Ndugu Rais, sasa naanza kuwaelewa wanawema wengi wanaosema mengi yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu au ni utabiri au ni unabii! Tumwachie Muumba afanye kazi yake.
Unaweza pia ukawa mfano wa mcheza bao hodari! Nasukumwa sasa kuwaelewa vema, kutokana na hotuba yako makini uliyoitoa ulipokuwa ukipokea ripoti ya pili ya makinikia. Ilikuwa ni hotuba iliyogusa wengi na kuumiza roho za Watanzania masikini. Uliyasema kama yalivyoandikwa katika ukurasa wa 103 wa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Maandiko ambayo yaliandikwa zaidi ya miaka kumi iliyopita. Kama viongozi wetu wangeyasoma kisha wakatafakari na wakayazingatia, Watanzania wasingeumizwa pakubwa hivi. Ndugu Rais, yaonekana umeyasoma, ukayatafakari na sasa unayafanyia kazi kwa maslahi ya nchi hii na watu wake. Kwa hili, baba, Mwenyezi Mungu akutangulie! Wezi wetu wenyewe walipoulizwa kwanini nchi yetu yenye raslimali nyingi kiasi hiki ni masikini, walijibu kilofa tu kuwa hata wao hawajui! Kumbe wao na familia zao ndiyo chanzo cha umasikini wa watu wa nchi hii! Tuombe Mungu awe amesikia kilio cha masikini wa nchi hii na sasa ameamua kuwajibia kupitia kwako baba!

Waliotutangulia walisema hakuna makali yasiyokuwa na ncha ndiyo maana sasa kuna kila dalili kuonyesha kuwa siku za wezi zimekwisha! Wakati wa kampeni nyinyi watatu mliomaliza vema mbio za urais mwaka 2015 mlikuwa na uchungu uliofanana. Hata kabla hujawa rais ulinukuliwa ukisema; “Kwani Watanzania hapa tunashindwa kutengeneza ‘smelter’ yenye temperature ya 1,500 ambayo ndicho kiwango cha juu cha joto la kuyeyushia shaba, fedha yakawa yanatoka tu huko kama maji”.
Naye akiwa katika kampeni kugombea urais mwaka 2015 kule Geita, Edward Lowassa alisema; “Kuna malalamiko mengi. Nikiingia madarakani nitaunda tume ya kuchunguza jambo hili, ili nihakikishe tunapata zaidi kuliko mgeni.
Pale ambapo mkataba umempendelea mgeni, nitaufutilia mbali na kuanza upya.”

Ana Mghwira aliwazidi wote kwa kuwa yeye alikuja na Azimio la Arusha. Azimio la Arusha ndiyo mwarobaini pekee. Kama manyang’au hawa wasingeliua Azimio la Arusha ufisadi huu usingetokea.
Ndugu Rais, kutambua tatizo ni jambo moja, lakini kutatua tatizo ni jambo lingine tofauti! Kama mpaka hapa tunaposoma maandiko haya waliotajwa na tume bado wanatembea barabarani, basi ole wetu tuliolianzisha! Nani asiyejua kuwa Rais Mstaafu hashitakiwi mahakamani? Lakini ni sheria ipi inayokataza Rais Mstaafu hata kuulizwa tu barabarani kile anachokijua? Wananchi wamejaa upepo!

Wakiachwa waamue wenyewe, adhabu yao ni kali na inatisha kama nini!
Imeelezwa katika ukurasa wa 22 wa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu kuwa; “Wananchi wenye hasira watayatongoa macho yao kwa ncha za vidole vyao na watayachana mapafu yao kwa kucha zao. Watakaonusurika watatawanyika katika pembe zote za dunia na kutangatanga kama kondoo wasio na mchungaji. Mume hatajua mke aliko, vivyo hivyo mke hatajua mume au mwana aliko! Huo ndiyo utakuwa ndiyo mwanzo na mwisho wao!”
Ndugu Rais katika simulizi hilo ukurasa wa 96 imeandikwa kuwa aliyekuwa wa kwanza kukamatwa alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Alipoitwa mheshimiwa alijibu; “Ndugu zangu naomba mniite ndugu, mimi siyo mheshimiwa. Mimi ni mwenzenu, ndugu yenu…Nyinyi sasa mmekwisha kuamka. Hamtakubali kudanganywa tena. Tuliwaona wananchi ni wajinga kumbe sisi viongozi ndiyo tulikuwa wajinga kwa kujiona tuna dola tukadhani tuna kila kitu na tukaipuuza nguvu ya wananchi. Lakini haya yangu madogo. Wenzangu wana makubwa ya kutisha. Madhali mmechachamaa, madhambi ya wakubwa yatafumuka na kujitokeza hadharani. Nawaambia hamtayaamini macho na masikio yenu. Chondechonde, msije mkajikuta mnawafukia wakiwa hai!”

Ndugu Rais, walisema kama leo haitoshi, kweli, itashinda kesho! Leo Watanzania wameanza kuwajua nani ni fisadi halisi wa nchi hii!
Aliyemtegemea Mungu wake pale alipochafuliwa na mafisadi halisi, sasa anatembea kifua mbele, mweupe kama theluji! Kweli kwa Mungu hakuna kinachoshindikana.
Ndugu Rais, umethibitisha pasipo shaka yaliyoandikwa katika ukurasa wa 103.“Tunataka Rais atambue kuwa utajiri mkubwa wa nchi hii, dhahabu na madini mengine walimilikishwa wageni. Wameachiwa wachimbe. Wapeleke kwao kiasi chochote watakacho, sisi watupatie mrabaha wa asilimia duni tu ya kile wanachotaka kutuambia kuwa wamechukua, kisha wakimaliza watuachie mashimo na mapango ya kutisha pamoja na milima ya mchanga uliotoka ardhini. Huo ndiyo urithi kwa vizazi vyetu.

Wananchi wa kawaida wanapoiona hali hii na viongozi wao wapo na wanaiona, lakini si tu hawafanyi chochote kuizuia bali wameridhia, unadhani wanasemaje? Lazima wanasema viongozi wetu ni sehemu ya waporaji hao. Ndiyo, kumbe wasemeje? Siku ikifika watacharukiwa wote.”
Aidha, imethibitika jinsi Bunge letu lilivyotumika vibaya na mafisadi.

Spika wa Bunge alipopewa nafasi tulitarajia angeonyesha uadilifu kwa kuwaomba radhi Watanzania kwa kuidhinisha sheria za kidhalimu. Badala yake amekubali aibu zirudishwe katika Bunge lilelile zikarekebishwe.
Unakula matapishi yako! Kwa mtu mwadilifu kabisa kabisa Spika angeonyesha ukomavu akawapisha wengine ndiyo wazirekebishe!
Imeandikwa katika ukurasa wa 16; “Spika wa Bunge kuwa mwanachama wa chama cha siasa imekuwa ni sababu tosha ya mijadala ya kisiasa na uchama bungeni. Baadhi ya wabunge wachovu wameligeuza Bunge kuwa jukwaa la kusisitiza jinsi walivyo waaminifu kwa serikali na kwa rais.

Wanapumbazwa na tamaa ya kuchaguliwa kuwa mawaziri au kuwekwa kwenye sehemu zenye maslahi zaidi. Wanaegemea upande wa serikali na kusahau majukumu yao ya kulinda demokrasia na haki za wananchi. Wanaodhani chama chao kitatawala mpaka Yesu atakaporudi hawajasoma historia.
“Bunge letu ambalo ndilo ndicho chombo pekee cha kutunga na kufuta sheria lilitakiwa liwe ndilo mwakilishi pekee wa wananchi. Serikali inaundwa na watu ili iwatumikie kwa namna wanavyotaka. Kwa kuwa Bunge ndio uwakilishi wa watu hao, basi kwa maana hiyo Bunge liko juu ya Serikali kwa mantiki ya demokrasia ya uwakilishi”.
Ndugu Rais, katika hili wananchi wanapaswa kuacha tofauti zao wakasema nchi yangu kwanza. Na wewe baba, tengue sasa kauli yako ya kupiga marufuku maandamano ili wananchi waandamane nchi nzima, dunia ijue kuwa jambo hili limewagusa Watanzania wote!