Ndugu Rais, bendi ya muziki ina ala nyingi. Wakati mwingine muziki unapigwa tangu mwanzo hadi mwisho na msikilizaji asisikie ala fulani ikijitokeza.

Baba Phillip Mangula ni mtu wa pili kwa nguvu katika Chama chetu Cha Mapinduzi. Lakini chama na serikali kama bendi vinapotumbuiza husikika mara chache sana. 

Tulimsikia kule Butiama wakati wa kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwafahamisha Watanzania jambo gumu. Aliwaambia Watanzania kuwa viongozi wote walioingia uongozini tangu wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi hawajapatiwa mafunzo ili wawe viongozi bora. Hawajaenda mafunzoni kufundwa. Hivyo viongozi tulionao sasa kila mtu hubuni utaratibu wake mwenyewe katika kuongoza nchi.

Kauli sononeshi na ya kuhuzunisha sana lakini ya ukweli. Makamu Mwenyekiti anathibitisha kuwa Watanzania wanaongozwa kwa kupuyanga tu.

Uchaguzi wa serikali za mitaa umekuja kama kuthibitisha maneno ya makamu mwenyekiti huyo. Uso wa nchi hivi sasa umejaa aibu kwa kile kinachoonekana kama hofu ya CCM kwa uchaguzi huo. Malalamiko nchi nzima lazima yatakuwa ni matokeo ya utendaji kazi usioridhisha wa viongozi ambao hawajafundwa. Kila kiongozi anabuni njia yake mwenyewe ya kuongoza nchi.

Baba Bashiru, sababu zinazotolewa na watendaji wa serikali unayoisimamia hata kama ni utoto, zimepitiliza. Mgombea timamu anajua kuwa P. O. Box (Boksi au sanduku la ofisi ya Posta) na S. L. P (Sanduku la Posta) maana ni ileile. 

Lakini mtu anayeamua kuandika P. O. Box au S.L.P. ni sababu tosha kweli ya kumuengua kuwa hawezi kuwa mjumbe wa mtaa au kuwa mwenyekiti wa kitongoji?

Baba Bashiru pamoja na usomi wako usiotiliwa shaka na kwa fikra zako mwenyewe kumbuka kuwa umejijengea heshima kubwa ndani na nje. Jitofautishe na watu ambao upeo wao wa kufikiri ni mdogo mno.

Ndani ya chama mambo hayajakaa sawa. Kinana angesema ni mzigo wa chama. Imeandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu kuwa: “Ujuzi ni mwalimu mzuri kuliko elimu. Ushindi wa nguvu hauwezi kuisuluhisha mioyo ya wananchi, bali utazidi kuivimbisha na kutafuta kisasi. Vita ni mbaya kwa aliyeshindwa, maana hupata hasara kubwa. Pia vita ni mbaya kwa anayeshinda, maana huandamwa na kisasi siku zote za maisha yake’’.

Baba Bashiru Ally ukiwa ukingali mpya, ulitamka neno lenye busara kubwa kuwa: “CCM kama tutakuwa tumejenga shule za kutosha zinazoonekana zikiwa na vitabu bora, vifaa vya kufundishia na walimu wenye ari na kama tutakuwa tumejenga zahanati za kutosha zinazoonekana zikiwa na dawa na vifaatiba na madaktari na wauguzi wenye ari, tutaogopa nini kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020?”

Ulitufariji sana vijana wako na wananchi wote kwa ujumla. Tukajimwambafai kuwa CCM ni chama makini sana. Imekata mti kuondoka Abdulrahman Kinana na sasa imepanda mti kumuingiza Bashiru Ally. Ulikuwa bado mpya. Fikra zako zikashabihiana na zile zilizowahi kutolewa na kionambali aliyesema: “Tutaanza kwa kujenga sekondari kwa kila kata. Tukimaliza, tutajenga zahanati kwa kila kata.”

Wosia wa Baba wa Taifa ni kwamba maadui wetu ni watatu; ujinga, maradhi na umaskini. Ukifaulu kumpiga vita adui ujinga, hao wengine watakimbia wenyewe. Kama si wakora, wangemwacha Edward atekeleze mawazo yake hayo, hakika maisha bora kwa kila Mtanzania yangekuwa.

Baba Bashiru, umekuwa muumini mzuri wa fikra za Baba wa Taifa. Mpaka leo zinarudiwarudiwa katika mitandao zikiwaimarisha Watanzania. Anasema, kujenga tu barabara ya lami si maendeleo. Kujenga tu majengo marefu si maendeleo. Anasema maendeleo lazima yawe ni yale yanayowagusa watu. Na watu wetu akasema ni wakulima. Hivyo maendeleo ni lazima yawe ya kuendeleza kilimo na wakulima. Bashiru sitaki niseme mimi, sema wewe mwenzao na muulizane iwapo haya makubwa mnayoyafanya katika nchi yanagusa watu?

Kuwa mkweli, kwa fikra za Baba wa Taifa angeyaita haya kuwa ni maendeleo? Anasema watu wetu ni wakulima, yanawagusa?

Ndugu Abdulrahman Kinana alipokwenda Rufiji hakupata wazo la umeme kama ambavyo Baba wa Taifa naye hakuwa na wazo hilo. Alijua kwa gesi nyingi tuliyonayo na miundo iliyo tayari tukiingiza hapo fedha kidogo tu kati ya hizi nyingi tulizonazo, tutakuwa na umeme wote tunaouhitaji. Tutakuwa na wakuuza nje na kubakiwa na ziada ya kumwaga. Lakini kwa umimi, tunaweza kujimwambafai kwa gesi ambayo sisi si waanzilishi?

Kinana alikusanya vijana wote ambao walikuwa hawana kazi akawafungulia mashamba walime. Nyerere alisema wananchi wetu ni wakulima. Kama pesa nyingi hizi tulizonazo tungewakusanya vijana, tukawawezesha, tukawafungulia mashamba walime kilimo cha kisasa, shida za wananchi zingetoka wapi? Kijana gani angekuja mjini kubangaiza kwa kukosa kazi? Maisha bora kwa kila Mtanzania inawezekana tu kama viongozi wetu wataacha kutaka kujimwambafai!

Baba Bashiru uliwataka viongozi waende vijijini kwa wananchi wakatoe elimu. Wakawaeleweshe wananchi mpaka waelewe hii miradi mikubwa inayofanyika nchini ina faida gani kwao.  Malango yako yabarikiwe. Bashiru wananchi wamepigika zaidi sasa fedha nyingi zinapoonekana kuzagaa kuliko walipokuwa wanaambiwa nchi ni maskini huku wanaibiwa.

Watume hao viongozi waende mpaka Vingunguti, Gongo la Mboto na Ukonga ambako wananchi wake wanazaliwa, wanakuwa na wanazeeka wakiwa wanaziona ndege za kila saizi kwa macho yao, zikitua na kupaa. Wakawaeleweshe hao mpaka waelewe, wanaokwenda uwanja wa ndege kushangaa ndege mpya kuna faida gani kwao?

Nimezaliwa Mkonko kijijini. Mpaka ninakua sikujua kama ndege ina matairi. Zilikuwa zikipita mbinguni matairi yakiwa tumboni.  Mzaliwa wa Vingunguti akiniita mshamba ninapokwenda kushangaa ndege mpya, hanitukani. Ananiambia ukweli. Kwa namna mwanadamu alivyoumbwa na Mungu, na kwa sababu jicho halijitazami, akiwa na uwezo japo kidogo, anaweza kwa ushamba wake akawaumiza watu wengi.