu halitakuja kukauka! Mpaka umauti unamkuta hakupata nafasi ya kujitetea! Na huyu naye baba, nakuapia, simfahamu. Lakini kushindwa kuendesha TRA kama tulivyotaka sisi, tusimhukumu kama kaua! Tumbuatumbua baba tulioifanya wakati wa mkutano na wafanyabiashara imetengeneza watu wengi sana ambao sasa hawana furaha na sisi. Wanatamani kipindi chetu kingeisha hata kesho.
Hakukuwa na ulazima wowote wa kuijenga chuki na watu hawa. Hata iweje, wao na wake zao, watoto wao, ndugu zao na jamaa zao na wengine wote walio wema, hawawezi tena kutuombea! Tumepoteza kundi kubwa la wapiga kura wa mwaka kesho! Upande mwingine tumewajengea wafanyakazi hofu kubwa. Mfanyakazi asiyekuwa na uhakika wa kesho yake hawezi kuzalisha ipasavyo. Akipata pa kupiga atapiga kisawasawa! Si anajua yuko kwa muda mfupi tu!
Baba wananchi walisikia neno ‘mheshimiwa’ likitamkwa na kila ulimi mpaka likawakifu! Neno mheshimiwa linathibitisha kukataa usawa kati ya wanadamu. Alisema Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi aliyepita Komredi Abdulrahman Kinana kuwa neno mheshimiwa linatumiwa na wenye tamaa ya utukufu! Ilikuja picha ya Mfalme na wajakazi wake. Lililetwa na wana mageuzi ambao hawakutarajia kuukwaa ubunge katika maisha yao. Watawala kwa tamaa pia wakalikubali. Kama neno mheshimiwa lenyewe lingekuwa na heshima hata kidogo tu, aliyeitwa angeonekana kama ka-mungu kadogo. Neno dhalilishi linalomdhalilisha zaidi anayeita kuliko anayeitwa! Nyerere anaheshimika mpaka leo kwa sababu hakunukia uheshimiwa. Miaka lukuki imepita tangu autoke ulimwengu huu, lakini Watanzania bado wanamlilia kama vile aliwatoka jana! Sababu ni moja tu na hakuna nyingine. Julius Kambarage Nyerere alikuwa ni mali ya wananchi! Hakujiona wa maana zaidi, akajiita ndugu. Watanzania wote wakamkubali kwa sababu nao walimuona ni kiongozi wao ndugu. Wakaitana ndugu tangu Rais mpaka mfagizi! Tazama Tanzania ilivyopendeza wakati wa Rais Nyerere, wananchi na viongozi wao walivyoishi vema kama ndugu!
Nani angemteka nani na nani angemtesa nani? Dhamira ya kutaka kuua na dhambi ya kuua vimeviziba pumzi vifua vya baadhi yetu! Tunaishi kwa hofu ya hukumu yetu ngumu ya kesho. Baba msikilize Katibu Mkuu wa chama chako ndugu Bashiru Ally ili ikikupendeza uwavue utukufu wa uheshimiwa waliojivika hawa watumishi wa wananchi, wasiostahili, wakakengeuka.
Mtumishi aliyeadilika hawezi kukubali kuitwa mheshimiwa mbele ya bwana wake. Bwana ni wananchi waliowaajiri. Hivyo la kwanza, wavue utukufu wanaokubali kuitwa waheshimiwa ili nawe uipate Tanzania iliyoadilika kama aliyokuwa nayo Rais Nyerere. Mheshimiwa siku zote ni mtu wa kutumikiwa. Anayewaambia wananchi kuwa ni mtumishi wao huku akikubali kuitwa mheshimiwa, huyo si mkweli! Kwa hili Kambarage, upumzike kwa amani Baba!
La pili muhimu, waliomuona Saddam Hussein akitembea mwenyewe kuelekea kwenye kitanzi ili anyongwe walidhani alikuwa anatembea kwa hiari yake. Hawakujua kuwa alikuwa amefungwa pingu za mwilini. Katibu Mkuu Bashiru Ally anajua kuwa maadili na miiko ya uongozi viliyokuwamo katika Azimio la Arusha vilikuwa ni pingu za mwilini kwa watumishi wa umma ambao hawakuwa waadilifu! Mzee wetu Job Lusinde alituambia kuwa, akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi walimpa kazi ya ujenzi wa barabara mkandarasi fulani. Bila kujua kuwa amekwishapata ile zabuni, mkandarasi alimpelekea fedha nyumbani kumhonga. Mzee Lusinde anasema sanduku lilipofunguliwa akaona fedha zimejaa mpaka juu. Akashtuka, akaruka, akasema, ‘Ah! Nitaziweka wapi pesa zote hizi?’
Fedha walizitaka, lakini waliziogopa kwa sababu hawakuwa na mahali pa kuziweka! Maadili na miiko ya uongozi ndani ya Azimio la Arusha viliondoa mahali pa kuweka fedha chafu! Baadhi ya watendaji wako hivi sasa baba, wananuka mali.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ameliambia Bunge kuwa dunia inaituhumu nchi yetu kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Na kwamba waliposhiriki katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa walizifafanua tuhuma hizo. Hakusema kama walikanusha na wala hakusema walizifafanuaje.
Kwa teknolojia ya sasa dunia inaweza ikakufungulia sauti ya kiongozi aliyefirisika kifikra inayosema tutakukatakata mpaka ukatike kabisa, ukakuta ni sauti ile ile ambayo baada ya Akwilina Akwilini kuuawa kwa kupigwa risasi iliyofyatuliwa ndani ya daladala iliyokuwa imejaza abiria ilisema, “Ndiyo, kwa sababu tuliambiwa wengine wataandamana kwa kutumia daladala’’. Utazikanushaje tuhuma hizo? Kuwafuga hawa na wanaonuka mali tunajikaanga kwa mafuta yetu wenyewe!