Ndugu Rais, tunasoma katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu kuwa: “Wananchi wanataka rais awathamini raia waandamizi waliokamilisha wajibu wao na kustaafu katika ujenzi wa taifa ili wasipate shida katika wakati wao wa kutokuwa na nguvu za kuendelea kujikimu. Hivi sasa wastaafu wanaishi katika uchochole wa kutisha. Pensheni yao ni ya kijungujiko.”

Tukiwa katika uelewa huu, naona ni vema nikufikishie ujumbe niliotumiwa na wanao wakiniomba nikufikishie. Nauandika kama ulivyokuja: “Mwalimu Mkuu, pole na majukumu. Unajua wewe ndiye msemaji wetu. Tunakuomba utusaidie kupiga kelele hata viziwi wasikie.

“Wastaafu wa Polisi wa mwaka 2017 tupo wengi sana. Hadi sasa hatujalipwa pesa za mizigo. Ukistaafu hakuna kiongozi anayekujali. Hili nadhani rais wetu halijui. Mwalimu Mkuu kupitia uandishi wako mfanye rais wetu atambue hili, atusaidie. Ni P. Musese Mwesa.”

Baba huo ni ujumbe kutoka kwa wanao polisi wastaafu. Na nyinyi polisi wastaafu tambueni kuwa baba yenu ni msikivu. Kilio chenu amekisikia.

Nakumbuka baba ulilisemea hili kwa makini sana ulipozungumza na viongozi wa Polisi pale Ikulu. Kinachoonekana hapa ni kama vile watendaji wako wanakutegea kiasi kwamba ukishamaliza kusema wao wanaona yamekwisha.

Kwa umakini uliotumia kulisemea jambo hili haikutarajiwa uandikwe ujumbe kama huu kutoka kwa polisi hao wastaafu. Wamelazimika kuuandika ujumbe huu baada ya kuona hakuna kinachofanyika na wao wanazidikuteseka.

Baba lifuatilie mwenyewe jambo hili. Hawa ni polisi ambao Wamestaafu, ina maana ni wazee. Unyeti wa kazi walizokuwa wanafanya wote tunaujua. Wanaowafuatia kustaafu wanawaona watangulizi wao wanavyotaabika. Watapata wapi ari ya kufanya kazi kwa uadilifu ili waje wastaafu kwa amani? Tunawajengea taswira gani askari polisi vijana ambao bado wako kazini?

Wastaafu katika nchi hii wapo katika kila kijiji, katika kila wilaya, katika kila mkoa na katika nchi nzima. Nchi hii ipo hapa ilipo na amani ambayo sasa tunaichezea pamoja na sisi wenyewe ni kwa sababu ya hawa wazee wetu wastaafu.

Baba umesema mara nyingi kuwa nchi hii ni tajiri sana. Kwa mapesa mengi ambayo nchi hii imeonyesha kuwa inayo, imeshindikana nini kumlipa mstaafu angalau pensheni inayolingana na mshahara wa kima cha chini? Kwa nini sasa kutamba kuwa nchi hii ni tajiri sana?

Mangapi tumeyafanya kwa mapesa mengi ajabu! Wazee hawa wameandika: “Ukistaafu hakuna kiongozi anayekujali.’’ Wamekata tamaa!

Baba, baada ya kuwasemea wastaafu, tuseme neno japo kidogo kuhusu mada ya leo. Ni ukweli unaojulikana kuwa siasa ni taaluma. Wako wengi wanaotumia neno siasa wakidhani wanafanya siasa na kwa upofu wao wanajiita wanasiasa. Siasa inafanyika duniani kote. Tumemuona Vladimir Putin wa Urusi, leo anakuwa rais, kesho anakuwa waziri mkuu, na kesho tena anakuwa rais. Yako mengi yanafanyika kwa jina la siasa.

Lakini baba, tunapokuja katika siasa za Tanzania mambo ni tofauti kabisa.

Ni kwa sababu tu wanaofanya mambo haya ni watu wazima, hivyo inakuwa vigumu kuwapasulia usoni jina wanalostahili. Lakini ukweli lazima utuambie utoto ni nini na upuuzi ni nini. Utupatie tofauti ili wengine wasije wakadhani ni utoto na upuuzi na yanayofanywa kwa jina la siasa katika nchi yetu na watu wazima ni kitu kile kile kimoja.

Watanzania ambao hawana vyama vya siasa ni wengi kuliko Watanzania waliojiunga na vyama vya siasa katika ujumla wao. Amani ya nchi hii inapaswa kulindwa na wote wenye vyama na wasio na vyama. Wale ambao

hatuna vyama tunapaswa kusimama pamoja nyuma ya rais wetu kuhakikisha wenye vyama vya siasa hawatuharibii amani yetu.

Vyombo vya serikali akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa, baadhi ya mahakimu, lakini hasa Jeshi la Polisi na taasisi nyingine lazima watambue kuwa wao ndio wanaifanya serikali iwe jinsi ilivyo. Viko chini ya mkuu wa nchi ambaye ndiye mkuu wa serikali.

Hivyo kusema serikali ni rais, ni kusema vema kabisa. Chochote kinachofanywa na kimojawapo kati ya vyombo hivi, anayefanya ni rais mwenyewe, kiwe chema au kibaya.  Hivi ni vyombo ambavyo vinaweza kumfanya rais kuwa kipenzi cha watu wake au kuwa chukizo kwa wananchi wake.

Kuna chama cha siasa kiliazimia kufanya mkutano wao. Kimepata wanachama wengi wapya ghafla. Wametoka wapi, hilo si tatizo la mtu yeyote. Kamanda akauzuia. Sababu alizotoa ni kwamba walipata taarifa kuwa wafuasi wa chama kingine walipanga kuwafanyia vurugu.

Mimi si polisi, lakini kinaadhibiwa na kudhibitiwa vipi chama kinachotaka kufanyiwa vurugu na si kuwadhibiti wafuasi waliotaka kukifanyia chama kingine vurugu? Kumbe baba alikuwa na haki kunung’unika kamanda

kaonekana akinywa chai na mateka Mo, bila kutoa maelezo yoyote ya mkasa ule kwa wananchi wala kwa mkuu wa nchi.

Kamanda mueleze mwananchi timamu akuelewe, anapoamua kuchoma moto kadi yake ya Yanga, Simba au ya chama chake chochote anavunja sheria gani? Unapowaambia wanachama wawe watulivu huoni kwamba unathibitisha kuwa maneno ya baba kwako yaliingia yakapitiliza? Baba alisema: “Watanzania sasa si wajinga sana, wanafahamu na wanajua ‘ku-analaizi’ mambo.”  Hili walikwisha kulifahamu na wamekwisha ‘li-analaizi’. Kuwaambia wawe watulivu ni kuwadhalilisha. Ah! Kamanda, kweli! Baba alisema kuna mambosasa ya Dar

es Salaam ndiyo haya? Wananchi hawawezi kukubali baba yao apakwe matope kutokana na uchovu wa fikra wa baadhi ya viongozi wetu.

Hivi karibuni tumeshuhudia vurugu nyingi zinazotokana na vyama vya siasa. Chama kimoja kimepata nguvu ya ghafla. Kinapata wanachama wengi wapya. Wanatoka wapi si muhimu. Muhimu ni je, wanajiunga na chama

hicho kipya kwa uamuzi wao wenyewe?

Kama wamedhamiria kufanya hivyo kwa hiari yao wenyewe, kuwazuia si kuwatendea haki. Na wanaowazuia wajue wanafanya kazi ya bure, kwa kuwa hawatafanikiwa.

Watakachofanikisha ni kuleta vurugu katika nchi. Kamanda ajitathmini, asije akawa anapigwa pasi. Hivi kati yake na hao wanachama nani anapigwa pasi?