Ndugu Rais, imeandikwa; kitabu hiki cha Torati kisitoke mdomoni mwako mchana hata usiku. Nami kama Daudi nimetumwa uyatafakari maandiko tuandikayo kwa maana hayo yataifanikisha njia yako kwa kuwa yatakustawisha!

Ndugu Rais, kama si wewe baba, ni nani atawatoa jalalani watoto wa Ifakara? Maisha yao ni sawa na yale ya mifugo iliyotelekezwa. Chakula chao wanakipata jalalani baada ya kuchakurachakura kama wafanyavyo kuku wa kienyeji! Haya ndiyo maisha ya watoto wa taifa hili nchi nzima. Baba kama si wewe ni nani atawatoa huko?

Wanasema shule iko mbali sana. Alituambia baba yetu wa kiroho kuwa nyota zilizoko mbali sana, nawe huwezi kuzifikia kwa njia yoyote ile, hizo nyota kwako hazipo. Ndiyo kusema shule kwa watoto wa Ifakara, haipo! Kama si wewe baba nani atawatoa watoto wa nchi hii majalalani? Tumekalia ‘politiki’, siasa, tukidhani tunayoyafanya yanawaletea wananchi maendeleo. Lakini hayati Edward Moringe Sokoine wakati wa uongozi wake, Rais Nyerere akishuhudia, aliwaambia wenye mamlaka kuwa kabla ya kung’ang’ania kuwaambia wananchi kuwa mnawaletea maendeleo, muwaambie kwanza, mnataka waendelee, waende wapi? Watoto wa Ifakara ni kielelezo cha watoto wengi walioko nchi nzima.

Hawa hawakuzuka katika awamu hii yako baba! Walikuwapo hata katika awamu zilizotangulia. Lakini ni kiongozi gani anayewatilia maanani? Wamekuwa wakiongezeka kama ishara iliyo wazi kuwa kuna makosa makubwa katika kupanga vipaumbele vya taifa. Busara inauliza, kipi kianze?

Tuliambiwa na Baba wa Taifa kuwa tuna maadui watatu. Ujinga, maradhi na umaskini. Tukiri kuwa, tumeyapuuza maneno ya Baba wa Taifa. Bila sababu za msingi baadhi ya viongozi wetu wamejijengea hofu kubwa. Ikija kujulikana kuwa tuling’ang’ana na vitu huku tukiwaacha watoto wa Ifakara na wenzao nchi nzima wakiishi kwa kuchakurachakura katika majalala ya nchi hii, nachelea kusema matokeo yake yatakuwa na madhara makubwa kuliko gharika ya tsunami. Watakaokuwapo, wataiomba miamba ifunguke waingie ndani nayo iwafunike, lakini miamba itakataa!

Mwisho wetu utakuwa mchungu kuliko shubiri! Narudia kusisitiza, kufikiri mara mbili au kurudia kutafakari kwa makini kwa baadhi ya uamuzi wetu tuliyokwisha kuuchukua, kwa baadhi ya miradi tunayoihangaikia sasa, siyo ujinga. Ni kwa afya ya nchi na wananchi wetu.

Kuna baadhi ya magazeti ambayo huandika habari zao kishabiki tu. Ni kwa upofu tu wanaona wanamshabikia mtu. Lakini wanachoandika ni udhalilishaji ulioambatana na ushamba mwingi. Hatukatai kuwa ni vijana wadogo, lakini wako vijana wadogo ambao katika machapisho yao wanaonyesha busara kubwa. Hawa ni matokeo ya ubongo kutindikiwa.

Tukienda kwa wenzetu nje, wanaosoma magazeti hayo, wanatuona Watanzania wengi ni washamba. Ni bahati mbaya sana kuwa hali imejidhihirisha hivi sasa kama vile machapisho hayo, yako juu ya sheria zinazosimamia maadili katika uandishi wa habari.

Wanaosema yana baraka ya serikali tuwaache waseme kwa sababu na serikali nayo haionyeshi kukerwa na uchapishaji huu. Wenzetu ambao nao marais wao walipokewa Afrika Kusini kwenye sherehe za kumuapisha Rais mpya wakatuuliza; marais wetu wote walipokewa kwa heshima kubwa, mnajionaje nyinyi kuwa mlipokewa kifalme? Tukainamisha vichwa vyetu chini kwa aibu! Hata kama serikali haikereki kwa yanayochapishwa na vijana hawa, lakini inatakiwa iwakemee kwa sababu wanawakera wananchi wengi.

Wanadhani wanawapamba watu fulani kumbe wanawafanya watu hao waonekane dhalili ambao bila kupambwa hawawezi kusimama. Waliodhalili watawezaje kuwatoa jalalani watoto wa Ifakara na wenzao nchi nzima? Siku hazigandi.

Huko tuendako anaweza kuja kupata madaraka mtu wa watu, mwenye hofu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu akawatoa katika majalala watoto wa Ifakara na wenzao walioko katika majalala mengine katika nchi yetu. Hawa wakijashika madaraka ambayo yameshikiliwa na baadhi ya viongozi wetu wa sasa, watataka kuijua kweli kwa matukio yote ya kikatili yanayosimuliwa nchini mwetu. Madai kwamba kuna watu wanatekwa, wanateswa na kuuawa yatawekwa ukurasa wa kwanza! Hapo ndipo wahusika watakapoikimbilia milima ili iwafunike, nayo itakataa!

Wanasema patakuwa hapatoshi, lakini mimi nawaambieni kuwa hakuna jiwe litakalobaki juu ya jiwe!  Ni kweli mbinu zinatofautiana, lakini kwa mazoezi ya viungo aliyokuwa anafanya Mohamed Dewji kila siku, inatia shaka mtu anayetuhumiwa kumteka kufanikisha tukio lile aghalabu bila msaada kutoka kwa watu wengine. Na watu hao wengine huenda walisahau kuwa siku ya tukio waliwaonyesha watu ambao waliwaambia wananchi kuwa ndiyo waliomteka Mohamed Dewji. Wakasisitiza tena bila kuonyesha hati zao za kusafiria, kuwa watekaji wale hawakuwa raia wa nchi yetu.

Wawaambie wananchi huyu anayetuhumiwa ni raia wa nchi gani? Wamesahau kuwa walisema alikuwa ni dereva tu wa taksi akiwaendesha watekaji. Sasa watekaji hao waliokuwa wanaendeshwa na mtuhumiwa wako wapi? Wananchi wengi wanaweza wakapata shida ya utambuzi wa picha kwa sababu ya mfanano mkubwa wa picha zilizoonyeshwa kwenye mitandao kuwa ndiyo watekaji wa Mohamed Dewji na zile zilizoonyeshwa kutokana na tuhuma kuwa huenda marehemu Regnald Mengi aliuawa. Lakini shaka kubwa zaidi ni pale Mohamed Dewji alipoongea mwenyewe baada ya kuachiwa.

Alinukuliwa akisema, ‘’Niliwaomba wasiniue. Kama wataniua, nikawaomba wasinitupe baharini’’. Kwanini alikuwa anatumia wingi katika kusema, kama kweli alikuwa ametekwa na mtu mmoja tu?

Watoto watakapokuwa wametoka majalalani ndipo maneno yaliyosemwa bungeni na waziri wetu ndugu Harrison Mwakyembe kuwa, “Wananchi siyo mabwege’’ yatakapotimilika! Hawa watakuwa wameishinda hofu! Hawatakuwa waoga! Kama waziri amekiri bungeni kuwa walitumia kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN), kufafanua tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu nchini, watataka kujua kwanini hawakukanusha! Walionyeshwa ushahidi wakalazimika kukiri? Watataka kujua iweje Bunge la bajeti liache kujadili bajeti badala yake lijadili watu? Stephen Masele, Naibu Rais wa Bunge la Afrika, amethibitisha uwepo wa vijana jasiri wenye weledi wa kuliongoza Bunge letu vema badala ya kulitia katika aibu na fedhea! Nani atawatoa huko?