NA PASCHALLY MAYEGA
 
Ndugu Rais, kabla wewe hujawa baba nilimwandikia aliyekuwa baba yetu wote, maneno ambayo hata binti yetu Martha aliyaimba kuwa, mimi ni mpitaji tu katika hii dunia. Makao yangu yako kwa baba tu. Baba yangu kaniaandalia makao ili alipo yeye nami ndipo niwepo. Kwa hiyo mimi ulimwenguni hapa siyo kwangu. Kwangu mimi ni kwa baba tu!
Ninaishi, ninajua niko hapa kwa muda tu, makao ya milele ni mbinguni kwa baba. Magumu yanipatayo yote ni ya kitambo tu. Nyumbani kwa baba kule hakuna taabu. Nitaubeba msalaba hata kama ni kwa shida! Ninajua Yesu wangu anarudi kunitwaa!
Ndugu Rais, maneno haya yalinijia baada yakuona shamrashamra nyingi zilizokuwa zikifanyika Mwanza kwa jina la sherehe za Uhuru. Nakumbuka siku ya Uhuru mwaka 1961 Waziri Mkuu Julius Kambarage Nyerere alitupatia vikombe na sahani za plastiki wanafunzi wote tuliokuwa shuleni. Tulivyojisikia siku hiyo ni tofauti kabisa na tulivyojisikia kuona watu wazima wakihangaika Mwanza.
Siku ya kuzaliwa na mahali ulipozaliwa havina makubaliano. Tarehe uliyozaliwa ni ileile miaka yote na mahali ulipozaliwa patabaki ni palepale milele yote! Tanganyika huru ilizaliwa tarehe 9 Desemba, 1961 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ni matarajio, wakubwa wetu japo wengine walikuwa bado wadogo sana au walikuwa hata hawajazaliwa, wangeitumia siku hiyo kuwarithisha wanaokua sasa siku hiyo ilikuwaje!
Hata wakawaonyesha milingoti, ule uliokuwa ukipeperusha bendera ya Mwingereza, Union Jack, ilivyoshushwa na bendera ya Tanganyika huru ilivyopandishwa. Leo vijana wetu wanaonyeshwa uwanja wa ajabuajabu kana kwamba uhuru ulipatikana pale. Tukiendelea hivi, vizazi vijavyo havitajua Mwalimu Nyerere aliupokea Uhuru akiwa wapi.
Binti yangu akiwa kidato cha nne matokeo ya moja ya mitihani yake aliwekewa vema katika swali lililomtaka ajibu Tanzania ilipata lini uhuru, naye akajibu, tarehe 9 Desemba, 1961. Nikamtuma akamuombe mwalimu wake amuwekee kosa, kwa sababu Tanzania haikuwahi kutawaliwa, hivyo haijawahi kupata Uhuru. Tunachokifanya ni kujaribu kupotosha historia ya nchi yetu labda tukidhani kwakufanya hivyo tunajitukuza! Inauma sana!
Ziko sikukuu nyingi ambazo unaweza ukaamuru zifanyike sehemu mbalimbali  za nchi kama kutia hamasa, lakini si siku ya Uhuru wa nchi! Hii ni siku nchi ilipozaliwa!
Ndugu Rais, taifa lilishikwa na kihoro, simanzi kuu ikatawala kusikia kilio, kuwa nimekuja kushiriki sherehe za miaka 58 ya Uhuru kama uthibitisho wa ulazima wa kuwepo maridhiano, kuwepo upendo, kuwepo mshikamano katika taifa letu.
Ninawapongeza sana Watanzania kwa siku ya leo na ninamwomba Mwenyezi Mungu, siku ya leo ikafungue milango tuweze kuishi kama taifa linalopendana, tuvumiliane, tukosoane, turuhusu demokrasia, tukajenge taifa lenye upendo na mshikamano na Mheshimiwa Rais una nafasi ya kipekee, una nafasi ya kipekee kuweka historia ya maridhiano katika taifa, kwani kuna wengine wanalalamika, wengine wanaumia. Basi, mheshimiwa tumia nafasi hiyo ukaliweke taifa katika hali ya utengamano!
Kauli hii ilijaa machozi iliyozifuta furaha zote za Uhuru! Labda ilikuwa bora kupeleka kilio hiki kule Mwanza. Nchi imejaa wananchi waliojaa machozi!
Ndugu Rais, Mungu ana makusudi yake. Akitaka kumtumia mtumishi wake humjaribu kwanza kwa magumu. Ni sasa ndiyo nayaelewa mazingira ambayo Mwenyezi alinitengenezea ili atimize makusudio yake wakati ninaandika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Kama watu wanasema kuna ku-chacha, hao hawajawahi kuchacha.
Ndugu Rais, naikumbuka vema siku ile! Tulikuwa katika jumba la Sarit Centre tukiendelea na maonyesho ya vitabu, Nairobi International Bookfair. Katika banda langu alikuja mwanamwema ambaye sasa ninamwona ni aliyekuwa ametumwa na Mungu aje kuchukua hadidu za rejea ili akaitangaze ile habari njema kwa mataifa. Aliitwa Samuel Kivuitu. Alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa la Kenya. Sasa ni marehemu. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi!
Baada ya kutambulishana nilimpatia nakala moja ya kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu huku nikimsihi akishakisoma anipe mrejesho.
Kwa unyenyekevu mkubwa mtu yule aliniahidi kufanya hivyo huku akinisihi nitegemee mrejesho baada ya siku thelathini, kwa sababu alikuwa amezidiwa kazi za tume.
Amini usiamini, baba, mzee yule alichukua kitabu saa nne asubuhi na kesho yake saa nne asubuhi alikuwa bandani kwangu akiniletea mrejesho! Kwa kifupi sana aliniambia maandiko aliyokutana nayo yalikuwa ni ya muhimu ambayo yalikuwa ni lazima yafanyiwe kazi.
Akaenda, na mpaka anafikwa na mauti hatukuwahi kuwasiliana tena. Sikumbuki mahali popote Wakristu wanapoambiwa Bikira Maria alikutana tena na malaika Gabriel!
Ndugu Rais, kilichonikumbusha haya yote ni baada ya kuona kongamano kubwa mjini Nairobi lililokusanya viongozi mbalimbali wa dini na wa kitaifa ambapo Rais Uhuru Kenyatta alishikana mikono na mpinzani wake mkuu, Railla Odinga, katika The National Morning Breakfast Prayer. Walisema, walijiuliza: “Kwanini Mkenya afe kwa ajili ya uchaguzi?” Wakaamua kuwa nchi kwanza!
Ndugu Rais, katika katiba bora tatu za nchi za Afrika, Katiba ya Kenya ni mojawapo. Bado wametumia muda mwingi kuiboresha tena zaidi katiba yao baada ya kuunda tume waliyoiita BBI – Building Bridges Initiatives.
Hawataki kuona mshindi wa uchaguzi akichukua kila kitu na aliyeshindwa kupoteza kila kitu. Wanataka walioshindwa wajumuishwe katika ujenzi wa taifa lao na katika kuifaidi keki ya taifa lao! Hivi ndivyo iliyvoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu. Nilijawa faraja kubwa kifuani mwangu baada yakuona mapendekezo ya katiba mpya yamechukuliwa kama yalivyo ya BBI.  Na mengine wameyachukua neno kwa neno!
Ah! Baba Rais, walisema: “Ni chema gani kinaweza kutoka Nazareti!” Yakipitishwa mapendekezo ya BBI, Kenya itakuwa ndiyo nchi ya amani kubwa katika Afrika kwa kuyatumia vema maandiko yaliyomo katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu! Mawazo yaliyoasisiwa kutoka Mbagala nchini mwetu!
Huwa ninarudiarudia kukisoma hiki kitabu. Ajabu ni kwamba kila ninaporudia hukutana na sentensi zinazonilazimisha kujiuliza, nilizipata wapi hizi?
Baba Rais wangu imeandikwa, jiwe walilolikataa waashi hapa kwetu Tanzania ndilo limekuwa jiwe kuu la pembeni nchini Kenya.
 
 
Mwisho