Ndugu Rais, Mwenyezi Mungu alipotuumba sisi wanadamu hakutuumba kwa bahati mbaya! Alikuwa na makusudi yake! Wala hakutuumba kwa ajili yetu, bali kwa utashi wake!

Kwa kuwa hakuna aliyeumbwa kwa bahati mbaya, basi kila aliyeumbwa, ameumbwa ili atimize kusudi la Muumba wake ambaye ndiye Mola wetu wote tunayemsujudia!

Wako wanaosema wanamtumikia Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu siyo mhitaji wa lolote, sembuse utumishi wetu! Lakini alitufundisha neno moja pale aliposema, lolote mtakalomfanyia yeyote kati ya hawa waja wangu, mtakuwa mmenifanyia mimi! Kumbe kuwatumikia wengine ndio kumtumikia Mwenyezi Mungu!

Kwa kutimiliza hilo, kila mmoja wetu amepewa nafasi yake ya kuwatumikia wengine. Wapo watumishi wa umma na wengine wa sekta zao binafsi. Wako na waliopewa utawala kama ulivyo wewe baba Rais wetu! Elewa kuwa umepewa nafasi hiyo si kwa ajili yako, bali ili utimize kusudi lake Mwenyezi Mungu la kukuleta hapa duniani. Utakuwa unamtumikia Mungu kama utawatumikia Watanzania wake wote bila kuwabagua. Ukiwa na mwelekeo wa kiitikadi au uchama jua shetani anakuongoza; acha kulitaja bure jina la Bwana Mungu wako!

Ndugu Rais, ukiona kazi ya urais inakuwa ngumu jua unaikosea! Usitafute mchawi. Kama vile ambavyo hakuna kazi ngumu duniani, vivyo hivyo hakuna kazi nyepesi zaidi ya urais! Wengi wangedhani kazi ngumu ingekuwa ni kupasua mawe. Lakini Mzee Nelson Mandela alisema:

“Mwanzoni kazi ya kupasua mawe gerezani ilionekana kuwa ngumu, lakini tulipoizoea tukaona ni sawa tu.” Ukiona kazi ya urais inakutoa jasho, tafakari na ujiulize, iweje kijana mdogo aweze kuliinua dege kubwa la mizigo hadi anga za juu kwa vidole tu?

Kioo cha kiongozi anayemtumikia Mungu ni kuridhika kwa waja wa Mwenyezi

Mungu. Kama wanaoshitakiwa mahakamani kwa kuukashfu uongozi wanaongezeka siku hadi siku hilo linapaswa kuwa funzo kwako.

Atawahamasisha wananchi wakapande miti nao wakihamasika, siku ya kupanda miti, miti ya kupanda haionekani. Kwa kujawa woga unatishwa hata na nyoka wa plastiki wa wapinzani! Wananchi wameitikia usafi kila wiki.

Matokeo yake uchafu umefukuliwa kule ulikokuwa na kuanikwa mabarabarani kwa kukosa magari ya kuuzoa. Uongozi wa kupapasa!

Ndugu Rais, kwa kuwa kila awaye yote ameletwa hapa duniani kutimiza kusudi la Muumba wake kwa kuwatumikia wengine, mtumishi mwadilifu anayewatumikia wengine hawezi kuwa mheshimiwa wao isipokuwa wale tu wanaoutukuza ubinadamu ambao kila mwanadamu alizaliwa nao! Hao wamejijengea kiburi vichwani mwao na kujiona wako juu ya wengine. Huo ndiyo ujinga alionao mwanadamu. Kuwa mnyenyekevu kwa wengine ndiyo kumtumikia Mungu.

Ndugu Rais, wanawema hawawezi kukejeli ununuzi wa ndege mbili mpya.

Kama ni Serikali au kama ni wewe mwenyewe umetimiza wajibu wako. Pale ambako mtu hana cha kumpongeza, kumpongeza kwa kutimiza wajibu wake ni sawa. Jasiri hujivunia pongezi kwa kile alichokibuni kutoka kichwani mwake kama Mwalimu Nyerere alivyobuni Azimio la Arusha.

Katika uzinduzi wa ndege hizo Baba, majigambo yako yaliwakatisha wengine tamaa! Mpango wa kununua ndege nyingine mbili kubwa zaidi ni jambo la maendeleo. Ulipojigamba kuwa mna fedha nyingi kiasi hata cha kuwapiga ‘tanchi’ matajiri wa dunia waliokwishatangulia kuagiza ndege hizo kulitutoa machozi wazee wastaafu wa TTCL ambao bado tunalipwa pensheni ya shilingi elfu hamsini kwa mwezi! Ulipotuchoma mkuki moyoni ni pale ulipotamba kwa kujiamini ukasema: “Fedha hizo zote, zipo!”

Yaani kumbe fedha unazo! Tunajiuliza, ‘kipi kianze?’ Unusuru maisha yetu au uongeze ‘mi-dege mingine miwili?’

Wastaafu wa TTCL pamoja na Bunge ambalo na wewe ulikuwamo, kuamua wastaafu walipwe pensheni ya shilingi laki moja kwa mwezi, bado mpaka leo wanalipwa pensheni shilingi elfu hamsini kwa mwezi. Ni zaidi ya mwaka sasa hawajaongezewa hata shilingi moja! Wanapokusikia Rais wao ukitamba kuwa “Fedha hizo zote, tunazo!” mioyo yao inanyong’onyea!

Baba, wahurumie wateswa wako! Waliokuwa na matumaini makubwa ulipokuwa waziri wanaanza kuona umebadilika.

Baba, nimefanya kazi tangu ikiwa East Africa Posts and Telecommunication mpaka ikawa TTCL, kwa miaka 20. Tangu kustaafu, huu ni mwaka wa 22. Nalipwa pensheni ya Sh 50,000 kwa mwezi.

Wanasema TTCL imefilisika! Kama umeamua kununua ma-dege, wastaafu wa TTCL hawawezi kukukejeli baba, bali wanaomba huruma yako kwa sababu wewe sasa, ndiye baba yetu!

Ndugu Rais, wananchi wametangaziwa kuwa MSD wameshindwa kupeleka dawa muhimu katika hospitali za Serikali kwa sababu Serikali imeshindwa kulipa fedha inazodaiwa. Wamejikunyata wanajiuliza kati ya ndege na dawa za kunusuru maisha yao, kipi kingeanza? Wanakumbuka wakati ule MSD ilipositisha kupeleka dawa katika hospitali za Serikali kwa kutolipwa. Wengi walipoteza wapendwa wao! Serikali ilisema haina fedha, lakini wakati huo huo manyang’au waliokuwa viongozi wetu walikuwa wanashinda wakielea angani na kukesha kwenye madanguro ya wazungu, Ulaya! Baba, kipi kianze!